Vatican News
Kardinali Marc Ouellet asema shutuma dhidi ya Papa Francisko hazina mvuto wa mashiko! Kardinali Marc Ouellet asema shutuma dhidi ya Papa Francisko hazina mvuto wa mashiko! 

Kardinal Marc Ouellet: shutuma dhidi ya Papa Francisko hazina mvuto wala mashiko!

Shutuma dhidi ya Baba Mtakatifu Francisko na Sekretarieti kuu ya Vatican mintarafu kashfa ya nyanyaso za kijinsia iliyomkumba Askofu mkuu mstaafu Theodore McCarrick ambaye ameng’olewa pia kwenye Baraza la Makardinali ni upotofu wa ukweli na nidhamu. Ni shutuma zinazojikita katika matamanio ya kisiasa na kamwe hazina ukweli ndani yake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Marc Ouellet, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu katika barua yake ya wazi, amesema, shutuma zilizotolewa na Askofu mkuu Carlo Maria Viganò dhidi ya Baba Mtakatifu Francisko na Sekretarieti kuu ya Vatican mintarafu kashfa ya nyanyaso za kijinsia iliyomkumba Askofu mkuu mstaafu Theodore McCarrick ambaye ameng’olewa pia kwenye Baraza la Makardinali ni upotofu wa ukweli na nidhamu. Ni shutuma zinazojikita katika matamanio ya kisiasa na kamwe hazina ukweli ndani yake

Shutuma hizi zinalenga kumchafua Baba Mtakatifu Francisko, ambaye amekuwa ni shuhuda kama kiongozi, Baba mwenye huruma na mwenye mwono wa kinabii kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake. Familia ya Mungu inaendelea kumsindikiza kwa sala na sadaka ili aweze kutekeleza utume wake wa mageuzi ya kimisionari. Katika pango hifadhi ya nyaraka za Maaskofu, hakuna mahali ambapo Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alipotoa adhabu ya kumfungia huduma Askofu mkuu mstaafu McCarrick hadi katika siku za hivi karibuni, shutuma hizi zilipoibuka kwa kasi cha Baba Mtakatifu Francisko kuchukua maamuzi magumu ya kumsimamisha na hatimaye, kumwondoa kutoka katika orodha ya Baraza la Makardinali ili kupisha uchunguzi wa shutuma hizi na hatimaye, maamuzi kuweza kutolewa kwa kuzingatia ukweli na haki.

Tangu Mwaka 2006 Askofu mkuu mstaafu McCarrick alishauriwa kutojishughulisha na shughuli za kichungaji hadharani na badala yake, alitakiwa “kujichimbia” katika maisha ya upweke, sala na tafakari kwa ajili ya toba na wongofu wa ndani! Huu ni wosia uliotolewa na Kardinali Giovanni Battista Re, aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu wakati huo. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kardinali Ouellet, amekuwa makini sana katika uteuzi wa Maaskofu wapya na kwamba, kwa wale Maaskofu na viongozi wa Kanisa wenye matatizo na changamoto za maisha na utume wao wa Kikuhani, amekuwa akiwashughulikia kwa: upendo, huruma na umakini mkubwa, jambo linaloweza kushuhudiwa katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Dhamana na utume wake, kama Padre, Askofu mkuu na hatimaye Kardinali, McCarrick haukuwa na utata wowote, hadi pale shutuma za nyanyaso za kijinsia zilipoanza kulipuka kama “moto wa mabua” na hivyo kuanza kuchafua hali ya maisha na utume wa Kanisa ndani na nje ya Marekani na Papa Francisko akamsimamisha mara moja. Msimamo wa Vatican kwa sasa ni kuhakikisha kwamba, inawashughulikia kadiri ya sheria, kanuni na taratibu za Kanisa, wale wote watakaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo na wale wote watakaowalinda na kwamba, kashfa ya nyanyaso za kijinsia haitavumiliwa tena ndani ya Kanisa.

Kardinali Marc Ouellet, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu amewataka Maaskofu kuwa waaminifu kwa kusimamia na kutangaza ukweli na tunu msingi za Kiinjili badala ya kuwachafulia watu majina na hivyo kusababisha mahangaiko makubwa kwa watu wa Mungu kwa shutuma zisizokuwa na “kichwa wala miguu” kama njia ya mtu kutaka kujijenga kisiasa. Kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani na nje ya Marekani kisiwe ni kisingizio cha kutaka kumpokonya Baba Mtakatifu Francisko dhamana yake ya kimaadili kwa watu wa Mungu.

Papa Francisko ni kiongozi ambaye amekuwa ni mfano bora wa kuigwa katika kuishi mashauri ya Kiinjili kwa kutoa kipaumbele cha kwanza: kwa utu, heshima, ustawi na maendeleo ya wengi; haki na amani na kwamba, anapania kwa nguvu zake zote kutangaza Furaha ya Injili pamoja na kuhakikisha kwamba, Injili ya upendo inamwilishwa katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.

Mwishoni, Kardinali Marc Ouellet anamwalika Askofu mkuu Carlo Maria Viganò ambaye amewahi kuwa Balozi wa Vatican nchini Marekani, kutubu na kuomba msamaha kwa shutuma zisizokua na ukweli dhidi ya Baba Mtakatifu Francisko. Amtambue kuwa kweli ni mchungaji makini, mwenye huruma na mapendo kwa watu wa Mungu, aliyekirimiwa neema ya kinabii, ili kusimamia mchakato wa wongofu wa kimisionari unaotekelezwa ndani ya Kanisa.

Kardinali Marc Ouellet

 

09 October 2018, 10:00