Tafuta

Ufunguzi wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana 2018 Ufunguzi wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana 2018 

Sinodi ya vijana: ni maadhimisho ya furaha, ukweli na sanaa ya kuwasikiliza vijana

Kardinali Sergio da Rocha, moja ya wawawezeshaji wakuu katika Sinodi anasema, Mababa wa Sinodi watafuata mfumo ambao umegawanyika katika sehumu kuu tatu: Mosi: Kung’amua: Kanisa kusikiliza ukweli. Pili, Kutafsiri imani na mang’amuzi ya miito. Tatu: Ni kuchagua: Njia za kichungaji na wongofu wa kimisionari.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 3 Oktoba 2018 alizindua rasmi maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana yanayoongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya miito” na kilele cha maadhimisho haya ni hapo tarehe 28 Oktoba 2018. “Instrumentum Laboris” yaani “Hati ya kutendea kazi” inawahimiza vijana kufuata mfano wa Mtakatifu Yohane, Mwanafunzi aliyependwa zaidi na Kristo Yesu katika maisha na utume wake. Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa Kanisa kumsikiliza Roho Mtakatifu atakayewafundisha juu ya ukweli wote.

Maadhimisho ya Sinodi ya Vijana yanaingia katika juma la pili. Kadiri ya Kardinali Sergio da Rocha, moja ya wawawezeshaji wakuu katika Sinodi anasema, Mababa wa Sinodi watafuata mfumo ambao umegawanyika katika sehumu kuu tatu: Mosi: Kung’amua: Kanisa kusikiliza ukweli. Pili, Kutafsiri imani na mang’amuzi ya miito. Tatu: Ni kuchagua: Njia za kichungaji na wongofu wa kimisionari. Mababa wa Kanisa wanasema, Mama Kanisa anatakiwa kufanya maamuzi magumu katika maisha na utume wake ili kujenga mazingira bora yatakayowezesha utekelezaji wa mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji, maisha ya kiroho na wongofu wa kimisionari unaokwenda sanjari na usikivu wa kichungaji.

Sinodi imegusia umuhimu wa liturujia katika maisha na utume wa Kanisa, ili Mwenyezi Mungu aweze kuabudiwa na mwanadamu kutakatifuzwa na hatimaye, kupata wokovu. Hii ni Sinodi ya furaha, ukweli na mchakato wa ujenzi wa sanaa na utamaduni wa kuwasikiliza vijana ili hatimaye Kanisa kuweza kujibu changamoto zao halali. Vijana wanasema, imani ni chemchemi ya nguvu katika maisha yao na kwamba, kuna haja ya kukuza na kudumisha majadiliano, umoja, ushirikiano na mafungamano katika familia. Haitoshi kuwasiliana, bali kushirikishana kikamilifu.

Itakumbukwa kwamba, Mababa wa Sinodi katika juma la kwanza wamekazia kwa namna ya pekee: Umuhimu wa Kanisa kujenga utamaduni na sanaa ya kuwasikiliza vijana. Lengo ni kuliwezesha Kanisa kuibua mbinu mkakati utakaomwilishwa katika shughuli za kichungaji, maisha na utume wa Kanisa. Wanasema, kuna haja ya kujenga umoja, mshikamano na mafungamano thabiti kati ya Kanisa an familia, ili kuweza kuwasindikiza vijana hatua kwa hatua tangu wakiwa nyumbani, shuleni, kwenye taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu. Vijana wajengewe uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maisha ya kijamii, kisiasa na kitamaduni kwa kutambua kwamba, imani na michezo ni sawa na chanda na pete, au kwa maneno mengine, ni sawa na “uji kwa mgonjwa”.

Mababa wa Sinodi wamekazia: haki msingi za kinadamu, utu na heshima ya binadamu, lakini kwa namna ya pekee kabisa, wasichana ambao wanadhalilishwa kutokana na utandawazi usiokuwa na mashiko, utumwa mamboleo na utamaduni wa kifo. Vijana katika ujumla wao wajengewe uwezo wa kupambana na hali pamoja na mazingira yao, kwa njia ya: malezi, majiundo makini na endelevu. Walezi na mababa wa maisha ya kiroho, wapigwe msasa ili kuweza kukabiliana vyema na changamoto za utandawazi na ulimwengu wa maendeleo ya sayansi na teknolijia ili kuwasaidia vyema zaidi vijana katika kupambana na hali zao.

Ukosefu wa fursa za ajira, kumong’onyoka kwa: maadili, utu na heshima ya binadamu miongoni mwa vijana wa kizazi kipya; wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wengi wao wakiwa ni vijana sanjari na misimamo mikali ya kidini na kiimani ni kati ya changamoto mamboleo katika ulimwengi wa vijana kwani ni hatari sana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafungamano ya kijamii. Kwa upande wao, vijana wanataka kuona Kanisa linalosimamia na kushuhudia ukweli na uwazi; Kanisa linalojikita katika umoja, upendo na mshikamano kama kielelezo chenye mvuto na mashiko katika ukuaji na ukomavu wa vijana mintarafu malezi ya: kiutu, kiimani, kijamii na kitamaduni.

Ndoa za utotoni ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya wasichana sehemu mbali mbali za dunia.Kimsingi, Kanisa linapaswa kujikita katika majadiliano ya kweli na vijana pamoja na kujenga sanaa na utamaduni wa kuwasikiliza vijana, ili hatimaye, kujibu matamanio yao halali!

sinodi vijana 2018
08 October 2018, 07:28