Tafuta

Vatican News
Sehemu ya tatu ya Hati ya kutendea kazi: Kuchagua: Njia za kichungaji na wongofu wa kimisionari Sehemu ya tatu ya Hati ya kutendea kazi: Kuchagua: Njia za kichungaji na wongofu wa kimisionari  (Vatican Media)

Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana: Sehemu ya III: Uchungaji na wongofu wa kimisionari

Kuchagua ni mchakato unaofumbatwa katika toba na wongofu wa ndani unaojikita katika upyaisho wa sera, mikakati na shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Mama Kanisa kwa kukazia ushuhuda wa huduma ya upendo inayolisukuma Kanisa kutoka na kuwaendelea vijana “waliotokomea vijiweni” ili kuwashirikisha furaha ya Injili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Sergio da Rocha, mmoja ya wawawezeshaji wakuu katika Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana anasema, Mababa wa Sinodi wanafuata mfumo ambao umegawanyika katika sehemu kuu tatu: Mosi: Kung’amua: Kanisa kusikiliza ukweli. Pili, Kutafsiri imani na mang’amuzi ya miito. Tatu: Ni kuchagua: Njia za kichungaji na wongofu wa kimisionari. Kwa sasa  wa Sinodi wameanza kutafakari na kujadili sehemu hii ya tatu ya “Instrumentum Laboris” yaani hati ya kutendea kazi. Mababa wa Sinodi wanasema, Mama Kanisa anatakiwa kufanya maamuzi magumu katika maisha na utume wake ili kujenga mazingira bora yatakayowezesha utekelezaji wa mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji, maisha ya kiroho na wongofu wa kimisionari unaokwenda sanjari na usikivu wa kichungaji.

Kardinali Sergio da Rocha anafafanua kwamba, kuchagua ni mchakato unaofumbatwa katika toba na wongofu wa ndani unaojikita katika upyaisho wa sera, mikakati na shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Mama Kanisa kwa kukazia ushuhuda wa huduma ya upendo inayolisukuma Kanisa kutoka na kuwaendelea vijana “waliotokomea vijiweni” ili kuwashirikisha furaha ya Injili, kama kielelezo cha ushuhuda wa umoja na udugu unaofumbatwa katika kazi ya kimisionari inayopania kutoa majiundo na malezi kamili kwa mtu mzima: kiroho na kimwili.

Mababa wa Sinodi wanakaza kusema, vijana wana ari na mwamko wa kutaka kumtafuta Kristo katika hija ya maisha yao, lakini wakati mwingine wanajikuta wakiwa wanaogelea katika utupu, upweke hasi pamoja na kugubikwa la blanketi la huzuni nyoyoni mwao! Vijana wa kileo wanaweza kuwa kama Mtakatifu Petro ambaye, wakati fulani katika maisha na utume wake, alielemewa na ubinafsi na mapungufu yake kama binadamu, lakini huyu ndiye aliyeteuliwa na Kristo kuwa jiwe la msingi kama walivyo hata Mitume wengine.

Vijana ambao ni matumaini ya leo na kesho iliyo bora katika uongozi wanapaswa kuandaliwa kikamilifu, mintarafu Maandiko Matakatifu na Mafundisho ya Kanisa, ili kweli waweze kuwa wasikivu, tayari kujisadaka kwa ajili ya ujenzi wa jamii inayosimikwa katika utu, kwa kukazia haki msingi za binadamu; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Vijana watakaoweza kusimama kidete kupambana na rushwa, ufisadi na ubinafsi, dhambi inayowapekenya viongozi wengi na matokeo yake ni mateso na mahangaiko ya watu wasiokuwa na hatia.

Malezi na majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya yanapaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika utume wa miito na shughuli za kichungaji kwa vijana sanjari na maboresho ya mfumo wa elimu, kwa kusoma alama za nyakati, ili kweli vijana waweze kujisadaka katika huduma, ustawi na maendeleo ya wengi. Malezi na majiundo ya kiroho yawawezeshe vijana kupata majibu muafaka ya maana halisi ya maisha kwa kujenga na kuimarisha imani, matumaini na mapendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake! Vijana wajenge na kudumisha upendo wa dhati, umoja na mshikamano, tayari kuchakarika kwa ajili ya maboresho ya maisha yao kwa leo na kwa siku za usoni. Wawe ni vyombo na mashuhuda wa upendo kwa Mungu na jirani, tayari kujisadaka katika huduma makini katika sekta mbali mbali za maisha. Vijana wajengewe uwezo ili kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaofumbatwa katika huduma, kielelezo cha imani tendaji. Wawe ni vyombo na mashuhuda wa imani ya Kristo na Kanisa lake. Kazi, daima itambulike kuwa ni kielelezo cha utimilifu wa utu na heshima ya binadamu! Vijana wapatiwe fursa za ajira kwa njia ya ushirikiano na mshimano kati ya Mabaraza ya Maaskofu.

Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni changamoto kubwa inayohitaji kuangaliwa kwa jicho la kichungaji kwani hapa ni sehemu muhimu sana ya majadiliano ya kidini na kiekumene; ili hatimaye, kuwawezesha waamini kuendeleza utambulisho wao wa asili, kwa kushirikisha utajiri wa maisha ya kiroho na kitamaduni na jamii zinazowapatia ukarimu. Majadilino ya kidini na kiekumene, yawawezeshe vijana kuwa na upeo mpana wa maisha na kwamba, wongofu wa shuruti haina nafasi tena katika ulimwengu mamboleo. Ikumbukwe kwamba, kila mtu katika imani yake, anaweza kumfikia Mwenyezi Mungu.

Mababa wa Sinodi wanakazia tena na tena, umuhimu wa Parokia kuamka na kuanza kujikita katika maisha ya kiroho kwa kukuza na kuendeleza Ibada mbali mbali kadiri ya marika na matamanio ya watu mahalia. Vijana washirikishwe vyema katika maisha na utume wa Makanisa mahalia na kwamba, Parokia zinaweza kuwa ni mahali muafaka pa majiundo ya kiroho, kiutu na kitamaduni; mahali pa Katekesi endelevu inayowapatia pia vijana fursa ya kufanya mang’amuzi ya miito katika maisha yao. Vijana wajengewe uwezo wa kutamadunisha imani, ili kweli Habari Njema ya Wokovu iweze kuingia na kuwataka watu.

Mababa wa Sinodi wanasema, vijana ni watu wanaopenda sana sanaa na michezo; kumbe, muziki unaweza kuwa ni fursa muhimu sana ya uinjilishaji, na mahali pa kushuhudia furaha ya Injili, imani na matumaini yao kwa Kristo na Kanisa lake. Utume wa waimbaji ni muhimu unapaswa kukuzwa na kuimarishwa, ili kweli kwaya ziwe ni majukwaa la uinjilishaji na kamwe zisiwe ni vijiwe vya watu waliokosa dira na mwelekeo sahihi wa maisha!

Sinodi Vijana: Wongofu
18 October 2018, 16:36