Askofu mkuu Charles Jude  Scicluna Askofu mkuu Charles Jude Scicluna 

Askofu mkuu Scicluna ateuliwa kuwa Katibu mwambata, Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa

Askofu mkuu Charles Jude Scicluna wa Jimbo kuu la Malta, kuwa Katibu Mwambata wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa na ataendelea kushika wadhifa wake kama Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Malta.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu Charles Jude Scicluna wa Jimbo kuu la Malta, kuwa Katibu Mwambata wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa na ataendelea kushika wadhifa wake kama Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Malta. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Charles Jude Scicluna alizaliwa tarehe 15 Mei 1959 huko Toronto, Canada. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 11 Julai 1986.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI tarehe 6 Oktoba 2012 akamteua kuwa Askofu wa Jimbo kuu la Malta na kuwekwa wakfu tarehe 24 Novemba 2012. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 27 Februari 2015 akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Malta na tarehe 13 Novemba 2018 amemteua kuwa Katibu Mwambata Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Ni kiongozi mtaalam wa Kanisa aliyebobea katika: sheria, kanuni maadili na utu wema.

Askofu mkuu Charles Jude Scicluna Amekuwa ni kiongozi ambaye amejipambanua sana katika utume wake, kushughulikia kesi za nyanyaso za kijinsia ambazo zimechafua kwa kiasi kikubwa maisha na utume wa Kanisa! Changamoto kubwa kwa sasa ni toba na wongofu wa kimisionari, ili kuliwezesha Kanisa kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu!

Askofu mkuu Scicluna
13 November 2018, 16:06