Cerca

Vatican News
Sinodi: Kanisa liwasaidie vijana kutekeleza ndoto na matamanio halali katika maisha Sinodi: Kanisa liwasaidie vijana kutekeleza ndoto na matamanio halali katika maisha!  (Vatican Media)

Sinodi ya Vijana: Kanisa liwasaidie vijana kutimiza ndoto na matamanio halali katika maisha!

Vijana wanahamasishwa na Mama Kanisa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki jamii, wamisionari miongoni mwa wakimbizi na wahamiaji na kwamba, utakatifu ni wito na mwaliko kwa wote, lakini Kanisa linataka kuwaona vijana wakiwa mstari wa mbele, kwani hili linawezekana, ikiwa kama watatoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo na Kanisa lake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kuchagua ni mchakato unaofumbatwa katika toba na wongofu wa ndani unaojikita katika upyaisho wa sera, mikakati na shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Mama Kanisa, kwa kukazia ushuhuda wa huduma ya upendo, inayolisukuma Kanisa kutoka na kuwaendea vijana “waliotokomea vijiweni” ili, kuwashirikisha furaha ya Injili. Kwa muhtasari hii ni sehemu ya tatu ya “Instrumentum Laboris” yaani “Hati ya Kutendea Kazi” inayoongozwa na kauli mbiu “Kuchagua: Njia za kichungaji na wongofu wa kimisionari”.

Mababa wa Sinodi katika taarifa zao za Makundi wameendelea kutafakari kuhusu: changamoto za vijana wa kizazi kipya; umuhimu wa utume wa vijana ndani ya Kanisa; malezi ya vijana wa ulimwengu wa kidigitali, ili kuunda raia wanaowajibika katika malezi na makuzi yao. Vijana wanahamasishwa na Mama Kanisa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki jamii, wamisionari miongoni mwa wakimbizi na wahamiaji na kwamba, utakatifu ni wito na mwaliko kwa wote, lakini Kanisa linataka kuwaona vijana wakiwa mstari wa mbele, kwani hili linawezekana, ikiwa kama kweli vijana wataamua kumpatia Kristo Yesu, kipaumbele cha kwanza katika maisha yao!

Mababa wa Sinodi wanataka kuona Kanisa linatekeleza sera na mikakati itakayowawezesha vijana kumwilisha ndoto na matamanio halali katika maisha yao, huku wakiendelea kuchangia: wema, uzuri na utakatifu mambo msingi yanayolipyaisha Kanisa la Kristo. Wongofu wa kimisionari ni changamoto pevu katika dhana ya ufuasi wa Kristo na wala si wazo linaloelea katika ombwe. Hapa vijana wanaalikwa kujisikia kuwa ni sehemu muhimu sana ya Kanisa, wanalopaswa kulipenda na kulitumikia kwa moyo mkuu.

Mababa wa Sinodi wanataka kuliona Kanisa ambalo linashuhudia tunu msingi za Injili, chachu muhimu sana itakayowawezesha vijana kujikita katika toba na wongofu wa ndani, kwa kutambua kwamba, wao si watazamaji tu wa sera na mikakati ya shughuli za kichungaji, bali wadau na watekelezaji wa mikakati hii kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa ni uwajibikaji wa pamoja sanjari na urika, ili kushirikishana na kutajirisha na hatimaye, kumwachia Kristo Yesu, aweze kufanya miujiza!

Mababa wa Sinodi wanasema, kuna: matatizo na changamoto nyingi ambazo zinawaandama vijana wa kizazi kipya. Ukosefu wa fursa za ajira; matumizi haramu ya dawa za kulevya na ulevi wa kupindukia; mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo pamoja na ukahaba; kumong’onyoka kwa tunu msingi za kimaadili na utu wema kama vile masuala ya ushoga na ndoa za watu wa jinsia moja! Zote hizi ni changamoto zinazopaswa kuvaliwa njuga katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji, ili kuwasaidia vijana kuwa na mwelekeo sahihi wa maisha; kwa kukua na kukomaa katika imani, maadili na utu wema, bila kuwatenga na kuwanyanyasa vijana.

Sera za utamaduni wa kifo na nyanyaso za kijinsia ni mambo yanayopaswa kuangaliwa kwa jicho la kijuchungaji, toba na wongofu wa kimisionari, ili kuliwezesha Kanisa kuwa kweli ni Mama na mwalimu, aliyepewa dhamana na wajibu wa kutangaza na kushuhudia Injili; kurithisha: imani, utu na maadili mema. Katika mchakato wa kuchagua, Kanisa liwasikilize na kuwasindikiza vijana kufanya mang’amuzi katika maisha na miito yao. Kanisa linapaswa kujikita katika wongofu na tasaufi ya kimisionari, ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili, hata katika sanaa na michezo!

