Waamini wanaalikwa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia duniani! Waamini wanaalikwa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia duniani! 

Injili ya familia na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia!

Baba Mtakatifu Francisko kunako tarehe 15 Agosti 2016 alianzisha Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kama sehemu ya mchakato wa Sekretarieti kuu ya Vatican kusoma alama za nyakati na kujibu kwa ufasaha na weledi mkubwa changamoto mamboleo katika maisha na utume wa Kanisa, ili waamini waweze kutangaza na kushuhudia Injili ya familia duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na familia, kwa kutangaza na kushuhudia: ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia katika jamii. Kanisa linatambua kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, ni shule ya utakatifu haki na amani; ni mahali pa kujifunzia fadhila mbali mbali za Kikristo, kiutu na kijamii! Lakini, familia katika ulimwengu mamboleo inakabiliwa na changamoto pevu kama zilivyoainishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume, “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia”.

Injili ya Kristo ni chemchemi inayowapatia wanafamilia ari, nguvu na jeuri ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa nyakati hizi kwa kuzingatia tunu msingi za Injili ya familia mintarafu Mafundisho ya Kanisa. Ili kuweza kukabiliana na changamoto zote hizi, Baba Mtakatifu Francisko kunako 15 Agosti 2016 alianzisha Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kama sehemu ya mchakato wa Sekretarieti kuu ya Vatican kusoma alama za nyakati na kujibu kwa ufasaha na weledi mkubwa changamoto mamboleo katika maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu akamteua Kardinali Kevin Farrell kuwa Mwenyekiti wake wa kwanza. Hili ni Baraza ambalo kimsingi, linawahusisha watu wote wa Mungu katika maisha na utume wake! Changamoto kubwa ni kuwasaidia waamini walei kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; kuhakikisha kwamba, waamini walei wanashiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kama njia ya kuyakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Waamini walei wanapaswa kuwa kweli mstari wa mbele katika kutangaza na kushuhudia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, mintarafu mpango wa Mungu katika maisha ya binadamu, Mafundisho tanzu ya Kanisa, kanuni maadili na utu wema.

Kardinali Kevin Farrel anasema, anashirikiana na Padre Alexandre Awi Mello, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha. Hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko alimteua Linda Ghisoni kuwa Katibu mkuu msaidizi, Idara ya Walei na Gabriella Gambino kuwa Katibu mkuu Msaidizi, Idara ya Maisha. Mwezi Oktoba, 2017, Baba Mtakatifu Francisko alitembelea Makao makuu ya Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha ili kukutana na kusalimiana na wafanyakazi wa Baraza hili pamoja na kuwatia shime, kusonga mbele kwa imani na matumaini katika kukabiliana na changamoto za maisha ya ndoa na familia, wanapoendeleza sera na mikakati ya Injili ya familia kadiri ya mpango wa Mungu kwa binadamu!

Kama Baraza la Kipapa, changamoto kubwa iliyoko mbele yao kwa sasa ni mchakato wa kufanya kazi katika mwono na mawazo mapya, kwa kushirikiana ili kutoa huduma bora zaidi, kwa kutambua kwamba, Baraza hili linapaswa kufikiri na kutenda kama chombo kimoja, chenye idara mbali mbali. Ni chombo cha ushauri kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro na ambacho kinapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake, kwa kushirikiana kwa karibu sana na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, Vyama vya kitume pamoja na kuratibu maadhimisho makubwa ya Kanisa kama vile: Siku ya Vijana Kimataifa na Mkutano wa Familia Duniani ambao kwa mwaka 2018, unaadhimishwa huko Jimbo kuu la Dublin, nchini Ireland, kuanzia tarehe 22- 26 Agosti 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Injili ya familia: furaha ya ulimwengu”. Maandalizi haya yanaongozwa kwa namna ya pekee kabisa na Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia”.

Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 25 Machi 2017 alitoa mwongozo wa maandalizi ya mkutano huo ambao unapaswa kufuatwa kama sehemu ya tafakari ya Wosia wa Kitume, "Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia”. Swali la msingi hapa ni kujiuliza ikiwa kama Injili inaendelea kuwa ni sababu ya furaha kwa ulimwengu? Je, Familia bado inaendelea kuwa ni sehemu ya Habari Njema kwa ulimwengu mamboleo? Baba Mtakatifu anakiri kwa kusema kwamba, ni kweli familia inaendelea kuwa ni sababu ya furaha na Habari Njema kwa walimwengu, kwani, uhakika huu unafumbatwa katika mpango wa Mungu kwa mwanadamu; upendo ambao unapaswa kupewa jibu la “Ndiyo” na viumbe vyote kwani hiki ni kiini cha moyo wa binadamu.

