Vatican News
Kardinali Fernando Filoni na  Rais João Lourenço wa Angola Kardinali Fernando Filoni na Rais João Lourenço wa Angola 

Vyama na mashirika ya kitume ni muhimu katika uinjilishaji nchini Angola

Vyama vya kitume ni kama shule ya imani, matumaini na mapendo. Hapa ni mahali ambapo waamini wanaweza kusaidiana katika: imani, maisha ya kisakramenti, maadili na sala. Karama ni zawadi ya Roho Mtakatifu kwa waamini ndani ya Kanisa, tukio ambalo ni endelevu katika maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Vyama vya kitume vilivyoibuka baada ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, ni zawadi kubwa kwa Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Vinapaswa kupokelewa kwa imani na moyo wa shukrani, kama rasilimali kwa Kanisa, ili hatimaye, viweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika maisha yao. Kanisa nchini Angola linapaswa kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili. Kanisa linathamini sana mchango wa watawa wa ndani katika maisha na utume wa Kanisa hasa katika mchakato wa uinjilishaji.

Waamini walei nchini Angola, Sao Tomè na Principe wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanakuwa shupavu na wajasiri katika kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, kwa njia ya matendo adili, yenye mashiko na mguso kwa wale wanaowazunguka. Ikumbukwe kwamba, vyama vya kitume ni kama shule ya imani, matumaini na mapendo. Hapa ni mahali ambapo waamini wanaweza kusaidiana katika: imani, maisha ya kisakramenti, maadili na sala. Karama ni zawadi ya Roho Mtakatifu kwa waamini ndani ya Kanisa, tukio ambalo ni endelevu linalowapatia changamoto wahusika, kuzitumia karama hizi kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya Kanisa kadiri ya busara na hekima ya viongozi wa Kanisa.

Hayo yamebanishwa na Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu wakati wa ziara yake ya kichungaji nchini Angola kuanzia tarehe 10 - 20 Novemba 2018 kama sehemu ya kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, Sao Tome na Principe, CEAST. Anasema, vyama vya kitume vinapaswa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kwa kutambua kwamba, waamini walei wana mchango mkubwa katika ujenzi wa Kanisa la Kristo kwa kushirikiana na wakleri pamoja na watawa. Vyama vya kitume, vijenge na kudumisha utamaduni wa kushika sheria, kanuni na miongozo inyotolewa na Maaskofu mahalia, ili kujenga na kuimarisha umoja, upendo, mshikamano.

Ikumbukwe kwamba, ustawi wa Kanisa la Kristo huanzia ndani ya familia, jumuiya ndogo ndogo za kikristo, vigango, parokia, jimbo na Kanisa katika ujumla wake. Ikiwa kama vyama vya kitume vitashindwa kufuata sheria, kanuni na taratibu, Kanisa linaweza kujikuta likiogelea katika kinzani na migogoro isiyokuwa na tija hata kidogo! Kardinali Filoni anakaza kusema, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na wongofu wa kimisionari katika maisha na utume wa Kanisa, ili kuzaa matunda yanayokusudia sanjari na kupyaisha sera na mikakati ya shughuli za kimisionari nchini Angola. Kanisa linaendelea kuwahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya maadhimisho ya Mwezi Oktoba 2019 uliotengwa maalum kwa ajili ya kuhamasisha ari na mwamko wa kimisionari duniani.

Kuna haja ya kudumisha majiundo makini; umuhimu wa tafakari ya Neno la Mungu; vigezo muhimu kwa Jumuiya ya Kimonaki kuweza kujitegemea pamoja na uwezekano wa kuunda Shirikisho la Wamonaki ndani ya Kanisa. Haya ni kati ya mambo ambayo Baba Mtakatifu Francisko anayapatia kipaumbele cha pekee katika Katiba ya Kitume “Vultum Dei Quaerere” Yaani “Kuutafuta Uso wa Mungu” iliyotiwa mkwaju na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2016 kwa ajili ya Wamonaki wa Mashirika ya Taamuli.

Katika Waraka huo, Baba Mtakatifu anasema, kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika historia na maisha ya mwanadamu katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, tangu Kanisa lilipoadhimisha Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Lengo la Waraka huu ni kuendeleza majadiliano na walimwengu, kwa kuzingatia tunu msingi za maisha ya taamuli yanayojikita kwa namna ya pekee katika: Ukimya, Usikivu na Udumifu; mambo ambayo yanapaswa kukabiliana na changamoto mamboleo. Baba Mtakatifu katika utangulizi wa Waraka huu anaonesha umuhimu wa maisha ya taamuli ndani ya Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake.

Umuhimu wa Maisha ya Taamuli: Baba Mtakatifu Francisko anasema, walimwengu wanaendelea kuutafuta Uso wa Mungu na watawa kwa namna ya pekee wamekuwa ni mfano bora wa kuigwa ili kufahamu maswali na majibu yanayoulizwa na mwanadamu pamoja na Mwenyezi Mungu, changamoto endelevu katika maisha ya watu. Baba Mtakatifu anawasifu na kuwapongeza watawa wa Maisha ya Taamuli kwa kuonesha kwamba, Kanisa linawategemea katika mchakato wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu kati ya watu wa Mataifa.

Utume huu unakabiliwa na changamoto kubwa zinazofumbatwa katika: uchu wa mali na madaraka; faida za kiuchumi pamoja na ulaji wa kupindukia. Lakini watawa wanapaswa kuwa ni mwanga unaowaangazia walimwengu katika safari ya kumtafuta Kristo aliye njia, ukweli na uzima. Maisha ya Taamuli ni muhimu sana katika utume wa Kanisa na wala hayana mbadala. Maisha ya kuwekwa wakfu ni historia ya upendo wa Kristo kwa ajili ya walimwengu, upendo unaowahamasisha watu kuutafuta Uso wa Mungu kwa kutumia jicho la kiroho linalowawezesha kuutafakari ulimwengu na mambo yake kwa jicho la Kimungu. Baba Mtakatifu anawataka Wamonaki kujifunga kibwebwe kupambana na changamoto zinaoweza kujitokeza kutokana na mazoea ya kila siku, kwa kukosa hamasa na hatimaye kupoteza dira na mwelekeo wa maisha ya kitawa.

Baba Mtakatifu anatoa Tema 12 za kufanyiwa tafakari na mang’amuzi: Majiundo na sala;  Neno la Mungu, Ekaristi Takatifu na Upatanisho; Maisha ya kidugu ndani ya Jumuiya; Uhuru na Shirikisho; Maisha ya ndani, Kazi na Ukimya; Njia za Mawasiliano ya Jamii na Kiasi. Majiundo na Sala: Baba Mtakatifu anawaalika Wamonaki kufanya tafakari na mang’amuzi ya kina kuhusu tema 12 za maisha ya kitawa katika ujumla wake na kuchunguza kwa karibu zaidi Mapokeo ya Kimonaki, ili kuwasaidia watawa wa maisha ya Kitaamuli kuweza kufikia lengo la wito wa maisha yao.

Vyama vya Kitume Angola

 

 

19 November 2018, 13:13