Tafuta

Vatican News
Vitendo vya kigaidi vina madhara makubwa katika maisha na mafungamano ya kijamii. Vitendo vya kigaidi vina madhara makubwa katika maisha na mafungamano ya kijamii.  (AFP or licensors)

Mapambano dhidi ya vitendo vya kigaidi yapanie kungo'a mizizi yake!

Askofu mkuu Bernadirto Auza anasema katika kuongeza nguvu mapambano dhidi ya ugaidi, ni lazima Umoja wa Mataifa uzingatie utawala wa sheria, Makubaliano ya haki msingi za binadamu na sheria ya utu ili kuepuka vikundi vya kigaidi kutumia uvunjwaji wa haki kama vijisababu vya kufanya ghasia na kupandikiza vitendo vya chuki.

Na Padre Celestine Nyanda. - Vatican.

Katika mapambano dhidi ya ugaidi, uongozi wa Umoja wa Mataifa, hasa ule wa Baraza la Usalama, unapaswa kuchukua nafasi kubwa, kwa sababu Umoja wa mataifa una nyenzo nyingi katika kusaidia nchi wanachama zilizoko kwenye hatari ya mashambulio ya kigaidi, lakini zinajikuta na rasilimali chache katika kupambana na uovu huo. Askofu mkuu Bernadirto Auza, Mwakilishi wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, ndivyo anavyouasa uongozi wa chombo hicho kuweka pamoja rasilimali zake na zile za serikali husika ili kupambana na nadharia za kigaidi zisiendelee kusambaa, kwa namna hii ufanikishe kuzuia ghasia, uharibifu na hofu.

Uongozi wa mpango na shughuli za pamoja za Ofisi za Umoja wa Mataifa kupiga vita ugaidi ni muhimu sana katika kusaidia nchi wanachama. Ofisi za Umoja wa Mataifa, zisiishie kutazama uchambuzi wa amani na usalama kimazoea, bali zialike utendaji wa wataalamu wa haki za msingi za binadamu, maendeleo na elimu kati ya mambo mengine. Hii ndiyo namna bora itakayowezesha Umoja wa Mataifa kusaidia nchi wanachama kukabiliana na sera za vikundi vyenye misimamo mikali kabla ya ghasia zao kulipuka na kuwa tishio kubwa la amani na usalama kimataifa. Nguvu ya Umoja wa Mataifa ni za kipekee katika kusaidia nchi hizo katika hili, na hii ndiyo dhamana iliyopewa Ofisi ya Kimataifa ya kupambana na ugaidi.

Katika kuongeza nguvu mapambano dhidi ya ugaidi, ni lazima Umoja wa Mataifa uzingatie utawala wa sheria, Makubaliano ya haki msingi za binadamu na sheria ya utu ili kuepuka vikundi vya kigaidi kutumia uvunjwaji wa haki kama vijisababu vya kufanya ghasia na kupandikiza vitendo vya chuki. Askofu mkuu Auza anaalika Umoja wa Mataifa, Mashirika na Taasisi za kimataifa, kikanda na kitaifa zinazopambana na ugaidi, kuongeza nguvu katika kushirikiana na vyama vya kiraia na taasisi mahalia katika nchi husika ili kudumisha mafanikio kwa ufanisi mkubwa zaidi.

Mafanikio au kushindwa kwa mipango ya kupambana na ugaidi kunategemea sana ushirikishwaji wa uwezo na juhudi za watu mahalia, kwani serikali, taasisi na watu mahali ndio wapo karibu zaidi na ukweli na wenye fursa za kutosha kuwahusisha vijana katika elimu, ajira na mipango ya afya, kama sehemu mojawapo ya kutokomeza ugaidi. Ni taasisi na vyama vya kiraia vyenye uwezo na fursa kubwa kushinikiza serikali katika kuheshimu utawala wa sheria na haki msingi za binadamu. Haki hizi kwa namna ya pekee ni zile za uhuru wa kujieleza na kufanya mikutano ya hadhara, kwani ni moja ya mifumo ya kidemokrasia katika kutokomeza fujo na ghasia katika jamii.

Vatican inajihusisha na viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali ili kuweka nguvu ya pamoja katika kuzuia uchochezi wa chuki, ghasia, na ugaidi. Lengo la awali la Vatican ni kukuza moyo wa majadiliano ya kweli na ya kina kati ya dini na watu wa imani mbali mbali, pamoja na tamaduni tofauti, kwani baadhi ya vyanzo vya vitendo vya kigaidi ni misimamo mikali ya imani ama mtazamo potofu wa tamaduni, mila na desturi. Askofu Auza anamalizia hotuba yake kwa msisitizo kwamba, ugaidi ni tishio kwa wote, na hivyo ni lazima kupambana nao katika mfumo wowote unaobeba, kwa bendera yeyote unaopeperusha na kwa nyenzo zozote halali na za haki zinazowezekana, ili mradi tu kuhakikisha ugaidi unatokomezwa.

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

03 August 2018, 12:02