Tafuta

Mtakatifu Paulo VI ni Papa wa familia, alilinda na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Mtakatifu Paulo VI ni Papa wa familia, alilinda na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! 

Mtakatifu Paulo VI ni Papa wa familia, alilinda Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Mtakatifu Paulo VI alikuwa mwamba wa Injili ya familia na kamwe hakutikisika katika maamuzi na mafundisho yake ya kina! Ndiyo maana anakumbukwa kama “Papa wa familia” aliyekita mafundisho yake katika tasaufi ya Kikristo, wito na dhamana ya wazazi ndani ya familia, ili waweze kuwa mashuhuda wa upendo wa Kikristo,

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Paulo VI hapo tarehe 25 Julai 1968, miaka 50 iliyopita, alichapisha Waraka wa Kitume: “Humanae vitae” yaani “Maisha ya binadamu”. Ni waraka wa kinabii unaobainisha dhamana na wajibu wa wanandoa wanaoushiriki katika kazi ya uumbaji, ili kuendeleza zawadi ya maisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ni dhamana ambayo inapaswa kumwilishwa katika furaha ya maisha na utume wao ndani ya familia. Mtakatifu Paulo VI alikuwa na upeo mpana na uwezo wa kuona mbali, akagundua changamoto na vikwazo vinavyowakabili wanandoa; akabainisha wajibu wa Kanisa kama Mama na Mwalimu na kuwataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kusimama kidete kulinda, kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo ni kati ya mafundisho mazito ya Mtakatifu Paulo VI aliyetangazwa na Papa Francisko kuwa Mtakatifu hapo tarehe 14 Oktoba 2018. Anakita mawazo yake katika dhamana na wajibu wa uumbaji, malezi, makuzi na elimu ya watoto. Wanandoa wanapaswa kufikiri, kujiandaa kikamilifu, kusindikizana na hatimaye, kupokea mtoto kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, dhamana inayowawajibisha! Hizi ni changamoto zilizoibuliwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, zinazowataka waamini kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili ya uhai; kwa kujikita katika kanuni maadili na utu wema, sadaka na majitoleo binafsi.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, tarehe 18 Oktoba 2018 amezindua kitabu cha Waraka wa Kitume: “Humanae vitae” yaani “Maisha ya binadamu” kilichoandikwa na Monsinyo Gilfredo Marengo, Rais wa Taasisi ya Yohane Paulo II kwa ajili ya Ndoa na Familia anasema, Mtakatifu Paulo VI alikuwa mwamba wa Injili ya familia na kamwe hakutikisika katika maamuzi na mafundisho yake ya kina! Ndiyo maana anakumbukwa kama “Papa wa familia” aliyekita mafundisho yake katika tasaufi ya Kikristo, wito na dhamana ya wazazi ndani ya familia, ili waweze kuwa mashuhuda wa upendo wa Kikristo, changamoto inayoendelea kutolewa na Baba Mtakatifu Francisko licha ya matatizo, shida na changamoto katika maisha ya ndoa na familia!

Kardinali Parolin anasema, Waraka huu wa kitume ulikabiliwa na changamoto kubwa kwa wakati huo baada ya kuibuka “dhana ya kudhibiti uzazi” ili kupunguza idadi ya watu duniani na baadhi ya wanataalimungu wakajikuta wakitumbukia katika mtego huu kwa kulitaka Kanisa kusoma alama za nyakati kwa kusahau kwamba, walikuwa wanakwenda kinyume cha Mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu Injili ya uhai, zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Mtakatifu Paulo VI katika changamoto hii, akaonesha hekima ya kichungaji na kuungwa mkono na Kardinali Karol Wojtyla, aliyekuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Cracovia, Poland, ambaye baada ya kuteuliwa kwake kuliongoza Kanisa, akasimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Mtakatifu Paulo VI amewawezesha waamini kutambua kwamba, Mafundisho ya Kanisa ni endelevu na daima, Kanisa linapenda kusoma alama za nyakati kwa kuzingatia amana na utajiri wa Mafundisho Tanzu ya Kanisa.

Kumbe, kuna umuhimu wa kuhakikisha kwamba, kuna kuwepo na mshikamano wa dhati kati ya taalimungu na shughuli za kichungaji; kati ya imani na uhalisia wa maisha! Kulinda Mafundisho tanzu ya Kanisa kunahitaji uaminifu kwa viongozi na upendo unaoshuhudiwa na waamini. Waraka wa Kitume: “Humanae vitae” yaani “Maisha ya binadamu” ni ushuhuda endelevu wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaosimikwa katika upendo na uwajibikaji, utu na heshima ya wanandoa katika kutangaza na kushuhidia Injili ya familia kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko.

Kwa bahati mbaya, wanasiasa wamejichukulia madaraka makubwa ya kuamua hatima ya utu wa binadamu na maisha yake, jambo ambalo anasema Kardinali Parolin, si sahihi ingawa linaendelea kutendeka hadi leo hii. Katika unyenyekevu wa kichungaji, Mtakatifu Paulo VI alitafuta ushauri kwa viongozi mbali mbali wa Kanisa na hatimaye akaibuka na ushuhuda wa Kanisa kwa kusema kwamba, uchungu na fadhaa ya mwanadamu anayeteseka hasa makini ni furaha, matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia!

Injili ya uhai bado inakabiliwa na changamoto, kwani kuna baadhi ya wazazi na walezi wanawaona watoto wao kuwa ni “mzigo”; utu na heshima ya wanawake bado ni tete katika maeneo mengi duniani; elimu na malezi ya watoto yanapaswa kuboreshwa zaidi sanjari na kuwajengea vijana wa kupambana na hali pamoja na mazingira yao! Lakini, Kardinali Pietro Parolin anasema, pasi na familia, hakuna Kanisa wala jamii ya mwanadamu na kwamba, Kanisa litaendelea kutoa msaada wa kichungaji kwa familia ya Mungu ili kukuza na kudumisha Injili ya familia inayofumbatwa katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Mtakatifu Paulo VI ameacha utajiri mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, changamoto kwa familia ya Mungu kuwajibika kikamilifu katika kumwilisha Mafundisho tanzu ya Kanisa maisha na utume wake!

Injili ya Uhai
19 October 2018, 14:07