Tafuta

Vatican News
Mwenyeheri Tiburzio Arnàiz Munoz alijisadaka kwa ajili ya huduma ya upendo kwa maskini, wagonjwa na wafungwa! Mwenyeheri Tiburzio Arnàiz Munoz alijisadaka kwa ajili ya huduma ya upendo kwa maskini, wagonjwa na wafungwa!  (AFP or licensors)

Mwenyeheri Tiburzio Arnàiz Munoz: Padre aliyejisadaka kwa ajili huduma kwa wagonjwa, maskini na wafungwa!

Huyu ni Padre Myesuit ambaye maisha yake yalipambwa kwa huduma ya upendo kwa: maskini, wafungwa na wagonjwa; akajitahidi kuwa ni chombo cha amani na upatanisho, mahali ambapo kuliwa na kinzani na migawanyiko kutokana na sababu mbali mbali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwenyeheri Tiburzio Arnàiz Munoz, SJ., alizaliwa kunako mwaka 1865 huko Valladolid, nchini Hispania baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapadrishwa kunako mwaka 1890. Huyu ni Padre ambaye maisha yake yalipambwa kwa huduma ya upendo kwa: maskini, wafungwa na wagonjwa; akajitahidi kuwa ni chombo cha amani na upatanisho, mahali ambapo kuliwa na kinzani na migawanyiko kutokana na sababu mbali mbali.

Mwenyeheri Tiburzio Arnàiz Munoz Alifanikiwa sana kuwarejesha waamini waliokata na kujikatia tamaa katika imani kwa njia ya: mahubiri yaliyoandaliwa kikamilifu, kiasi hata cha kukita mizizi yake katika sakafu ya waamini wake. Alitumia muda mrefu katika kiti cha huruma ya Mungu na hivyo kuwapatia waamini waliotubu na kumwongokea Mungu nafasi ya kuonja tena ile furaha ya Injili ikibubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Alipendelea sana kutoa mafundisho ya dini shuleni, hasa siku za jumapili kama muda muafaka wa malezi, makuzi na uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, changamoto inayofanyiwa kazi na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana hapa mjini Vatican. Alizama zaidi katika huduma kwa wagonjwa ili kuwaganga kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini. Akawaonjesha wafungwa huruma na upendo wa Mungu unaookoa.

Mwenyeheri Tiburzio Arnàiz Munoz anakumbukwa sana na waamini wa Parokia ya Malaga, nchini Hispania, ambako Kardinali Giovanni Angelo Becciu, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 20 Oktoba 2018 amemtangaza kuwa Mwenyeheri! Ni katika Parokia hii, alipoanza kujielekeza zaidi katika mchakato wa uinjilishaji vijijini, huku akishirikiana kwa karibu sana na waamini walei kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili.

Mwenyeheri Tiburzio Arnàiz Munoz, alijitahidi sana kuwapatia mafundisho muhimu ya Kanisa na kuwasaidia katika maisha yao ya kiroho, Makatekista waliokuwa wanashirikiana naye, kwani hawa walikuwa ni sehemu ya mihimili mikuu ya uinjilishaji. Matokeo yake, Makatekista hawa wakaungana na kujenga Jumuiya ya waamini walei waliojiweka wakfu kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Hawa wanajulikana kama “Wamisionari wa Mafundisho Vijijini”. Katika maisha na utume wake, Mwenyeheri Tiburzio Arnàiz Munoz alionesha upendo wa dhati kwa Kristo na Kanisa lake, akafariki dunia hapo tarehe 18 Julai 1926.

Kardinali Becciu katika mahubiri yake anasema, Mwenyeheri Tiburzio Arnàiz Munoz kwa hakika alimshuhudia Kristo Mfufuka mbele ya watu wa Mataifa na sasa amemvisha taji ya utukufu kwa kuandikwa kwenye orodha ya wenyeheri, kwani alionesha upendo wa dhati! Ni shuhuda wa imani tendaji, iliyomwilishwa katika huduma kwa wagonjwa, maskini na wafungwa na kwa njia hii, akashiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, mfano bora wa kuigwa katika ushuhuda, kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo kati ya watu wake. Imani, matumaini na mapendo, zilikuwa ni nguzo katika utume wake katika mchakato mzima wa uinjilishaji wa kina unaogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili!

Ni Padre aliyerutubisha maisha yake kwa njia ya sala, tafakari na maisha ya Kisakramenti, akajinyenyekesha mbele ya Roho Mtakatifu na hatimaye, akajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Amekuwa ni chemchemi inayozima kiu ya maisha ya imani, faraja kwa wote wanaoteseka na shuhuda wa matumaini yanayofumbatwa katika ukarimu na mshikamano wa upendo, ili kuganga na kuponya madonda ya kijamii yanayoendelea kuwatesa watu wa Mungu!

Mwenyeheri Munoz
20 October 2018, 15:26