Tafuta

Kardinali Parolin asema, amani ni zawadi kutoka kwa Mungu inayofumbatwa katika ukweli, haki, upendo na uhuru. Kardinali Parolin asema, amani ni zawadi kutoka kwa Mungu inayofumbatwa katika ukweli, haki, upendo na uhuru. 

Kardinali Parolin: Amani ni zawadi kutoka kwa Mungu inayofumbatwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru!

Kardinali Parolin amekazia amani kama zawadi kutoka kwa Kristo Mfufuka; mateso na mahangaiko ya watu na kwamba, amani ya kweli inafumbatwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru na kwamba, amani ni jina jipya la maendeleo endelevu na fungamani

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumatano jioni, tarehe 17 Oktoba 2018 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuombea amani nchini Korea. Ibada hii imehudhuriwa na Rais Jae-in Moon wa Korea ya Kusini pamoja na familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya mji wa Roma. Katika mahubiri yake, Kardinali Parolin amekazia amani kama zawadi kutoka kwa Kristo Mfufuka; mateso na mahangaiko ya watu na kwamba, amani ya kweli inafumbatwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru na kwamba, amani ni jina jipya la maendeleo endelevu na fungamani; mambo yaliyopewa kipaumbele cha pekee na Mtakatifu Paulo VI, muasisi wa Siku ya Kuombea Amani Duniani.

Kardinali Parolin anasema, Kashfa ya Msalaba iliwasumbua sana Mitume wa Yesu, kiasi hata cha kujifungia ndani kwa hofu ya Wayahudi. Kristo Mfufuka alipowatokea, aliwakirimia amani kama zawadi yake ya kwanza. Hii ni amani inayobubujika kutoka katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake, kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Amani ya Kristo Mfufuka ni kitulizo kikuu kwa mwamini anayetafuta furaha ya kweli na utimilifu wa maisha. Hili ni fumbo la maisha ya kiroho linalounganisha nguvu ya sadaka ya Kristo Msalabani na uwezo wake wa kupyaisha mambo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Ufufuko. Amani ya Kristo ina uwezo wa kupyaisha mambo!

Kardinali Parolina amesikika akisema kwamba, Ibada ya Misa Takatifu jioni hiyo, ilipania kwa namna ya pekee, kuinua nyuso zao kwa unyenyekevu mbele ya Mwenyezi, anayeongoza historia na hatima ya mwanadamu, ili kuombea amani duniani. Lakini kwa namna ya pekee ni kwa ajili ya Korea ambayo kwa miaka mingi imekumbwa na kinzani pamoja na mipasuko ya kijamii, ili yote haya yaweze kupewa kisogo ili hatimaye, amani iweze kutawala katika akili na nyoyo za watu. Baada ya mateso na mahangaiko, familia ya Mungu nchini Korea inahamu ya kutaka kusikiliza Injili ya amani ikitangazwa na kushuhudiwa tena nchini mwao.

Amani inajengwa na kusimikwa katika huduma, haki na mshikamano; kwa kusimamia na kudumisha: utu na haki msingi za binadamu; sanjari na kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wanyonge ndani ya jamii. Lakini kwa mwamini, kwanza kabisa amani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Mfalme wa amani, ambaye ametangazwa na Manabii wengi katika Agano la Kale na kushuhudiwa kwa namna ya pekee na Kristo Mfufuka. Amani ni kati ya vipaumbele vya kwanza katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Amani kutoka kwa Mwenyezi Mungu inawafunulia waja wake Fumbo la Msalaba linalofumbata uhalisia wa maisha ya binadamu; Msalaba ni kielelezo pia cha mateso na mahangaiko ya binadamu na kwamba, amani ya Kristo inafumbatwa katika Fumbo la Msalaba! Mama Kanisa anamshukuru Mtakatifu Paulo VI, muasisi wa maadhimisho ya Siku ya Kuombea Amani Duniani, iliyoanzishwa kunako tarehe 1 Januari 1968, ili kuwasaidia waamini kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa amani duniani; kwa kuwawezesha walimwengu kujifunza kupenda amani, kuilinda na kuidumisha kwa kujikita katika misingi ya ukweli, haki, uhuru na upendo.

Mwishoni, Kardinali Parolin, ameitaka familia ya Mungu nchini Korea kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuikirimia neema ya amani kama sehemu ya utume wake katika ulimwengu mamboleo, kwa kujiaminisha chini ya Fumbo la Msalaba, daima ikiwa na matumaini ya ufufuko. Neema ya Mungu iwawezeshe kujenga ndani mwao: toba, msamaha, umoja na udugu; ili hata katika tofauti zao amani iweze kushuhudiwa pia hata kwenye Jumuiya ya Kimataifa. Amani na upatanisho ndiyo sala ambayo wamemtolea Mwenyezi Mungu katika Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kuombea Korea.

Parolin: Korea

 

 

18 October 2018, 16:17