Tafuta

Vatican News
Papa Francisko tarehe 15 Oktoba 2018 amekutana na kuzungumza na Rais wa Poland Bwana Andrzej Duda. Papa Francisko tarehe 15 Oktoba 2018 amekutana na kuzungumza na Rais wa Poland Bwana Andrzej Duda. 

Kumbu kumbu ya miaka 40 tangu Papa Yohane Paulo II achaguliwe kuliongoza Kanisa, 1978

Mazungumzo ya viongozi hawa yamejikita zaidi katika kumbu kumbu ya maadhimisho ya miaka 40 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 15 Oktoba 2018 amekutana na kuzungumza na Rais Andrzej Duda wa Poland ambaye, baadaye amepata fursa ya kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Mazungumzo ya viongozi hawa yamejikita zaidi katika kumbu kumbu ya maadhimisho ya miaka 40 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Wamegusia tunu msingi za maisha ya kikristo katika historia ya Poland, hususan katika mchakato wa majiundo ya utamaduni na maisha ya kiroho. Baba Mtakatifu pamoja na mgeni wake, wameendelea kudadavua tema mbali mbali kwa kukazia umuhimu wa kulinda, kutetea na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia pamoja na ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji.

Mwishoni mwa mazungumzo yao, viongozi hawa wamegusia: mchango wa Poland katika mpango mkakati wa ushirikishwaji katika Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, vita na kinzani huko Ukraine na Mashariki ya Kati; wakimbizi na wahamiaji; umuhimu wa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Itakumbukwa kwamba, mji wa Katowice, Desemba 2018, utakuwa ni mwenyeji wa mkutano wa kimataifa kuhusu mazingira unaoandaliwa na Umoja wa Mataifa.

Papa: Poland
15 October 2018, 14:38