Tafuta

Vatican News
Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana wanahimiza utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana wanahimiza utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote!  (AFP or licensors)

Sinodi ya vijana: utunzaji bora wa mazingira, ajira na uinjilishaji wa kina!

Athari za mabadiliko ya tabianchi ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inasikiliza na kujibu kilio cha maskini kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wanaoendelea kuteseka kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, changamoto changamani inayopaswa kuvaliwa njuga na wadau wote

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba wa Sinodi wanaendelea kutafakari na kushirikishana mang’amuzi kwa kujikita zaidi katika sehemu ya tatu ya “Instrumentum Laboris” yaani “Hati ya Kutendea Kazi: Kuchagua: Njia za kichungaji na wongofu wa kimisionari. Utunzaji wa mazingira nyumba ya wote ni kati ya mada ambazo zinaendelea kupewa uzito wa juu katika tafakari za Mababa wa Sinodi kwa wakati huu. Mama Kanisa amekuwa kweli nabii katika sera na mikakati ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na uchumi fungamani unaojikita katika mahitaji msingi ya binadamu.

Hii ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inasikiliza na kujibu kilio cha maskini kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wanaoendelea kuteseka kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, changamoto changamani inayopaswa kuvaliwa njuga na wadau wote, ili kuwarithisha vijana wa kizazi kipya mazingira bora zaidi yatakayokuwa na mvuto wa kuwekeza katika masuala ya kiuchumi, ili kuweza kukidhi mahitaji msingi ya binadamu. Kumbe, Kanisa katika ujumla wake, mashirika ya kitawa na kazi za kitume yanapaswa kujielekeza zaidi katika utunzaji wa mazingira nyumba ya wote, daima wakitoa kipaumbele cha kwanza kwa huduma kwa maskini.

Athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zimepelekea: ukame wa kutisha, mafuriko na maporomoko ya ardhi ni kati ya vyanzo vikuu ambavyo vimepelekea wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi, ambalo wengi wao ni vijana wa kizazi kipya wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Sera na mikakati ya uchumi na maendeleo zisaidie kuwapatia vijana fursa za ajira, kwani kimsingi kazi na utimilifu wa utu na heshima ya binadamu! Bila fursa za ajira vijana wengi watakata tamaa na hivyo kushindwa kutekeleza ndoto katika maisha yao.

Vijana wajengewe uwezo wa kupambana na hali mbali mbali za maisha, ili waweze kuwa ni wadau na wajenzi wa jamii mpya inayosimikwa katika umoja, udugu, haki, amani na mapendo. Mababa wa Sinodi wamekazia umuhimu wa kuwarithisha vijana Mafundisho Jamii ya Kanisa, Maandiko Matakatifu na Katekesi makini na endelevu. Watakatifu waendelee kuwa ni mifano bora ya kuigwa na vijana katika hija ya maisha yao hapa duniani, kwa kutambua kwamba, utakatifu ni wito wa kwanza kwa kila mwamini.

Takwimu zinaonesha kwamba, hadi wakati huu, Mama Kanisa amekwisha watangaza watakatifu vijana 160 ambao ni mifano bora ya kuigwa katika ushuhuda wa imani, maadili na utu wema. Vijana hawa katika maisha yao, walijenga urafiki wa dhati na Kristo Yesu kwa njia ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na Matendo ya huruma yaliyokuwa ni ushuhuda wa imani tendaji. Kanisa bado linaendeleza mchakato wa kuwatangaza vijana kuwa wenyeheri na watakatifu. Hii ni sehemu muhimu sana ya utume kwa vijana wa kizazi kipya na hivyo Kanisa linapaswa kuendelea kumwilisha sera na mikakati ya shughuli za kichungaji katika ngazi mbali mbali sanjari na toba na wongofu wa kimisionari; ili Kanisa liendelee kushuhudia uaminifu kwa Mchumba wake Kristo. Pale ambapo Kanisa limekumbwa na kashfa mbali mbali, iwe ni fursa ya toba, wongofu wa kimisionari na upyaisho wa rasilimali watu na miundombinu ili kuliwezesha Kanisa kujikita katika mchakato wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa ari na moyo mkuu!

Vijana wa kizazi kipya wanaendelea kuogelea katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Mitandao ya kijamii ina faida na madhara yake, kumbe, vijana wanapaswa kuwajibika na kuwa na makini zaidi, ili wasitumbukie katika masuala ya: utumwa mamboleo, biashara haramu ya binadamu na viungo vyake, vita na majanga mbali mbali yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Biashara haramu ya silaha ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa, ili haki, amani, ukweli, upendo na mshikamano wa dhati viweze kutawala akili na nyoyo za watu!

Sera na mikakati ya uchumi na maendeleo itoe msukumo wa pekee kwa vijana, ili kuwajengea matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Mababa wa Sinodi wanasema, kuna haja ya kujenga na kukuza fadhila ya unyenyekevu ili kuwaheshimu, kuwathamini, kuwasikiliza na kuwaenzi vijana wa kizazi kipya. Katekesi makini ipewe kipaumbele cha kwanza na wadau mbali mbali waendelee kuwekeza katika elimu kwa kuanzisha pale inapowezekana shule zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki ili ziweze kuchangia katika malezi na makuzi ya vijana wa kizazi kipya! Uinjilishaji, malezi na makuzi ni changamoto pevu kwa vijana.

Shule na taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu ni majukwaa maalum ya uinjilishaji, makuzi na malezi ya vijana. Ukahaba, ulevi wa kupindukia na matumizi haramu ya dawa za kulevya ni mambo ambayo yanawatumbukiza vijana wengi katika utamaduni wa kifo na hivyo kuwakatisha tamaa katika hija ya maisha yao! Maadhimisho ya Siku za Vijana Kitaifa na Kimataifa ni muda muafaka wa majadiliano ya kidini na kiekumene; kati ya Kanisa na vijana, zitumiwe barabara na Mama Kanisa, ili kuendelea kulipyaisha Kanisa kutokana na ari, mwamko na ujana wa vijana, jeuri na matumaini ya Kanisa.

Mababa wa Sinodi wameunda tume ya Mababa watano watakaohusika kuhariri Barua ya Baba wa Sinodi kwa Vijana, kati yao ni Kardinali Diudonnè Nzapalainga, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Bangui, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati. Muswada wa barua hii utakapokamilika, utawasilishwa kwa Mababa wa Sinodi kwa ajili ya maboresho zaidi.

Sinodi ya Vijana: Mazingira
19 October 2018, 15:22