Sr Petronilla Mukagoa (kushoto), Sr Laurina Kokutona, Papa Paulo VI na Kardinali Laurena Rugambwa (kulia) Sr Petronilla Mukagoa (kushoto), Sr Laurina Kokutona, Papa Paulo VI na Kardinali Laurena Rugambwa (kulia)  

14 Oktoba anatangazwa Papa Paulo VI kuwa Mtakatifu!

Papa Paulo VI ndiye aliye mfuata Papa Yohane XXIII, baadaye akafuatwa na Papa Yohane Paulo I. Alitangazwa na Papa Francisko kuwa mwenyeheri tarehe 19 Oktoba 2014. Na kwa maana hiyo Kanisa zima linajiandaa katika maadhimisho ya Kutangazwa kwake Mtakatifu, siku ya Jumapili 14 Oktoba 2018

Sr. Angela Rwezaula -Vatican

Papa Paulo VI alizaliwa 26 Septemba 1897 na jina lake la ubatizo lilikuwa Giovanni Battista Enrico Antonio Maria Montini. Alikufa tarehe 6 Agosti 1978) na alikuwa papa kuanzia tarehe 21 Juni 1963 hadi kifo chake. Yeye ndiye aliye mfuata, Papa Yohane XXIII na baadaye akafuatwa na Papa Yohane Paulo I. Alitangazwa na Papa Fransisko kuwa mwenye heri tarehe 19 Oktoba 2014. Sikukuu yake huadhimishwa tarehe ya kuzaliwa kwake 26 Septemba. Kwa njia hiyo katikati ya Sinodi  ya maaskofu walio unganika Roma kwa ajili ya Vijana, imani na mang’amuzi ya miito wanajiandaa na Kanisa zima kutangazwa kuwa Mtakatifu  Jumapili 14 Oktoba 2018. Ni madhimisho yatakayofanyika katika uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Maisha yake: Papa Paulo VI alizaliwa tarehe 26 Septemba 1897 huko Concesio, kijiji cha wilaya ya Brescia, katika mkoa wa Lombardia, Italia Kaskazini, ambapo familia Montini ilikuwa na nyumba ya kufanyia likizo. Jina lake la ubatizo lilikuwa Giovanni Battista Enrico Antonio Maria Montini. Wazazi wake, wakili Giorgio Montini na Giuditta Alghisi, walifunga ndoa mwaka 1895 wakazaa watoto watatu: Ludovico, aliyepata kuwa mbunge, Giovanni Battista mwenyewe, na Francesco, daktari. Papa huyo alipozaliwa, baba yake alikuwa mkurugenzi wa gazeti la Kikatoliki "Il Cittadino di Brescia", halafu akawa mbunge. Mwaka 1903 alianza masomo yake kwa Wajesuiti. Mwaka 1907 alihiji Roma kwa mara ya kwanza pamoja na familia, ili kuonana na Papa Pius X, halafu akapewa sakramenti za ekaristi na Kipaimara.

Masomo yake: Mwaka 1916 alimaliza sekondari akajiunga na seminari ya mji wake. Tarehe 29 Mei 1920 alipewa upadrisho katika Kanisa kuu la Brescia. Mwaka uleule akahamia Roma ili kusoma Sheria na Falsafa kwa wakati mmoja. Mwaka 1923 alianza kuelekea diplomasia na kushirikiana na Ofisi za Papa, kwa agizo la Papa Pius XI. Baada ya kutumwa Warsav (Juni-Oktoba 1923), mwaka 1924 alipata digrii tatu. Ushirikiano na Pio XI na Pio XII Baada ya kutimiza majukumu mengine, tarehe 13 Desemba 1937 alichaguliwa kuwa makamu wa Katibu wa Kanisa, Eugenio Pacelli, ambaye mwaka 1939 alichaguliwa kuwa Papa Pius XII. Alimuunga mkono katika jitihada zake za kuzuia vita na kurudisha amani na za kuokoa uhai wa Wayahudi (huko Roma 4.000 waliokolewa na Kanisa kutoka mikono ya Wafashisti). Hata hivyo baada ya vita kuu ya pili alijitahidi kuepusha Italia na ukomunisti.

