Tafuta

Vatican News
Usawa wa binadamu unafumbatwa katika utu na heshima yake kwani ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Usawa wa binadamu unafumbatwa katika utu na heshima yake kwani ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.  (AFP or licensors)

Usawa unapata chimbuko lake katika utu na heshima ya binadamu!

Jinsia ya kike na ya kiume ni sawa kwa misingi ya kupata mizizi yake kutoka kwenye uhalisia wa utu na heshima ya binadamu. Hata hivyo, tofauti za jinsia hizi mbili ni lazima zizingatiwe katika kuhusiana kifamilia, maeneo ya kazi na katika jamii kwa ujumla ili kutambua malengo na nafasi zake katika maisha ya mwanadamu.

Na Padre Celestine Nyanda. – Vatican.

Hivi karibuni, yaani tarehe 28 Juni 2018, Askofu mkuu Ivan Jurkovic, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko Geneva, Uswiss amechangia hoja kuhusu usawa kati ya wanaume na wanawake na umuhimu wa kuwawezesha wanawake kwa ajili ya maendeleo ya kila mwanadamu na maendeleo ya pamoja kama jamii.

Askofu mkuu Jurkovic analipongeza sana Shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa kwa kazi nzuri ambayo limeifanya katika kukuza uelewa na kuonesha mfano wa kuishi na kutenda kwa usawa wa kijinsia katika Ofisi zake na katika mipango mbali mbali linayoiendesha au kuisimamia. Kwa upande wa Vatican, usawa kati ya mwanaume na mwanamke unapata chimbuko lake kutoka kwenye utu wa mwanadamu mwenyewe, utu ambao hauwezi kufanyiwa hiana.

Hata hivyo ni muhimu pia kufahamu kwamba kanuni hiyo ya usawa inazingatia pia uzuri wa tofauti na kutegemezana kulikopo kati ya mwanamke na mwanaume. Jinsia hizi mbili zisichukuliwe kana kwamba ni nakala-mfanano kiasi cha kushindwa kuenzi utajiri wa tofauti zilizopo za maumbile, hulka, hisia, nafasi na uwezo kati ya jinsia ya kike na ya kiume. Kushindwa kutofautisha ni kupelekea kuzichanganya kana kwamba ni uhalisia ule ule jambo ambalo litakuwa ni kuonesha umaskini wa fikra na uelewa.

Jinsia ya kike na ya kiume ni sawa kwa misingi ya kupata mizizi yake kutoka kwenye uhalisia wa utu na heshima ya binadamu. Hata hivyo tofauti za jinsia hizi mbili ni lazima zizingatiwe katika kuhusiana kifamilia, maeneo ya kazi na katika jamii kwa ujumla ili kutambua malengo na nafasi zake katika maisha ya mwanadamu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, iwapo Familia ya binadamu inataka kupiga hatua katika maendeleo ya haki sawa kwa binadamu, ni lazima kuwapa wanawake nafasi za kutosha kusikilizwa na kutenda, lakini zaidi sana, sauti zao zipewe uzito katika maamuzi ya pamoja.

Vatican inatambua juhudi na hatua zilizoishapigwa na Shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa katika kulinda na kutetea usawa wa jinsia na kuwawezesha wanawake katika sekta na maeneo mbali mbali duniani. Hata hivyo bado kuna mengi yanahitaji kufanyika katika hili. Kwa sababu hiyo, Ujumbe wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko Geneva, unalialika Shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa kuwafikiria wanawake wenye uwezo ili kushika nafasi za juu za uwajibikaji katika Shirika hilo, na kuhakikisha linasimamia sera za kutovumilia hata kidogo unyanyasaji wa wanawake kwa namna yeyote ile.

Askofu mkuu Ivan Jurkovic anasema, kati ya nyanja za kuzingatia katika kufuta ubaguzi wa kijinsia ni pamoja na kuwashirikisha wanawake katika mchakato mzima wa kufanya maamuzi, kulipa ujira sawa kwa ajira ya nafasi sawa kwa wote na haki za wanandoa katika familia. Kwa sababu hiyo, wanawake wanaoamua kuwa mama, yaani kuzaa watoto, wasitengwe ama kuhatarisha ajira zao, bali haki zao zilindwe na utaratibu mzuri uwekwe ili waweze kufanya huduma zote hizo vema, yaani kuwa watumishi na wakati huo huo kuwa wazazi kamili katika familia zao, na hasa kwenye malezi ya watoto.  

Kumbe, sera za Shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa zizingatie umuhimu na nafasi ya familia inayoundwa kwa ndoa kati ya mwanamke na mwanaume kijinsia asilia, kwani familia ndicho kiini cha jamii bora. Msimamo huu ndio utakaosaidia kuepuka malengo mengine yanayotokana na mitazamo hafifu ya familia inayochanganya na kuvuruga watu. Jinsia itambulike kuwa inapata asili yake kutoka kwenye utambuzi wa kibaiolojia wa mwanamke ama mwanaume na wala sio vinginevyo.

Unaweza kusikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

07 August 2018, 12:10