Cerca

Vatican News
Haki msingi za binadamu, usalama wa raia, amani na utulivu ni mambo muhimu katika mipango miji! Haki msingi za binadamu, usalama wa raia, amani na utulivu ni mambo muhimu katika mipango miji! 

Haki msingi za binandamu, mendeleo ya miji na usalama wa wahamiaji ni mambo ya kuzingatiwa

Mkataba wa Kimataifa wa usalama wa wahamiaji umekuwa katika mazungumzano ya ushirikishaji kati ya serikali za Jumuiya ya Kimataifa, kwa lengo la kusuka kitendea kazi fumbata ili kuboresha sera na utekelezaji kimataifa wa kuhusika na suala la wahamiaji ili lilete faida kwa wote, bila kumuacha yeyote nyuma.

Na Padre Celestine Nyanda. - Vatican.

Uhamiaji ni agano katika matamanio asilia ya mwanadamu kutafuta furaha, fursa kubwa, maisha bora zaidi, na ni jibu la kawaida kabisa la mwanadamu wakati wa mahangaiko. Iwapo uhamiaji utaweza kushughulikiwa kwa taratibu nzuri na kwa nia njema, unaweza ukachangia vizuri katika maendeleo endelevu, ukuaji wa uchumi na afya ya jamii kitaifa, kikanda na kimataifa. Kwa namna hii, hivi karibuni, ndivyo Askofu mkuu Bernadirto Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa alivyoanza kutikisika ukumbi wa mkutano wakati wa kikao cha 51 cha Tume ya Kimataifa ya idadi ya watu na maendelo.

Mkataba wa Kimataifa wa usalama wa wahamiaji umekuwa katika mazungumzano ya ushirikishaji kati ya serikali za Jumuiya ya Kimataifa, kwa lengo la kusuka kitendea kazi fumbata ili kuboresha sera na utekelezaji kimataifa wa kuhusika na suala la wahamiaji ili lilete faida kwa wote, bila kumuacha yeyote nyuma. Mwono huu ni ule unaomuweka mwanadamu kuwa kiini katika changamoto ya wimbi la wahamiaji. Hivyo mbali ya kutazama haki za mataifa kulinda mipaka, unatazamwa pia wajibu wa kila taifa kulinda na kutetea haki msingi, uhuru na utu wa kila binadamu bila kubagua hali yake kijamii kama mhamiaji.

Kadiri ya Tamko la New York, namna ya kukabiliana na changamoto ya wahamiaji kimataifa inayozingatia mwanadamu kwanza, inapaswa kwanza kabisa kuhakikisha haki za kila mmoja kubaki katika nchi yake asilia kwa amani, usalama na fanaka. Huu wajibu wa kuhakikisha kwamba uhamiaji unakuwa sio jambo la lazima bali ni uchaguzi wa mtu, ni jukumu msingi la kila taifa kuhakikisha linatafuta usalama na hali nzuri sio tu kwa ajili ya raia wake, bali kwa ajili ya watu wote, jambo ambalo limepewa kipaumbele na Agenda ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa kufikia 2030.

Jukumu hili lijikite kwanza kabisa katika mapambano dhidi ya umaskini na matabaka yanayopelekea watu kukimbia makazi yao na kuhamia sehemu nyigine ndani ya nchi, na wakati mwingine kufikia ulazima wa kuzikimbia kabisa nchi zao. Hii inahitaji uwekezaji wa muda mrefu kitaifa na kimataifa katika sekta ya elimu, afya, mipango miji, usafirishaji, na sera nzuri za ajila na kazi, pamoja na usalama kijamii. Hii ni namna ya mpango wa muda mrefu kuhakikisha kwamba uhamiaji sio tena suala la shuruti au kukata tamaa, bali ni uchaguzi hiari wa mtu.

Askofu mkuu Auza anasema, kwa miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na wimbi kubwa la wahamiaji kutokana na kinzani, myumbo wa uchumi, majanga asilia, na uharibifu wa mazingira. Mataifa mengi yamejikuta hayakujiandaa kukabili changamoto ya kupokea wakimbizi na wahamiaji na kuwapa huduma stahiki bila kuathirika kisiasa, kiuchumi na kijamii. Zaidi sana, kumeonekana kupotea sana nia ya kisiasa katika mataifa mengi kupokea wakimbizi na wahamiaji kwa kuheshimu na kulinda utu wao kama binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Matokeo ya haya yote, pamoja na njia finyu na wakati mwingine hatarishi kwa wahamiaji wakati wa safari zao kutoka mahala pamoja kwenda pengine, imekuwa ni biashara haramu ya binadamu, dawa za kulevya, utumwa mamboleo na mifumo mingine mingi ya unyanyasaji na unyonyaji. Haya yote chimbuko lake ni kukosekana kwa ushirki wa pamoja kutafuta mahitaji msingi kwa kila mmoja na kulinda haki na hadhi ya kila binadamu, kuanzia nchi za nyumbani na baadae ugenini.

Kufuatia maendeleo ya utandawazi na mahusiano kati ya mataifa, kila maamuzi na hatua zinazochukuliwa na nchi moja zinaathiri moja kwa moja nchi zingine. Kila taifa linalotaka kulinda na kudhibiti mipaka yake dhidi ya wahamiaji, ni lazima tu lifikirie mafao ya nchi majirani. Askofu mkuu Auza anasema, historia ya hivi karibuni imeifundisha dunia ya kwamba hakuna njia ya mkato kukabiliana na wimbi la wahamiaji, kama sio ushirikiano na mshikimano kimataifa. Sera na mipango ya muda mfupi ya kujibagua kitaifa kutokana na hofu, zitapelekea mpasuko na mahangaiko makubwa zaidi kwa siku za usoni. Hivyo ni muhimu kuitikia wito wa Baba Mtakatifu Francisko wa kujenga utamaduni wa kukutana ambao unatambua kwa unyenyekevu kuwa matatizo yanayowakumba watu walioko safarini, hayatatuliwi kwa utengano bali kwa mshikamano mkubwa na kujikita kutafuta mafao ya wengi.

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

09 August 2018, 08:17