Tafuta

Vatican News
Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho ni chemchemi ya huruma ya Mungu kwa waja wake. Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho ni chemchemi ya huruma ya Mungu kwa waja wake.  (ANSA)

Balozi wa Vatican azindua Kituo cha Hija Kitaifa, Kiabakari, Jimbo Katoliki Musoma!

Askofu mkuu Marek Solczyn'ski amdewataka waamini kukimbilia Sakramenti ya Upatanisho na Ekaristi kwa: imani, uchaji na ibada. Amri za Mungu na mashauri ya Kiinjili yawe ni dira na mwongozo wa maisha ya Kikristo ili Mungu apewe sifa na mwanadamu aweze kukombolewa. Kituo cha hija kitaifa cha huruma ya Mungu, Kiabakari, kiwe ni shule ya sala. toba wongofu wa ndani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, katika mkutano wake wa tarehe 21 Juni 2018, liliridhia ombi lililowasilishwa na Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma na kukipandisha hadhi kituo cha Huruma ya Mungu Kiabakari kuwa sasa ni Kituo cha Hija Kitaifa cha Huruma ya Mungu, Kiabakari. Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwamba,  Kituo hiki kitakuwa msaada mkubwa kwa Familia ya Mungu nchini Tanzania katika mchakato wa kuimarisha imani, malezi na majiundo makini, kwa wale wote wanaokimbilia na kuzama katika “Bahari ya huruma ya Mungu”.

Ndoto hii, imefikia hatima yake, hapo tarehe 3 Oktoba 2018, wakati Askofu mkuu Marek Solczyn’ski, wakati wa ziara yake ya kichungaji Jimbo Katoliki Musoma alipozindua kituo, kwa kushirikiana na Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma. Katika mahubiri yake, amemshukuru sana PadreWojciech Adam Koscielniak, Paroko wa Parokia ya Kiabakari, Jimbo Katoliki la Musoma, muasisi wa Parokia na Kituo cha Hija cha Kiabakari Jimbo Katoliki Musoma, chemchemi ya huruma ya Mungu ndani na nje ya Tanzania. Huyu ni mmisionari kutoka Jimbo kuu la Krakow, Poland, mahali wanapotoka Mtakatifu Yohane Paulo II na Sr. Faustina, Mitume wakuu wa Huruma ya Mungu. Ibada hii imemsaidia sana katika maisha na utume wake kuweza kueneza Ibada ya huruma ya Mungu.

Askofu mkuu Marek Solczyn’ski anakaza kusema, hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko amefanya hija ya kichungaji kwenye mji mkuu wa Vilnius, nchini Lithuania, mahali ambako Sr. Faustina kwa mara ya kwanza katika maisha yake, alisali Rozari Takatifu ya Huruma ya Mungu na kuchora Picha ya Yesu wa Huruma. Kumbe, wajibu, dhamana na utume wa Mama Kanisa ni kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na hivyo kumfungulia njia inayompeleka kwenye wokovu na maisha ya uzima wa milele. Haya ni matunda ya Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko kutoka kwa wafu.

Kwa njia ya Kristo Yesu watu wamekombolewa kwa kuoshwa dhambi zao kwa Damu Azizi. Kumbe, kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo na Upatanisho, Kanisa linawashirikisha watu matunda ya Sadaka iliyotolewa na Kristo Yesu pale Msalabani. Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma, upendo na msamaha na kwamba, huruma ndiyo sifa yake kuu. Damu Azizi ya Kristo iwaletee watu msamaha wa dhambi na hivyo kuwakirimia maisha ya uzima wa milele. Changamoto kubwa kwa waamini ni kuondokana na ubaridi wa maisha ya kiroho, unaoendelea kusababisha mateso makali kwa Kristo Yesu.

Waamini wameshauriwa kukimbilia Sakramenti ya Upatanisho na Ekaristi kwa: imani, uchaji na ibada. Amri za Mungu na mashauri ya Kiinjili yawe ni dira na mwongozo wa maisha ya Kikristo ili Mungu apewe sifa na mwanadamu aweze kukombolewa. Waamini waendelee kumtumainia Mungu kama ilivyokuwa kwa Mtume Toma baada ya kukumbana na kashfa ya Msalaba, akabahatika kugusa Madonda Matakatifu ya Yesu. Waamini wajenge moyo wa Ibada, Imani na Uchaji wa Mungu kwa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa kuondokana na ibada za mazoea. Kwa njia hii, wataweza kutakaswa kwa Damu Azizi ya Kristo na kushirikishwa Mkate wa uzima wa milele

Kituo cha Hija cha Kitaifa cha Huruma ya Mungu, Kiabakari, Jimbo Katoliki la Musoma, Tanzania, kiwe ni mahali pa sala na chimbuko la huruma ya Mungu kwa waja wake. Mtakatifu Sista Faustina na Mtakatifu Yohane Paulo II, Mitume Wakuu wa Huruma ya Mungu, wawaombee wote ambao mahali hapa patakatifu watamsihi Mungu msamaha wa dhambi zao na kushika njia ya wokovu.

Tukio hili lilitanguliwa na mapokezi makubwa yaliyofanywa na Familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Musoma, hapo tarehe 2 Oktoba 2018, huku wakiongozwa na Askofu Msonganzila, kwa kumpokea mgeni wao kwenye Daraja la Mto Suguti unaotenganisha Jimbo Katoliki la Bunda na Jimbo Katoliki la Musoma. Askofu mkuu Marek Solczyn’ski alipata nafasi ya kuzungumza na waamini wa Dekania ya Butiama, akatembelea shule ya awali na msingi ya Mwenyeheri Edmund. Baadaye, kulifuatiwa na mkesha wa nguvu uliosheheni tafakari za kina kuhusu Mitume wa Huruma ya Mungu, Mtakatifu Yohane Paulo II na Sr. Faustina.

Waamini waliweza kushiriki Ibada ya Upatanisho na maungamo ya mtu binafsi pamoja na maandamano makubwa ya Rozari Takatifu kuzunguka Kilima cha Kiabakari, yaani hadi raha wanasema, watu wa Mungu kutoka Kiabakari, eneo ambalo kwa sasa limegeuzwa kuwa ni chemchemi ya huruma ya Mungu ndani na nje ya Tanzania.

Nuncio Tanzania

 

08 October 2018, 09:52