Tafuta

Vatican News
Vatican: Rasilimali na utajiri wa Afrika viwe ni kwa ajili ya maendeleo fungamani ya binadamu! Vatican: Rasilimali na utajiri wa Afrika viwe ni kwa ajili ya maendeleo fungamani ya binadamu!  (AFP or licensors)

Vatican: Rasilimali watu na maliasili Afrika itumike kwa maendeleo endelevu!

Leo hii Bara la Afrika limegeuka kuwa uwanja wa mapambano ya vita, mahali ambapo makampuni makubwa yanakwapua utajiri wa nchi za Kiafrika pasi na huruma hata kidogo na matokeo yake: ujinga, umaskini na magonjwa yanaendelea kuwaandama watu wa Afrika!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Bara la Afrika limebahatika kuwa na utajiri mkubwa wa mali asili lakini kwa bahati mbaya utajiri wa madini Barani Afrika umekuwa ni chanjo kikuu cha majanga, vita na umaskini kwa familia ya Mungu Barani Afrika! Utajiri huu kama ungetumika vyema, ungeweza kuwa ni kichocheo kikuu cha maendeleo endelevu na fungamani Barani Afrika. Leo hii Bara la Afrika limegeuka kuwa uwanja wa mapambano ya vita, mahali ambapo makampuni makubwa yanakwapua utajiri wa nchi za Kiafrika pasi na huruma hata kidogo na matokeo yake: ujinga, umaskini na magonjwa yanaendelea kuwaandama watu wa Afrika!

Hii ni changamoto ambayo imetolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Bernardito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, wakati Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipokuwa linajadili kuhusu: Amani na usalama: Uimarishaji wa Vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa, ambavyo kati yao saba vinatekeleza dhamana  hii katika nchi za Kiafrika! Vikosi hivi vinapaswa kuimarishwa ili kusaidia mchakato wa kudumisha amani; kuwalinda raia na mali zao pamoja na kusaidia jitihada za upatanisho na umoja wa kitaifa, ili amani iweze kutawala. Wanawake wanapaswa pia kushirikishwa kikamilifu katika harakati za kulinda na kudumisha amani, kwani wao wanao uwezo wa kujenga madaraja yanayowakutanisha watu!

Wanajeshi wa vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa ni watu wanaotekeleza wajibu wao katika mazingira magumu kiasi hata cha kuhatarisha usalama wa maisha yao! Hawa ni watu wanaojisadaka na wanapaswa kutambuliwa na Jumuiya ya Kimataifa, licha ya changamoto mbali mbali wanazokumbana nazo katika operesheni za kulinda amani sehemu mbali mbali za dunia. Umoja wa Mataifa hauna budi kuongeza rasilimali fedha na vitu ili: kuzuia vita na kuimarisha amani na maridhiano kati ya watu. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano, ili kukabiliana kwa pamoja na changamoto hizi.

Askofu mkuu Bernardito Auza anasema, Bara la Afrika linahitaji maboresho makubwa katika sekta ya elimu, ili kuendeleza karama na vipaji vya watu wa Mungu kutoka Afrika, ili hatimaye, waweze kujengewa uwezo wa kupambana na hali pamoja na mazingira yao. Bila elimu makini, Bara la Afrika litaendelea kunyonywa na kugeuka kuwa ni uwanja wa vita na majanga! Baba Mtakatifu Francisko aliwahi kusema, kuna mataifa na makampuni makubwa yanayokwapua utajiri wa Afrika na wala hayana nia hata kidogo ya kuweza kuliendeleza Bara la Afrika!

Bara la Afrika
22 November 2018, 13:52