Siku ya Kimisionari Duniani 2018: Pamoja na vijana, tupeleke Injili kwa wote! Siku ya Kimisionari Duniani 2018: Pamoja na vijana, tupeleke Injili kwa wote! 

Siku ya Kimisionari Duniani 2018: Fursa ya kusali na kulitegemeza Kanisa katika mchakato wa uinjilishaji

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya Kimisionari Duniani, anakazia umuhimu wa maisha kuwa ni sehemu ya utume wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, changamoto ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kwa kutambua umuhimu wa vijana katika maisha na utume wa Kanisa, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya Kimisionari Duniani kwa mwaka 2018, inayoongozwa na kauli mbiu “Pamoja na vijana, tupeleke Injili kwa wote”, anawaalika waamini wote kushikamana na vijana katika kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kwa watu wote.  

Siku ya Kimisionari Duniani kwa Mwaka 2018 inaadhimishwa Jumapili tarehe 21 Oktoba 2018. Ushuhuda wa Injili ni changamoto endelevu kwa Wakristo wote! Lakini, umisionari unawataka Wakristo kuwa na moyo na ari ya ujana, ili kuthubutu kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya Kimisionari Duniani, anakazia umuhimu wa maisha kuwa ni sehemu ya utume wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, changamoto ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, kwa njia ya ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili!

Siku ya Kimisionari Duniani ni mwaliko kwa waamini  kulitegemeza Kanisa kwa njia ya sala, sadaka na majitoleo kama sehemu ya ushiriki wao katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa! Kanisa halina sababu ya kufanya wongofu wa shuruti, bali litaendelea kuwa ni chombo na shuhuda wa Injili ya upendo inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu, lakini zaidi maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hivi ndivyo anavyosema Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu. Waamini wahakikishe kwamba, wanatumia vyema maisha yao, kwani ni sehemu ya utume wa Kanisa.

Kristo Yesu ndiye kiini cha Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa anayewawajibisha kutangaza na kushuhudia Injili hadi miisho ya dunia, kwa kutambua kwamba, bado kuna umati mkubwa haujabahatika kusikia Injili ya Kristo. Kutokana na changamoto hii, kuna haja ya kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano yanayofumbatwa katika huduma ya upendo inayomwilishwa katika elimu, afya, ustawi na maendeleo endelevu na fungamani. Uinjilishaji ni mchakato unaofumbatwa katika uhalisia wa maisha ya watu, mwaliko kwa Kanisa kuendelea kujikita katika utamadunisho, kwa kuthamini na kuenzi tamaduni za watu mbali mbali.

Kardinali Filoni
20 October 2018, 14:11