Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anawataka waamini kupyaisha ari na mwamko wa kimisionari kwa njia ya: maisha ya kiroho, ushuhuda, majiundo na huduma ya upendo. Papa Francisko anawataka waamini kupyaisha ari na mwamko wa kimisionari kwa njia ya: maisha ya kiroho, ushuhuda, majiundo na huduma ya upendo.  (AFP or licensors)

Papa Francisko: Imarisheni umisionari kwa njia ya: maisha ya kiroho, shuhuda, majiundo na huduma ya upendo!

Mwezi Oktoba 2019 Kanisa litakuwa linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Benedikto XV alipochapisha Waraka wa Kitume"Maximum Illud" yaani “Kuhusu Shughuli za Kimisionari.” Waraka unapembua mchakato mzima wa shughuli za kimisionari zinazotekelezwa na Mama Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwezi Oktoba 2019 kitakuwa ni kipindi maalum sana kwa maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa linapaswa kujiekeleza zaidi katika utekelezaji wa mambo makuu manne: Mosi, waamini kukutana na Kristo Yesu kwa njia ya Ekaristi Takatifu, Neno la Mungu na Sala. Pili ni ushuhuda wa wamisionari watakatifu, wafiadini na waungama imani, kielelezo makini cha uwepo wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Tatu ni majiundo makini na endelevu ya kimisionari kwa kujikita katika: Biblia, Katekesi, Tasaufi na Taalimungu. Nne ni huduma ya upendo kama kielelezo cha imani tendaji!

Hii ni sehemu muhimu sana kwa ajili ya maandalizi ya matukio makuu katika maisha na utume wa Kanisa. Mwaka 2019 Kanisa litakuwa pia linaadhimisha Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia yatakayofanyika mjini Vatican, mwezi Oktoba 2019 kwa kuongozwa na kauli mbiu "Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa jili ya ekolojia endelevu". Hati ya maandalizi ya Sinodi ya Amazonia inakazia umuhimu wa: kuona, kung'amua na kutenda!

Askofu mkuu Giovanni Pietro Dal Toso, Katibu Mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu na Rais wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kimisionari Duniani kwa Mwaka 2018 anasema, ifikapo mwaka 2022, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu litakuwa linaadhimisha Jubilei ya Miaka 400 tangu kuanzishwa kwake; Miaka 200 tangu kuanzishwa kwa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari na miaka 100 tangu baadhi ya Mashirika ya kitume yalipopewa hadhi ya kuwa ni Mashirika ya Kipapa, ili kuweza kulihudumia Kanisa la Kristo ulimwenguni kote! Lengo ni kupyaisha tena ari na mwamko wa kimisionari ambao waamini wamejitwalia kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, ili kuwa na mashiko na mvuto, kielelezo makini cha uinjilishaji mpya!

Utakuwa ni muda wa kusali na kutafakari utume kama msingi wa mchakato mzima wa uinjilishaji mpya unaotekelezwa na Mama Kanisa. Kwa hakika hiki ni kipindi cha ushuhuda wa  huruma ya Mungu inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Mwezi Oktoba 2019 Kanisa litakuwa linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Benedikto XV alipochapisha Waraka wa Kitume"Maximum Illud" yaani “Kuhusu Shughuli za Kimisionari.” Waraka unapembua mchakato mzima wa shughuli za kimisionari zinazotekelezwa na Mama Kanisa. Unakazia umuhimu wa maandalizi ya wamisionari na wakleri katika maisha na utume wa Kanisa; umuhimu wa mapadre, watawa na waamini walei kuchuchumilia utakatifu wa maisha pamoja na kuendelea kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Waamini walei wanashirikishwa kwa namna ya pekee, utume wa kimisionari kwa njia ya sala; kwa kusaidia kutegemeza miito mbali mbali ndani ya Kanisa sanjari na kuchangia kikamilifu katika mchakato wa kulitegemeza Kanisa Mahalia. Utakuwa ni muda wa: sala, katekesi, tafakari na matendo ya huruma!

Ni wakati muafaka kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanatelekeza vyema dhamana na wajibu waliojitwaliwa kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo inayowashirikisha: Unabii, Ukuhani na Ufalme wa Kristo. Waamini wakiwa wamezaliwa kwa “Maji na Roho Mtakatifu”, wanawajibu wa kukiri na kutangaza imani ambayo wameipokea kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kanisa na hivyo kushiriki katika utendaji wa kitume na wa kimisionari wa Taifa la Mungu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Jubilei ya miaka 100 tangu kuchapishwa kwa Waraka wa Kitume “Maximum illud”, Mwezi Oktoba, 2019 kitakuwa ni kipindi cha sala na shuhuda za watakatifu na wafia dini.

Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu anakaza kusema, Kanisa linahitaji kupyaishwa daima kutoka katika undani wa maisha na utume wake kwa njia ya: toba na wongofu wa ndani, unaofanywa na watoto wa Kanisa. Kwa moyo unaowaka mapendo, Kanisa litaendelea: kupenda, kutangaza, kushuhudia na kuhudumia watu wote!  Maandalizi ya maadhimisho ya kipindi hiki maalum cha kutangaza na kushuhudia Injili kilisaidie Kanisa kuwa daima katika mchakato wa kujiinjilisha kwanza. Jumuiya za waamini ziwe ni jumuiya za matumaini yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha, kwa kuwashirikisha wengine. Ziwe ni Jumuiya za upendo wa kidugu; zenye utamaduni wa kusikilizana daima sanjari na kuamini kuhusu matumaini yanayofumbatwa katika Amri mpya ya upendo kwa Mungu na jirani.

Familia ya Mungu, kuna wakati inashawishiwa na kujikuta ikimezwa sana na malimwengu. Kumbe, kuna haja kwa familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia kusikiliza matendo makuu ya Mungu yakitangazwa tena mbele yake; kwamba, wanahamasishwa kumwongokea Mwenyezi Mungu na wanaalikwa kuungana naye tena kwani daima familia ya Mungu inapaswa kuinjilishwa, ili kujichotea nguvu ya ya kutangaza na kushuhudia Injili.

Padre Fabrizio Meroni, Katibu mkuu wa Mashirika ya Kipapa ya Kazi za kimisionari anakaza kusema, itakuwa ni nafasi ya kufanya tafakari ya Kibiblia na Kitaalimungu; katekesi makini pamoja na matendo ya ukarimu, yatakayolisaidia Kanisa kuinjilishwa tena, ili kupata ari na nguvu ya kushuhudia upendo ule wa kwanza kwa Kristo: aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ili hatimaye, kuinjilisha kwa kujikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kielelezo makini cha imani tendaji inayobubujika kutoka katika tafakari makini ya Neno la Mungu. Lengo ni kuamsha tena ari na moyo wa kimisionari, ili kupyaisha sera na mikakati ya shughuli za kichungaji inayotekelezwa na Mama Kanisa.

Kardinali Filoni anaendelea kufafanua kwamba, Mwezi Oktoba, 2019, utakuwa ni mwezi maalum kwa Mama Kanisa kujikita katika: Sala, matendo ya huruma, katekesi makini sanjari na tafakari ya kina kuhusu taalimungu ya maisha na utume wa Kanisa. Kumbe, wakristo wote wanahamasishwa kusaidia kuyategemeza Makanisa Mahalia, kwa hali na mali, ili kweli yaweze kusimama imara kutangaza na kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili pamoja na kuwa na mihimili ya uinjilishaji, yaani: wakleri, watawa na makatekista. Hapa kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa kuchangia ukuaji wa Makanisa Mahalia, kwa kutambua kwamba, kila mwamini anaweza kuchangia kadiri ya uwezo na nafasi yake. Makanisa mahalia hayana budi kuanza kujitegemea kiuchumi kama sehemu ya mchakato wa ukomavu unaojikita katika uinjilishaji na ushuhuda wa imani katika matendo.

Katika mwelekeo huu, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu linaendelea kujipanga ili kuweza kuunganisha vyombo vyake vya habari kuwa ni chombo kimoja chenye nguvu zaidi, sanjari na kuendeleza mageuzi katika Sekretarieti kuu; kwa kukazia majiundo awali na endelevu ya wamissionari; umoja na mshikamano kwa Makanisa Mahalia kwa kuunganisha nguvu katika masuala ya: familia, uzazi na malezi bora; Injili ya uhai; elimu na shule; pamoja na kuendelea kujikita katika kuwalinda watoto wadogo, kwa kusaidia majiundo makini ya wazazi na walezi; mapadre, watawa na makatekista!

Padre Fabrizio Meroni, anaendelea kufafanua kwamba, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana kilichoko mjini Roma kinajiandaa kuadhimisha makongamano ya kimataifa yatakayojikita katika taalimungu, umisionari mintarafu: Uinjilishaji awali; Nyaraka za viongozi wa Kanisa kutoka “Maximum illud” hadi “Evangelium gaudium” yaani “Furaha ya Injili. Kutakuwepo na mkutano na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume utakaotafakari pamoja na mambo mengine juu ya: “Uinjilishaji, Sakramenti na Ushuhuda” katika mchakato wa uinjilishaji wa awali.

Ili kuweza kufanikisha mbinu mkakati huu, kuna haja ya kuwa na ushirikiano kati ya Baraza la Kipapa na Makanisa mahalia, ili Injili iweze kutangazwa, Sakramenti kuadhimishwa na Wakristo kutoa ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Baraza pia linaendelea kuandaa fursa makini za malezi na majiundo ya kimisionari na kisomi ili kushirikishana sera na mikakati ya shughuli za kichungaji. Kunatarajiwa kuwepo na Kongamano kwa ajili ya Bara la Afrika, Bara Asia na Oceania pamoja na Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Amazonia. Kanisa Barani Ulaya, litajipanga kivyake vyake.

Maximum Illud
22 October 2018, 08:06