Tafuta

Vatican News
Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, Sao Tome na Principe mwaka 2018 linaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, Sao Tome na Principe mwaka 2018 linaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. 

Kardinali Filoni mgeni rasmi Jubilei ya Miaka 50 ya CEAST, Angola

Tarehe 18 Novemba 2018, Siku ya Maskini Duniani, kitakuwa ni kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Angola Sao Tome na Principe, CEAST. Kardinali Filoni ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, atakutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu kuanzia tarehe 10- 20 Novemba 2018 anafanya safari ya kitume nchini Angola, Sao Tome na Principe, kama sehemu ya hitimisho la maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, Sao Tome na Principe, CEAST., kunako mwaka 1967.

Mwanzoni, Msumbiji, pia ilikuwa ni sehemu ya Baraza la Maaskofu Katoliki CEAST kabla ya mwaka 1967. Angola ina Majimbo makuu 5 yanayoundwa na Majimbo 14. Sao Tomè ina jimbo moja tu! Kardinali Filoni, anatarajia kukutana na kuzungumza na watawa, wakleri na waamini walei pamoja na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa makundi mbali mbali nchini Angola.

Akiwa nchini Angola, Kardinali Filoni atakutana na kuzungumza na Rais João Manuel Gonçalves Lourenço, Rais wa awamu ya tatu, aliyeanza kushika madaraka tarehe 26 Septemba 2017. Atapata nafasi pia ya kuzungumza na wanajumuiya kutoka katika nyumba za malezi nchini Angola, hasa wakati huu, Mama Kanisa anapoendelea kujikita katika utekelezaji wa mwongozo wa malezi ya kipadre unaotoa mwelekeo na uwiano sahihi wa malezi: kiutu, kiroho, kiakili na kichungaji kwa njia ya safari ya malezi na majiundo makini ya Kipadre, taratibu, lakini kila jandokasisi akiangaliwa kwa jicho la pekee.

Tarehe 18 Novemba 2018, Siku ya II ya Maskini Duniani, kitakuwa ni kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, Sao Tome na Principe, CEAST. Kardinali Filoni ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, atakutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu. Mwishoni mwa ziara yake ya kikazi, Kardinali Filoni atapata nafasi ya kutembelea maeneo mbali mbali ya Sao Tome na Principe.

Kardinali Filoni: Angola

 

 

10 November 2018, 15:00