Papa Francisko katika mkesha wa Siku ya Vijana Italia, 2018 Papa Francisko katika mkesha wa Siku ya Vijana Italia, 2018 

Vijana wa Italia wanasali kwa ajili ya Sinodi ya vijana, 2018

Vijana katika hija hii, wameonja udhaifu wa miili yao; wakagundua umuhimu wa uhuru unaowajibisha pamoja na kufanya maamuzi magumu, ili kuweza kufikia lengo la maisha! Katika hija hii, vijana wameweza kukutana na kufahamiana na vijana wenzao kutoka sehemu mbali mbali za Italia; wameshibishwa kwa ushauri na nasaha kutoka kwa walezi na viongozi wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wawakilishi 70, 000 wa vijana kutoka katika Majimbo 195 kati ya Majimbo 226 yanayounda Kanisa Katoliki nchini Italia, Jumamosi, tarehe 11 Agosti 2018 walitia timu kwenye Uwanja wa “Circo Massimo” ulioko mjini Roma, kwa ajili ya mkesha na Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, itakayoadhimishwa mjini Vatican, Oktoba 2018. Mkesha huu umeboreshwa kwa sala, tafakari, shuhuda, maungamano pamoja na kusherehekea zawadi ya maisha, kwa vijana kupata “muziki mnene” ndo raha ya maisha ya ujana, lakini fainali uzeeni!

Elena kwa niaba ya vijana wenzake kutoka sehemu mbali mbali za Italia katika salam zake kwa Baba Mtakatifu Francisko amesema, wakiwa wamesheheni furaha isiyokuwa na kipimo, vijana wa Italia wapo, jeuri na matumaini ya Kanisa, tayari kuitikia mwaliko kutoka kwa Kristo Yesu, njooni nanyi mtaona! Na kwa hakika wametembea kama mahujaji na kusali, daima wakiwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora. Hawa ni vijana wakakamvu na wenye ujasiri unaobubujika kutoka katika Injili ya Kristo. Njiani, wameshibishwa kwa Neno la Mungu na Mkate ulioshuka kutoka mbinguni, yaani Ekaristi Takatifu, ili kurutubisha maisha ya kiroho na kukata kiu ya upendo katika maisha ya ujana.

Vijana wanasema, katika hija hii, wameonja udhaifu wa miili yao; wakagundua umuhimu wa uhuru unaowajibisha pamoja na kufanya maamuzi magumu katika maisha, ili kuweza kufikia lengo la maisha! Katika hija hii, vijana wameweza kukutana na kufahamiana na vijana wenzao kutoka sehemu mbali mbali za Italia; wameshibishwa kwa ushauri na nasaha kutoka kwa walezi na viongozi mbali mbali wa Kanisa waliobahatika kukutana nao, lakini jambo la msingi ni kwamba, vijana wametambua kuwa, hata katika udhaifu wao, bado Mwenyezi Mungu anaweza kuwanyanyua kwa huruma na upendo wake na kuwasindikiza katika hija ya matumaini.

Mama Kanisa pia anaendelea kuwasindikiza hatua kwa hatua. Vijana wanamshukuru Baba Mtakatifu anayewataka kukaza macho yao kwenye Moyo Mtakatifu wa Yesu uliotobolewa kwa mkuki, humo zikabubujika Sakramenti za Kanisa, amana na utajiri unaowasukuma vijana kujisadaka pia kwa ajili ya huduma kwa jirani zao, ushuhuda wa furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Vijana wanamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu kwa ukarimu, sanaa na kipaji cha kusikiliza shida na matamanio halali ya vijana, na hatimaye, kuyafanyia kazi.

Vijana wanasema, hija yao kutoka sehemu mbali mbali za Italia, imewafikisha Roma,  kwani wanatamani kufanya hija pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Vijana wamempatia Baba Mtakatifu Fimbo ya kuchungia kondoo wake! Vijana wanasema, ikimpendeza Baba Mtakatifu katika unyenyekevu wake, wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, wangetamani kuiona akiwa anaitumia, ili kuwakumbusha tena maagano yao. Vijana wanaendelea kusali na kuwasindikiza Maaskofu katika maandalizi ya maadhimisho haya, ili kweli Sinodi hii iweze kuwa ni mwanga kwa vijana katika maisha na utume wa Kanisa kwa vijana. Wanataka kusikia na kuona Kanisa linalowasindikiza vijana! Vijana wamemhakikishia Baba Mtakatifu uwepo wao wa karibu kwa njia ya sala na kwamba, kwa hakika wanampenda sana!

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

11 August 2018, 13:18