Vatican News
Papa Francisko, Alhamisi tarehe 18 Oktoba 2018 amekutana na kuzungumza na Rais wa Korea ya Kusini. Papa Francisko, Alhamisi tarehe 18 Oktoba 2018 amekutana na kuzungumza na Rais wa Korea ya Kusini.  (AFP or licensors)

Papa Francisko akutana na kuzungumza na Rais wa Korea ya Kusini

Viongozi hawa wameridhishwa na juhudi zinazofanywa na wadau mbali mbali ili kubomoa kuta za kinzani zilizopo kati ya Korea ya Kaskazini na Korea ya Kusini, ili hatimaye, kufungua ukurasa mpya wa amani na maendeleo fungamani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 18 Oktoba 2018 amekutana na kuzungumza na Rais Moon Jae-in wa Korea ya Kusini, ambaye baadaye, alibahatika kukutana na kuzungumza pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko pamoja na mgeni wake, wakati wa mazungumzo yao ya faragha, wameridhishwa na uhusiano wa kidiplomasia uliopo kati ya nchi hizi mbili pamoja na mchango wa Kanisa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi hususan katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii; majadiliano na upatanisho kati ya Korea ya Kusini na Kaskazini.

Viongozi hawa wameridhishwa na juhudi zinazofanywa na wadau mbali mbali ili kubomoa kuta za kinzani zilizopo kati ya Korea ya Kaskazini na Korea ya Kusini, ili hatimaye, kufungua ukurasa mpya wa amani na maendeleo fungamani. Mwishoni, Baba Mtakatifu na Rais wa Korea ya Kusini wamegusia pia masuala ya kikanda!

Papa Francisko: Korea
19 October 2018, 07:14