Vatican News
Siku kuu ya Deepavali: Wakristo na Wahindu washikamane kulinda maskini na wanyonge katika jamii! Siku kuu ya Deepavali: Wakristo na Wahindu washikamane kulinda maskini na wanyonge katika jamii!  (ANSA)

Siku kuu ya Deepavali: Shikamaneni kulinda na kuwatetea wanyonge!

Siku kuu ya “Deepavali” au “Diwali” yaani “Sherehe mwanga” kwa waamini wa dini ya Kihindu, linawaalika: Wakristo na Wahindu kushikamana kwa ajili ya ulinzi wa watu wanyonge ndani ya jamii”. Kilele cha sherehe hii ni tarehe 7 Novemba 2018.

Na Padre Richard A. Mjigwa. C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku kuu ya “Deepaval” au “Diwali” yaani “Sherehe mwanga” kwa waamini wa dini ya Kihindu, linawaalika: Wakristo na Wahindu kushikamana kwa ajili ya ulinzi wa watu wanyonge ndani ya jamii”. Kilele cha sherehe hii ni tarehe 7 Novemba 2018. Askofu Miguel Angel Ayuso Guixot, MCCJ, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini anasema, maadhimisho ya sherehe hii kwa mwaka huu, yasaidie kujenga na kudumisha moyo wa urafiki na udugu kati yao; amani na furaha katika familia na jumuiya katika ujumla wake.

Taarifa kutoka katika njia mbali mbali za mawasiliano ya jamii zinawasaidia waamini wa dini hizi mbili kutambua mateso na mahangaiko ya watu wanyongne ndani ya jamii. Hawa ni: maskini, wagonjwa, wazee, walemavu, waliotelekezwa, wahamiaji na wale ambao wanatengwa mintarafu misimamo ya: kijamii, kidini, kitamaduni na kilugha. Kuna waathirika wa nyanyaso na mashambulizi, wengi wao ni watoto na wanawake. Haya ni makundi ya watu ambao hawawezi kujilinda wenyewe; wanabezwa na kudharauriwa kiasi cha kusukumizwa pembezoni mwa jamii na hivyo kiasi kwamba, mahangaiko yao kama binadamu yanasahaulika. Wanyonge sehemu mbali mbali za dunia, ndio wanaoteseka sana!

Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini linasema, kutokana na changamoto hii, Wakristo na Wahindu, wanaweza kuunganisha nguvu zao ili: kuwalinda, kuwatetea na kuwahudumia watu hawa, kwani huu ni wajibu wa kimaadili mintarafu imani ya waamini wa dini hizi mbili, kwani wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, na hivyo ni ndugu wenye utu sawa, wanaowajibikiana kwa kutambua kwamba, hata wao ni dhaifu na wakati mwingine wanahitaji pia msaada kutoka kwa jirani zao. Uelewa wa dhati kabisa kuhusu hali yao ya kibinadamu na wajibu wao wa kimaadili, vinawasukuma kusimama kidete na kuwapatia huduma makini, bila kusahau kulinda, kutetea haki zao msingi na kuwarejeshea tena utu na heshima yao kama binadamu!

Hizi ni juhudi ambazo zinaendelea kutekelezwa sehemu mbali mbali za dunia, lakini kutokana na wimbi kubwa la waathirika, hii inakuwa ni changamoto changamani, ili kuweza kukidhi mahitaji yao msingi ambayo kwa sasa yanaonekana kuwa kama “tone la maji baharini”. Lakini, ikumbukwe kwamba, hawa ni watu wanaoishi katika jamii, wanaohitaji kuonjeshwa moyo wa upendo na mshikamano, ili kufurahia uwepo wa ndugu zao, wanaojitaabisha, kuwafungulia nyoyo na hazina ya maisha, ili kuwawezesha kujisikia kuwa ni marafiki na ndugu zao! Ustawi na maendeleo ya jamii yoyote unapimwa kwa jinsi ambavyo jamii inawashughulikia maskini.

Umakini na ushirikiano ni mambo msingi katika kulinda na kudumisha haki msingi za watu wanyonge ndani ya jamii na hivyo kurutubisha pia utamaduni wa huduma kwa jamii ya watu maskini. Kuwepo na mazingira kiasi kwamba, kila mtu ndani ya familia anajisikia kwamba anapendwa, anathaminiwa na kushirikishwa kikamilifu. Kwa viongozi wa serikali na wanasiasa waliopewa dhamana ya kulinda haki zao msingi, wahakikishe kwamba, wanawaonesha uso na moyo wa binadamu, wanyonge na maskini katika jumuiya; watu ambao wananyanyaswa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii.

Askofu Miguel Angel Ayuso Guixot, MCCJ, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini anahitimisha ujumbe wake kwa kusema, ukarimu huu unapaswa kuwa ni ushuhuda wa kazi ya huruma na upendo wa Mungu anayewalinda watu wake. Waamini wa dini hizi mbili wakiwa wameshikamana kadiri ya tamaduni na mapokeo yao ya kiimani, wakiwa pia wameungana na watu wote wenye mapenzi mema, waunganishe nguvu zao, ili kuwakirimia maskini na wanyonge furaha kwa leo na kesho yenye matumaini zaidi!

Sherehe ya Mwanga

 

31 October 2018, 15:48