Askofu mkuu wa Milano: Tarehe 1 Novemba 1954, alichaguliwa kuchunga Jimbo kuu la Milano akapewa daraja ya uaskofu tarehe 12 Desemba. Huko alifaulu kuinua hali ya jimbo katika kipindi kigumu sana. Baada ya kifo cha Pius XII, alichaguliwa badala yake, tarehe 28 Oktoba 1958, Papa Yohane XXIII, aliyemchagua Kardinali wa kwanza kati ya wale aliowateua tarehe 15 Desemba 1958. Chini ya Papa huyo, kardinali Montini alihusika sana na maandalizi ya Mtaguso wa pili, hadi ulipofunguliwa tarehe 11 Oktoba 1962. Mtaguso ulikatika mara moja tarehe 3 Juni 1963 kutokana na kifo cha Papa, Yohane XXIII,

Kuchaguliwa kwa Papa Paulo VI: Mkutano wa makardinali ulichukua muda mfupi kumchagua Montini kuwa Papa, naye alijichagulia jina la Paulo VI, tarehe 21 Juni 1963. Mbele ya mabadiliko ya harakaharaka ya ulimwengu, Papa Paulo VI alishika msimamo wa kujadiliana na wote na kuelekeza mtaguso mkuu uendelee kwa msimamo huo. Haikuwa rahisi kuimarisha Kanisa Katoliki katika mvutano uliojitokeza hasa baada ya mtaguso kati ya wasiokubali mabadiliko na waliotaka kubadili hata mambo ya msingi, lakini alifaulu kwa uvumilivu mkubwa. Alikuwa ni mtu mpole na wa aibu, mwenye elimu kubwa pamoja na maisha ya kiroho ya hali ya juu, alifungua kurasa mpya katika uekumeni, kama  vile alipokubaliana na Patriarki Atenagora I wa Konstantinopoli kufuta hati za mwaka 1054 zilizotenganisha Wakatoliki na Waorthodoksi (1964). Tarehe 14 Septemba 1965, alianzisha Sinodi ya Maaskofu na tarehe 8 Desemba 1965 alifunga rasmi mtaguso.

Ziara za  Papa Paulo VI:  Papa Paulo VI alikuwa Papa wa kwanza kusafiri kwa ndege akaenda mpaka nchi ya mbali, akiwa wa kwanza kwenda Israeli na kutembelea mabara yote. Afya yake ilianza kuleta mashaka haraka mwaka 1978 ambapo alifariki tarehe 6 Agosti saa 3:40 usiku huko Castel Gandolfo, akiacha wasio mzuri sana. Mchakato wa  kumtangaza Mwenye heri Kwa uamuzi wa Papa Yohane Paulo II, tarehe 11 Mei 1993, Kanisa la Roma lilifungua mchakato wa kumtangaza mwenye heri na hatimaye mtakatifu. Tarehe 20 Desemba 2012 Papa Benedikto XVI alipitisha uamuzi wa kukiri ushujaa na fadhila za maadili yote ya Paulo VI, ambaye hivyo alistahili kuitwa Mtumishi wa Mungu. Baada ya kuthibitisha muujiza uliopatikana kwa maombezi yake, Papa Fransisko alimtangaza mwenye heri tarehe 19 Oktoba 2014.

Maandiko muhimu ya Papa Paulo VI: Mbali ya hati za mtaguso mkuu, Mwenyeheri Papa Paulo VI alitoa nyaraka kuu saba: Ecclesiam Suam (6 Agosti 1964), kuhusu majadiliano ya wokovu na binadamu wote; Mense Maio (29 Aprili 1965), kuombea mtaguso na amani; Mysterium Fidei (3 Septemba 1965), kuhusu Ekaristi; Christi Matri (15 Septemba 1966), kumuomba Bikira Maria aombee amani duniani; Populorum Progressio (26 Machi 1967), kuhusu maendeleo ya mataifa; Sacerdotalis Caelibatus (24 Juni 1967), kuhusu useja wa mapadri; Humanae Vitae (25 Julai 1968), kuhusu ndoa na uzazi wa mpango. Hizi ni hat nzuri ambazo bado ni hai katika Kanisa lote la ulimwengu.

11 October 2018, 16:01