Tafuta

Kardinali Napier: Matatizo, changamoto na matamanio halali ya vijana wa Afrika hayana budi kuwasilishwa vyema kwenye Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana 2018. Kardinali Napier: Matatizo, changamoto na matamanio halali ya vijana wa Afrika hayana budi kuwasilishwa vyema kwenye Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana 2018. 

Kardinali Napier: Vijana wa Afrika hawana budi kuwakilishwa vyema kwenye Sinodi ya Maaskofu!

Kardinali Wilfrid Fox Napier, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Durban, Afrika ya Kusini anasema, matamanio halali, shida na mahangaiko ya vijana kutoka Barani Afrika hayana budi kuwasilishwa kikamilifu katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu vijana, ili Mababa wa Kanisa waweze kuyafanyia kazi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kanisa linataka kujenga na kudumisha sanaa na utamaduni wa kuwasikiliza, kuambatana na kuwasindikiza vijana, ili kuweza kukabiliana na changamoto, matatizo na fursa mbali mbali zinazopatikana katika maisha yao. Kanisa linapania kuona kwamba, vijana wanakuwa mstari wa mbele kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu katika uhalisia wa maisha yao na kwamba, Kanisa linataka kusikiliza wasi wasi na mashaka wanayoyafumbatwa katika sakafu ya nyoyo za vijana wa kizazi kipya.

Sehemu ya pili ya “Instrumentum Laboris” yaani “Hati ya Kutendea” inajikita zaidi kuhusu: Kanisa: Imani na miito; mang’amuzi pamoja na kuwasindikiza vijana. Mababa wa Sinodi wanasema, ni furaha na wajibu wa Kanisa kuwasindikiza vijana katika safari yao ya imani, katika ulimwengu, maisha na utume wa Kanisa. Kardinali Wilfrid Fox Napier, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Durban, Afrika ya Kusini, katika taarifa yake kwa waandishi wa habari mjini Vatican amesema kwamba, hii ni Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana wote.

Kumbe, matamanio halali, shida na mahangaiko ya vijana kutoka Barani Afrika hayana budi kuwasilishwa kikamilifu katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu vijana, ili Mababa wa Kanisa waweze kuyafanyia kazi. Kumekuwepo na wimbi kubwa la vijana kutoka Ulaya na Marekani ambao hawaoni tena sababu ya kwenda Kanisa, lakini, vijana Barani Afrika, bado wana ari na moyo wa kuhudhuria na kushiriki katika maadhimisho ya Sakramenti na Mafumbo mbali mbali ya Kanisa. Vijana kutoka Barani Afrika, wanatamani kuona kwamba, Kanisa linayavalia njuga, matatizo, changamoto na matamanio yao halali.

Kazi za shuruti miongoni mwa watoto wadogo, umaskini, ukosefu wa fursa za ajira, vita, kinzani na mipasuko ya kijamii; gharama kubwa za elimu; rushwa na ufisadi ni kati ya mambo yanayowakatisha vijana tamaa kutoka katika nchi nyingi Barani Afrika. Rushwa imekuwa ni donda ndugu katika huduma mbali mbali zinazotolewa Barani Afrika, hali ambayo imeshamilishwa na uchu wa mali, madaraka na utajiri wa haraka haraka. Haya ni mambo msingi yanayopaswa kuingizwa katika hati ya mwisho kutoka kwa Mababa wa Sinodi, ili Mama Kanisa aweze kuyapatia majibu muafaka.

Kardinali Wilfrid Fox Napier anasema, kazi ya makundi inaendelea ili kuweza kubainisha mambo mingi yatakayoingizwa kwenye hati ya mwisho kutoka kwa Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa mwaka 2018. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwahamasisha vijana kuhakikisha kwamba, wanawasilisha shida, magumu, changamoto na matarajio yao, ili yaweze kufanyiwa kazi na Mababa wa Sinodi. Utumwa mamboleo na athari zake katika kudumaza haki msingi za binadamu, utu na heshima ya binadamu; uhamiaji wa shuruti; kumong’onyoka kwa maadili na utu wema miongoni mwa vijana wa kizazi kipya ni kati ya mambo ambayo zimefanyiwa rejea na Mababa wengi wa Sinodi. Lengo ni kuwawezesha vijana kuonja furaha ya Injili katika maisha na utume wa Kanisa.

Kwa upande wake, Kardinali Juan Josè Omella, Askofu mkuu wa Barcellona, anasema, vijana wanapenda kuongozwa na wala si kuamrishwa. Kumbe, mapadre, watawa na waamini walei wanapaswa kusoma alama za nyakati ili kuwasindikiza vyema vijana wa kizazi kipya, ili hatimaye, waweze kufanya maamuzi magumu katika maisha yao kwa imani, matumaini na mapendo thabiti.

Kashfa ya nyanyaso za kijinsia imelichafua sana Kanisa, kiasi hata cha kuwakatisha vijana tamaa kama ambayo anasema Askofu Damiano Giulio Guzzetti wa Jimbo Katoliki Moroto. Lakini, takwimu zinaonesha kwamba, mambo haya yanatendeka hata katika familia. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kulivalia njuga tatizo hili kwa kuwashughulikia wahusika kadiri ya sheria, haki na huruma ya Mungu. Kumbe, hii ni changamoto ya jamii nzima na Kanisa linaendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake.

Ukwapuaji wa rasilimali na mali asili kutoka Barani Afrika, ukoloni mamboleo pamoja na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni changamoto kubwa inayopaswa kushughulikiwa kikamilifu, ili Bara la Afrika liweze kuhakikisha kwamba, rasilimali na utajiri wa Afrika unatumika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na wala si kwa ajili ya watu wachache katika jamii.

Sinodi: Kardinali Napier
15 October 2018, 13:35