Utume wa Familia, uziwezeshe familia za Kikristo kuwa ni: Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo; haki, amani; maadili na utu wema, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya familia inayofumbatwa katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Mababa wa Sinodi wanakazia pia utume wa Kanisa kwa vijana, ili kuziwezesha Parokia kuwa ni mahali pa malezi na majiundo ya vijana: kwa kuwasikiliza, kuwasindikiza; mahali pa umoja, upendo na mshikamano katika mchakato wa uinjilishaji. Parokia ziwe ni kielelezo cha furaha, matumaini na upendo unaowajibisha katika ujenzi wa umoja na udugu; mahali pa vijana kukua na kukomaa: kiimani, kiutu na kimaadili. Parokia ziwe ni mahali ambapo vijana watajenga imani na matumaini yao kwa Mwenyezi Mungu. Parokia ziwe ni majukwaa ya utume katika huduma, sala na michezo.

Ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano, umeuwezesha ulimwengu kuwa kama kijiji! Maendeleo ya mawasiliano yatumike vyema, ili kuhakikisha kwamba, yanasaidia pia mchakato wa uinjilishaji. Vijana waelimishwe kutambua athari zinazoweza kujitokeza katika matumizi mabaya ya vyombo vya mawasiliano ya jamii na hasa katika mitandao ya kijamii, kwani wanaweza kujikuta wakiwa wahanga wa nyanyaso na mmong’onyoko wa maadili na utu wema.

Vijana wajifunze kuwa ni raia wema na wanaowajibika katika ulimwengu wa kidigitali. Shule, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa, viwe ni mahali muafaka pa majiundo makini, endelevu na fungamani. Nidhamu, ubora, utu, heshima na ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana na kujadiliana ni kati ya vipaumbele vinavyoweza kutambulisha taasisi za elimu zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki, kwani elimu inapania kujenga upendo na kuimarisha umoja na mshikamano kati ya watu!

Mababa wa Sinodi wanawataka vijana kuwa ni vyombo na mashuhuda watakaosimama kidete: kulinda na kutetea haki jamii kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini ambao kimsingi ni amana na utajiri wa Kanisa. Katika umaskini na mahangaiko ya watu, vijana wajifunze kukutana na Mwenyezi Mungu katika maisha yao. Haki jamii, iwasaidie vijana kujenga na kukuza majadiliano ya kidini na kiekumene, ili ulimwengu uweze kuwa ni mahali bora zaidi pa kuishi kwa kujikita katika haki, mshikamano na udugu. Vijana wafundwe kikamilifu Mafundisho Jamii ya Kanisa, wapewe mbinu na miongozo ya utamadunisho ili kuendeleza misingi ya haki, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote!

Kimsingi, vijana wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa utamaduni wa upendo unaofumbatwa katika tunu msingi za kiinjili, huruma na msamaha mambo yanayoweza kumwilishwa katika masuala ya kisiasa, kiuchumi, huduma bora za afya pamoja na mawasiliano ya kijamii. Hii ni sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu, kwa njia ya chachu na furaha ya Injili! Vijana wawe ni watetezi na wahudumu wa wakimbizi kwa: kuwapokea, kuwalinda na kuwashirikisha katika maisha yao. Kwa njia ya Kanisa, pale inapowezekana, wakimbizi na wahamiaji, wahudumiwe katika nchi zao wanamotoka.

Vijana wawezeshwe pia kushiriki katika Ibada, hija na majiundo mbali mbali yanayofanywa na vyama vya kitume, ili waweze kuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu: Mafundisho tanzu ya Kanisa; Kanuni maadili na utu wema, chachu ya uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Yote haya yanalenga kujibu kimsingi, wito wa utakatifu wa maisha, unaoyatakatifuza malimwengu, kwa kufanya maamuzi makini. Vijana wajenge utamaduni wa sala, tafakari na ushiriki mkamilifu wa maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa.

Ibada ya Misa Takatifu, iwe ni mahali pa kukutana na Mwenyezi Mungu: kwa kusikiliza Liturujia ya Neno na kushiriki Fumbo la Ekaristi Takatifu, ili hatimaye, kuweza kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mazingira, tafakari na nyimbo za Ibada ziwasaidie vijana kujenga na kuimarisha imani yao kwa Kristo na Kanisa lake!

Sinodi vijana: Kuchagua

 

23 October 2018, 06:46