Tafuta

Vatican News
Kitengo cha CHARIS kuzinduliwa rasmi tarehe 8 Desemba 2018, ili kuratibu shughuli za Karismatiki Wakatoliki Kimataifa. Kitengo cha CHARIS kuzinduliwa rasmi tarehe 8 Desemba 2018, ili kuratibu shughuli za Karismatiki Wakatoliki Kimataifa. 

Kitengo cha CHARIS kuratibu huduma ya Wakarismatiki Kimataifa

CHARIS ni kitengo kitakachokua kinatoa huduma ya kimataifa kwa Chama cha Kitume cha Wakarismatiki Wakatolik. CHARIS kinatarajiwa kuzinduliwa rasmi tarehe 8 Desemba 2018, Mama Kanisa atakapokua anaadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha limeanzisha kitengo maalum kijulikanacho kama “CHARIS” katika asili yake, neno hili maana yake ni “neema au zawadi maalum kutoka kwa Roho Mtakatifu”. Kwa sasa hiki ni kitengo kitakachokuwa kinatoa huduma ya kimataifa kwa Chama cha Kitume cha Wakarismatiki  Wakatoliki na kinatarajiwa kuzinduliwa rasmi tarehe 8 Desemba 2018, Mama Kanisa atakapokua anaadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Hii itakuwa ni siku ya kuzindua rasmi Katiba itakatosimamia shughuli za kitengo hiki kama dira na mwongozo wa kusimamia na kukuza imani ya Kanisa Katoliki. Zote hizi ni kazi za Roho Mtakatifu zinazoendelea kupyaisha maisha na utume wa Kanisa.

Kimsingi kitengo hiki, hakitakuwa na mamlaka juu ya Chama cha Wakarismatiki Wakatoliki, bali wataendelea kutekeleza dhamana na shughuli zao kama kawaida, chini ya usimamizi wa Maaskofu mahalia. Kila tawi linaweza kupata huduma na msaada wa kiufundi utakaokuwa unatolewa na CHARIS sehemu mbali mbali za dunia. Katiba hii itaanza kutekelezwa kwa majaribio baada ya Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kumteua Professa Jean –Luc Moens, kutoka Ubelgiji kuwa Mratibu mkuu wake wa kwanza, huku akisaidiwa na wajumbe kumi na wanane kutoka sehemu mbali mbali za dunia, watakaoshika madaraka kwa muda wa miaka mitatu.

Wawakilishi kutoka Barani Afrika kwa wale wanaozungumza lugha ya Kifaransa ni Bwana Jean Christophe Sakiti, kutoka Togo, kwa wazungumzaji wa lugha ya Kiingereza kutoka Afrika, watawakilishwa na Bwana Fred Mawanda kutoka Uganda. Padre Raniero Cantalamessa, Mhubiri mkuu wa Nyumba ya Kipapa ndiye aliyeteuliwa kuwa Baba wa maisha ya kiroho wa Chama cha Kitume cha Wakarismatiki Wakatoliki. Viongozi wote hawa wataanza kutekeleza dhamana na wajibu wao wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste kwa Mwaka 2019 na Kitengo cha CHARIS kitaanza kazi rasmi!

Tangu wakati huo, Chama cha Huduma ya Upyaisho ya Wakarismatiki Wakatoliki Kimataifa “International Catholic Charismatic Renewal Services”, Chama cha Kidugu cha Wakarismatiki wa Jumuiya za Agano “Fraternity of Charismatic Covenant Communities” pamoja na Chama cha Umoja wa Wakarismatiki, “Fellowship” vitakoma kutoa huduma. Rasilimali yote ya vyama hivi itapaswa kuhamishiwa kwenye kitengo cha CHARIS, ili kukijengea uwezo wa kiuchumi wa kutekeleza dhamana na wajibu wake kadiri ya matakwa ya Baba Mtakatifu Francisko.

Monsinyo Miguel Delgado Galindo, Mwakilishi wa Mashirika na Vyama vya Kitume katika Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha anasema, Chama cha Wakarismatiki Wakatoliki, wengine wanapenda kukiita kama “Mkondo” unaovuviwa na Roho Mtakatifu ambaye ndiye aliyepewa dhamana ya kumshuhudia Kristo Yesu kwa kutakatifuza, kufundisha, kuongoza, kukumbusha pamoja na kuwasaidia waamini kutumia karama zao kwa ajili ya ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Hiki ni kikundi kinachopaswa kustawisha karama za binadamu, ili waweze kupata wokovu kwa kuendelea kumakinika na karama zao za kiroho kwa utukufu wa Mungu, ukuaji wa Kanisa na wokovu wa walimwengu wote.

Baba Mtakatifu Francisko anatambua na kuthamini mchango wa Wakarismatiki Wakatoliki katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Wakarismatiki wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya uekumene wa kiroho, huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii sanjari na kudumisha umoja na mshikamano wa Kanisa.

Wanachama wake wanapaswa kujikita katika toba na wongofu wa kimisionari, kwa kuonesha upendo kwa Kristo na Kanisa lake, ili Mwenyezi Mungu atukuzwe na binadamu atakatifuzwe na hatimaye, akombolewe! Hiki ni chama ambacho kina tofautiana kwa mtindo wa maisha ya sala na huduma, ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko anataka kuwaunganisha wanachama wake wote katika utofauti wao, ili kujenga na kudumisha umoja wa Kanisa.

Monsinyo Miguel Delgado Galindo kuanzia tarehe 3- 4 Novemba 2018 ameshiriki katika mkutano wa Udugu wa Wakatoliki kutoka Kusini mwa Bara la Ulaya. Katika mkutano huu, amekazia umuhimu wa CHARIS katika kuratibu shughuli za Chama cha Wakarismatik Wakatoliki mintarafu mafundisho ya Mababa wa Kanisa, lakini kwa namna ya pekee, mchango wa Baba Mtakatifu Francisko tangu mwaka 2014 na kilele chake ni katika hotuba yake aliyoitoa tarehe 3 Juni 2017 wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Chama cha Wakarismatik Wakatoliki duniani. Hii ni sehemu ya marekebisho makubwa yanayoendelea kutekelezwa na Baba Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kukazia umoja na utofauti kadiri ya karama na mapaji ya Roho Mtakatifu.

CHARIS-Karama

 

 

08 November 2018, 09:31