Tafuta

Uinjilishaji unaofumbatwa katika upendo wa kibinadamu! Uinjilishaji unaofumbatwa katika upendo wa kibinadamu! 

Uinjilishaji unaofumbatwa katika upendo wa kibinadamu!

Kongamano la Shirikisho la Maisha ya Familia ya Kiafrika, huko Mauritius kuanzia tarehe 10-15 Novemba 2018 linaongozwa na kauli mbiu “Kutoka Waraka wa Humanae vita hadi Amoris laetitia: Uinjilishaji unaofumbatwa katika upendo wa kibinadamu”

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha katika ujumbe aliowaandikia washiriki wa kongamano la Shirikisho la Maisha ya Familia ya Kiafrika, huko Mauritius kuanzia tarehe 10-15 Novemba 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Kutoka Waraka wa Humanae vitae hadi Amoris laetitia: Uinjilishaji unaofumbatwa katika upendo wa kibinadamu” anafafanua mambo msingi yanayofumbatwa katika nyaraka hizi za kitume ili kuzisaidia familia kutekeleza vyema wajibu na dhamana yake kwa kuendelea kukabiliana na changamoto mamboleo katika maisha na utume wa familia.

Kardinali Farrell anakazia umuhimu wa kulinda na kudumisha Injili ya uhai; wajibu na dhamana ya wazazi na walezi kwa watoto wao pamoja na utume wa Kanisa katika mchakato wa kuzisaidia familia za Kikristo zinazoogelea katika shida na magumu mbali mbali katika maisha ya ndoa na familia. Mababa wa Kanisa tangu Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican hadi Papa Francisko wanaendelea kukazia Injili ya uhai na umuhimu wa kuhudumia zawadi ya maisha kama ambavyo angelifanya Kristo mwenyewe!

Mtakatifu Paulo VI katika Waraka wake wa Kitume “Humanae vitae” yaani “Maisha ya binadamu”, anapembua: kanuni maadili na Mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu mwono na maisha ya mwanadamu, tangu pale anapotungwa mimba hadi pale mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Akakazia: wajibu wa wazazi katika kushiriki kazi ya uumbaji, kulea na kutetea zawadi ya maisha. Anafafanua dhamana na wajibu wa wanandoa kushiriki katika kazi ya uumbaji. Hii ni dhamana wanayoitekeleza kwa uhuru kamili na uwajibikaji, kwani wanashiriki katika mpango wa Mungu katika kazi ya uumbaji. Dhamana hii ni chemchemi ya furaha na matumaini, lakini anasema, wazazi wanakabiliwa na changamoto pevu wanapotekeleza wajibu huu kutokana na kuibuka kwa kasi kubwa kwa dhana ya utamaduni wa kifo dhidi ya Injili ya uhai.

Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia” ni dira na mwongozo wa maisha ya ndoa na familia. Ni matunda ya mwanga wa Neno la Mungu unaozingatia ukweli na changamoto za maisha ya ndoa na familia katika ulimwengu mamboleo. Hili ni jibu kwa familia moja moja kadiri ya hali na mazingira yake. Wosia huu unatoa mwelekeo wa Yesu katika kukuza tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili kuzijengea familia uwezo wa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia. Unakazia upendo thabiti ndani ya familia; upendo unaogeuka na kuwa ni chemchemi na asili ya maisha.

Baba Mtakatifu Francisko anatoa mapendekezo yanayopaswa kufanyiwa kazi katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji mintarafu utume wa maisha ya ndoa na familia. Anawataka wazazi na walezi kuimarisha elimu na makuzi ya watoto wao, ili waweze kuwajibika kikamilifu katika maisha yao. Ni wajibu wa Kanisa kuwasindikiza, kung’amua na kuwasaidia wanafamilia wanaolegalega katika maisha na wito wao. Baba Mtakatifu anachambua kwa kina na mapana tasaufi ya maisha ya ndoa na familia!

Injili ya familia
13 November 2018, 17:05