Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Vita ni matokeo ya uvunjwaji wa haki msingi za binadamu! Papa Francisko: Vita ni matokeo ya uvunjwaji wa haki msingi za binadamu!  (AFP or licensors)

Vita ni uvunjwaji wa haki msingi za binadamu!

Operesheni za amani zinazotekelezwa na Umoja wa Mataifa, zisaidie kuzuia vita, migogoro na mipasuko ya kijamii na hatimaye, zianze kujikita katika mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani kwa kuzingatia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili! Utamaduni wa amani ni muhimu sana katika utekelezaji wa sera na mikakati ya maendeleo endelevu na fungamani duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa vinauwakilisha Umoja wa Mataifa, kwa namna ya pekee, katika kulinda na kudumisha: utulivu, upatanisho pamoja na kuwajengea wananchi matumaini kwa siku za usoni. Umoja wa Mataifa unapania kuona kwamba, utulivu na amani vinatawala; ukosefu wa haki msingi za binadamu pamoja na woga vinatoweka kabisa. Kwa kuondokana na vitendo vya namna hii, amani ya kudumu inaweza kutawala katika akili na nyoyo za watu na hivyo kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Askofu mkuu Bernardito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, New York, Marekani, akichangia mjadala kuhusu vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa anasema, hakuna maendeleo endelevu na fungamani pasi na amani duniani. Kumbe, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuwekeza katika mchakato utakaosaidia kudhibiti uhamiaji wa nguvu na shuruti unaotumiwa kama silaha ya vita katika baadhi ya maeneo yenye migogoro duniani.

Operesheni za amani zinazotekelezwa na Umoja wa Mataifa, zisaidie kuzuia vita, migogoro na mipasuko ya kijamii na hatimaye, zianze kujikita katika mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani kwa kuzingatia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili! Utamaduni wa amani anasema Askofu mkuu Auza ni muhimu sana katika utekelezaji wa sera na mikakati ya maendeleo endelevu na fungamani duniani. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kunako mwaka 2015 alisikika akisema kwamba, vita ni matokeo ya uvunjwaji wa haki msingi za binadamu.

Ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa inataka kukuza na kudumisha maendeleo endelevu na fungamani anasema Askofu mkuu Auza haina budi kujikita katika mchakato wa kutafuta, kukuza na kudumisha amani duniani; kwa kujikita katika utawala wa sheria na majadiliano katika ukweli na uwazi! Katiba ya Umoja wa Mataifa ni dira na mwongozo katika utekelezaji wa maamuzi mbali mbali duniani!

Wanawake wakihusishwa kikamilifu, wanaweza kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya amani duniani, kwa kuzuia vita pamoja na kusaidia utekelezaji wa mikataba ya amani duniani, kwani wao wana uwezo wa kusamehe pamoja na kuanza kupiga hatua ya upatanisho katika ukweli na uwazi. Ni walimu mahili katika mateso na mahangaiko ya watu. Ikumbukwe kwamba, hakuna maendeleo ya kweli pasi na amani na wala hakuna amani pasi na maendeleo endelevu na fungamani; kwani haya mambo mawili yanategemeana na kukamilishana katika ukweli wake!

Vita, uvunjaji wa haki msingi, utu na heshima ya binadamu; ukosefu wa usawa, rushwa, utawala mbovu pamoja na biashara haramu ya silaha ni kati ya mambo ambayo yanaendelea kuchochea vita duniani. Vita inakwamisha ustawi na maendeleo ya jamii. Kutokana na changamoto hii, anasema Askofu mkuu Auza kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwekeza katika: maendeleo, ustawi na mafao ya wengi kwa kudumisha amani na utulivu!

Ujumbe wa Vatican unasikitishwa sana na uhamiaji wa nguvu na shuruti ambao kwa sasa umegeuzwa kuwa kama silaha ya vita. Matokeo yake ni maafa makubwa kwa watu na mali zao. Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kwa sasa ni changamoto changamani inayotokana na vita, dhuluma na nyanyaso za kidini na kijamii. Kumbe, kuna haja ya kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu kama zinavyobainishwa kwenye Katiba ya Umoja wa Mataifa na kwamba, utu, heshima, ustawi na maendeleo ya binadamu viwe ni kati ya vipaumbele vya kwanza katika sera na mikakati ya mendeleo endelevu na fungamani!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, wakimbizi na wahamiaji wanapaswa kwanza kabisa: Kupokelewa, Kulindwa, Kuendelezwa na Kuhusishwa katika sera na mikakati ya jamii inayotoa hifadhi. Ujumbe wa Vatican unaunga mkono jitihada za Operesheni za amani zinazotekelezwa na Umoja wa Mataifa, sehemu mbali mbali za dunia. Ni hatari kubwa ikiwa kama jitihada za kulinda na kudumisha amani sehemu mbali mbali za dunia, zitafutiliwa mbali kama ndoto ya mchana! Kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kushikamana kulinda na kudumisha amani katika maeneo ambayo yalikumbwa na migogoro ya vita, kinzani na mipasuko ya kijamii

[ Audio Embed Vikosi Vya Ulinzi na Usalama].

30 November 2018, 08:12