Kardinali Filoni: Dumisheni ari na mwamko wa kimisionari ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili Kardinali Filoni: Dumisheni ari na mwamko wa kimisionari ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili 

Kardinali Filoni: Dumisheni ari na mwamko wa kimisionari!

Sao Tome kwa sasa imeanza mchakato wa maandalizi ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Uinjilishaji Kisiwani hapo itakayofikia kilele chake kunako mwaka 2030, maadhimisho ambayo tayari yalipangiwa mikakati tangu mwaka 2014. Waamini wanatakiwa kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu wakati wa ziara yake ya kichungaji nchini Angola kuanzia tarehe 10 - 20 Novemba 2018 kama sehemu ya kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, Sao Tome na Principe, CEAST, amehitimisha kwa kutembelea Sao Tome inayohudumiwa na Maaskofu wawili na kati yao, mmoja ameng’atuka kutoka madarakani na kuna mapadre 13, watawa 31 na makatekista 472 wanaosimamia maisha na utume wa Kanisa kwenye Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo!

Kardinali Filoni, ameitaka familia ya Mungu Sao Tome kuhakikisha kwamba, inajizatiti katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, daima ikijitahidi kujenga na kudumisha umoja katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji. Sao Tome kwa sasa imeanza mchakato wa maandalizi ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Uinjilishaji Kisiwani hapo itakayofikia kilele chake kunako mwaka 2030, maadhimisho ambayo tayari yalipangiwa mikakati tangu mwaka 2014. Waamini wanatakiwa kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo.

Waamini wajenge na kuimarisha moyo na utamaduni wa maisha ya sala, tafakari ya Neno la Mungu na ushiriki mkamilifu wa Sakramenti za Kanisa kama njia ya kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu katika maisha yao, chachu muhimu sana katika mchakato mzima wa uinjilishaji. Wakleri wanapaswa kutambua kwamba, wao ni sehemu muhimu sana ya mchakato wa uinjilishaji, wanapaswa kukita maisha yao katika tafakari ya kina katika Maandiko Matakatifu, ili Neno liweze kupyaisha maisha yao, kwa njia ya wongofu wa kimisionari, ili waweze kuwa ni mitume wamisionari, wanaotangaza na kushuhudia furaha ya Injili kati ya watu wa Mataifa.

Kardinali Filoni anasema mambo makuu ya kuzingatia katika maisha na utume wa watawa ni: ufukara wa kiinjili, maisha ya sala na uvumilivu katika utekelezaji wa sera na mikakati ya shughuli za kichungaji mintarafu karama ya mashirika yao. Kanisa linatambua kwa namna ya pekee kabisa mchango unaotolewa na Makatekista Barani Afrika, katika kuwatayarisha Wakatekumeni ili kuweza kupokea Sakramenti mbali mbali za Kanisa. Wao ni nuru inayong’aa mbele ya waamini ili kuweza kumtukuza Mwenyezi Mungu. Ni wadau wakuu wa Uinjilishaji, ni watu ambao wamejitoa kimasomaso kuwainjilisha ndugu zao katika Kristo. Dhamana hii inapaswa kutekelezwa kwa ari na moyo mkuu zaidi. Makatekista wanapaswa kuandaliwa barabara ili waweze kutekeza dhamana na wajibu wao ndani ya Kanisa. Majiundo haya yaguse mambo ya kiakili, mafundisho tanzu ya Kanisa, maadili na shughuli za kichungaji pamoja na kulinda heshima na utu wa Makatekista; washughulikie mahitaji yao na familia zao, wapewe ujira au posho inayostahili.

 Makatekista kwa upande wao, wanapaswa kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika maisha na utume wao; watu wanaoheshimika na kuaminika katika jamii; Wakarimu na watu wenye maadili mema. Kwani, kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao, wataweza kutoa katekesi ya kina inayomgusa mkatekumeni katika undani wake; wataweza kuwa ni viongozi hodari wa vikundi vya sala pamoja na maadhimisho ya Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo.

Kimsingi wao ni wasaidizi wakuu wa mapadri kwenye parokia na vigango wanavyohudumia. Huu ni utume endelevu, stahimilivu na chanzo cha uvuvio na kamwe wasijikite katika ubinafsi unaoweza kuvuruga jitihada zote hizi. Makatekista wanapaswa kuwa waaminifu katika maisha na utume wao kwa Kristo na Kanisa lake, ili kuchangia kwa namna ya pekee kabisa, utakatifu wa maisha unaohitajika kwa ajili ya ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.

Kardinali Fernando Filoni, amelitaka Kanisa  Angola na Sao Tome, daima lijitahidi kujenga na kuimarisha umoja na mafungamano na vijana, kwa kuandamana na kukaa nao, ili kuwasaidia kung’amua maisha yao; kutafsiri matukio mbali mbali katika mwanga wa Maandiko Matakatifu na hatimaye, kufanya maamuzi magumu ambayo watapaswa kuyatekeleza haraka, kwa kushirikishana mang’amuzi yao baada ya kukutana na Kristo Mfufuka kama ilivyokuwa kwa wanafunzi wa Emau.

Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, amekazia ushiriki mkamilifu katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho kuwa ni muhimu sana katika maisha ya vijana. Waguswe na kuvutwa na Kristo Yesu, ili wawe tayari kuitwa na kutumwa kwenda kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili. Vijana watambue na kuthamini vipaumbele katika maisha yao, wakijitahidi kuwa imara katika imani, ili wasitumbukizwe katika ukoloni mambo leo na utamaduni wa kifo. Vijana wawe ni wajenzi na mashuhuda wa utamaduni wa umoja, mshikamano na upatanisho wa kitaifa.

Filoni: Sao Tome
21 November 2018, 11:30