Kanisa lina matumaini na vijana wa Angola. Kanisa lina matumaini na vijana wa Angola. 

Kardinali Filoni: Kanisa lina matumaini na vijana wa Angola!

Kardinali Filoni amewataka vijana wa Angola kukataa kishawishi cha kutumbukizwa katika ukabila na udini; uchawi na ushirikina; na badala yake waambate tunu msingi za Kiinjili, mambo yanayohitaji malezi na majiundo makini yanayopaswa kutolewa na mihimili ya uinjilishaji nchini Angola.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu anaendelea na ziara yake ya kichungaji nchini Angola kama sehemu ya kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, Sao Tome na Principe, CEAST. Kardinali Filoni, Jumatatu jioni, tarehe 12 Novemba 2018 amekutana na kuzungumza na vijana wa kizazi kipya kutoka Jimbo Kuu la Saurimo, Angola na kuwataka vijana kutoka kifua mbele ili kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa, changamoto iliyotolewa na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa Mwaka 2018 iliyohitimishwa hivi karibuni.

Kardinali Filoni amewataka vijana kujiunga na vyama vya kitume ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa njia ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Vijana wajisikie kuwa ni sehemu ya mitume wamisionari wanaotumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, changamoto inayohitaji wongofu wa kimisionari kutoka kwa viongozi wa Kanisa. Vijana watambue na kuheshimu dhamana waliojitwalia wakati walipopokea Sakramenti ya Ubatizo kwani watambue kwamba, wanashiriki: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo, wanaopaswa kuutolea ushuhuda katika maisha, lakini kwanza kwa kuimarisha mahusiano na mafungamano na Kristo Yesu kwa njia ya: Sala na Sakramenti za Kanisa.

Amewataka vijana wa Angola kutokubali kumezwa na malimwengu, bali wasimame imara katika imani, matumaini na mapendo kwa Kristo na Kanisa lake. Amewataka vijana kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya upendo; kwa kuhakikisha kwamba, wanakuwa na vipaumbele katika maisha yao, tayari kuvifanyia kazi, kwa kuzingatia kanuni, sheria, tartibu na tunu msingi za kimaadili na kiutu. Amewataka vijana wa Angola kukataa kishawishi cha kutumbukizwa katika ukabila na udini; uchawi na ushirikina; na badala yake waambate tunu msingi za Kiinjili, mambo yanayohitaji malezi na majiundo makini yanayopaswa kutolewa na mihimili ya uinjilishaji nchini Angola. Malezi na makuzi endelevu wanaweza kuyapata ikiwa kama watashiriki kikamilifu katika vyama na mashirika ya kitume ndani ya Kanisa nchini Angola!

Kardinali Filoni akizungumza na Wakleri wa Jimbo kuu la Saurimo amewakumbusha kwamba, Mwezi Oktoba 2019 kitakuwa ni kipindi maalum sana kwa maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Utakuwa ni muda wa kusali na kutafakari utume kama msingi wa mchakato mzima wa uinjilishaji mpya unaotekelezwa na Mama Kanisa. Kwa hakika hiki ni kipindi cha ushuhuda wa  huruma ya Mungu inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Mwezi Oktoba 2019 Kanisa litakuwa linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Benedikto XV alipochapisha Waraka wa Kitume"Maximum Illud" yaani “Kuhusu Shughuli za Kimisionari.” Ni muda wa: sala, katakesi, tafakari na matendo ya huruma! Ni wakati muafaka kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanatelekeza vyema dhamana na wajibu waliojitwaliwa kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo inayowashirikisha: Unabii, Ukuhani na Ufalme wa Kristo. Waamini wakiwa wamezaliwa kwa “Maji na Roho Mtakatifu”, wanawajibu wa kukiri na kutangaza imani ambayo wameipokea kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kanisa na hivyo kushiriki katika utendaji wa kitume na wa kimisionari wa Taifa la Mungu.  

Kardinali Fernando Filoni, anasema, Kanisa linahitaji kupyaishwa daima kutoka katika undani wa maisha na utume wake kwa njia ya: toba na wongofu wa ndani, unaofanywa na watoto wa Kanisa. Kwa moyo unaowaka mapendo, Kanisa litaendelea: kupenda, kutangaza, kushuhudia na kuhudumia watu wote! Anasema, tarehe 30 Novemba 2019, Kanisa litakuwa linaadhimisha Jubilei ya miaka 100 tangu Papa Benedikto XV alipochapisha Waraka wa Kitume “Maximum Illud” unaopembua mchakato mzima wa shughuli za kimissionari zinazotekelezwa na Mama Kanisa. Ameweataka wakleri nchini Angola kujitahidi kuyaisha mashauri ya Kiinjili ambayo ni: Ufukara, Utii na Useja kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Ufalme wa Mungu ndani na nje ya Angola, tayari kupyaisha maisha na utume wa Kanisa la Kristo nchini humo!

Kardinali Filoni: Vijana
14 November 2018, 14:11