Kardinali Kevin Farrel anasema, maadhimisho ya Siku ya IX ya Familia Duniani yanapania kuwa ni maadhimisho ya chemchemi ya furaha ya Injili ya familia kwa walimwengu, kwa kumshukuru Mungu kwa kuwajalia wanadamu uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia unaofumbatwa katika upendo wa dhati kati ya bwana na bibi na wala si vinginevyo! Huu ni upendo unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku, bila kusahau changamoto na mapungufu yanayomwandama mwanadamu! Bila upendo huu, si rahisi sana kuweza kuishi kama watoto wa Mungu, watu wa ndoa, wazazi na kama ndugu.

Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii kuhimiza umuhimu wa familia kuishi kwa kujikita katika upendo kwa ajili ya upendo na ndani ya upendo wenyewe. Hii ina maana kwamba wanandoa wanapaswa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusameheana, kuvumiliana na kuheshimiana. Anawaalika wanafamilia kumwilisha ndani mwao maneno makuu matatu: “Hodi, samahani na asante”. Mama Kanisa kila wakati anapata mang’amuzi ya udhaifu wa binadamu, ndiyo maana watu wote, familia pamoja na viongozi wa Kanisa wanapaswa kujenga tabia ya unyenyekevu uliopyaishwa, unaotamani kufundwa vyema; kuelimishwa ili uweze kuelimisha; kusaidiwa ili uweze kusaidia; kusindikiza, kung’amua, kuwaingiza na kuwashirikisha watu wote wenye mapenzi mema katika maadhimisho na ushuhuda wa mradi mkubwa wa upendo wa Mungu kwa binadamu unaofumbatwa katika Injili ya familia!

Ni matumaini ya Kardinali Kevin Farrel kwamba, Katekesi za Kimataifa zilizoandaliwa kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya IX ya Familia Duniani zitawasaidia waamini kujiandaa vyema kuadhimisha Sakramenti ya Ndoa Takatifu na hatimaye, kuimarisha familia, Kanisa dogo la nyumbani! Mpango wa Mungu kwa ajili ya familia ya binadamu ndicho kiini cha tafakari ya ukuu na utakatifu wamaisha ya ndoa na familia. Mama Kanisa anapenda kuhimiza pia umuhimu wa maisha ya sala na tafakari ya Neno la Mungu katika familia kwani familia inayosali, itashibana na kuungana wakati wote!

Wanandoa wanapaswa kuhakikisha kwamba, wanamwilisha ndani mwao ile ndoto ya Mungu kwa mwanadamu, kwa kutambua kwamba, binadamu katika maisha yake, anakabiliana na udhaifu pamoja na mapungufu yake, ndiyo maana, familia inapaswa kuwa ni shuhuda na chombo cha Injili ya maisha dhidi ya utamaduni wa kifo; familia inapaswa kuwa ni shuhuda wa Injili ya matumaini na chemchemi ya furaha kwa walimwengu mamboleo!

Kardinali Kevin Farrell anasema kwamba, maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kuanzia tarehe 22 - 27 Januari 2019 yanaongozwa na kauli mbiu “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; iwe kwangu kama ulivyosema”. Lk. 1:38. Tayari, Baraza la Maaskofu Katoliki Panama limebaini maeneo makuu yatakayotumika katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019. Vijana wameanza kuwasha joto miongoni mwa vijana wenzao kwa kuandika nembo pamoja na wimbo maalum utakaotumika kwa ajili ya maadhimisho hayo, ambayo kimsingi ni sehemu ya mbinu mkakati wa Mama Kanisa, katika mchakato wa uinjilishaji mpya, unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha linaendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na wadau mbali mbali ilikuhakikisha kwamba, linaunda Mfuko wa Mshikamano, utakaowawezesha hata vijana kutoka katika familia maskini kuweza kushiriki kikamilifu katika tukio hili muhimu sana, katika maisha na utume wa Kanisa kwa vijana wa kizazi kipya! Katekesi, malazi ya vijana, Msalaba wa vijana unaoendelea kutembezwa huko Amerika ya Kusini, sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa vijana ni kati ya mambo ambayo yanaendelea kuboreshwa kwa wakati huu. Baraza pia limeanza kuchapisha barua ya wazi kwa familia katika lugha mbali mbali, kama ushiriki wa Baraza katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Mawasiliano ni muhimu sana katika maisha ya ndoa na familia kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

 

Gabriella Gambino ndiye Katibu mkuu Msaidizi, Idara ya Maisha ambayo ina wajibu na dhamana ya kuhakikisha kwamba, Injili ya uhai inalindwa na kudumishwa dhidi ya utamaduni wa kifo; yaani tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi pale mauti yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Hii ni idara inayokazia mahitaji ya mtu mzima katika hatua zake mbali mbali za ukuaji. Idara hii inashirikiana na wadau mbali mbali ili kuhakikisha kwamba, utu, heshima na haki msingi za wanawake na watoto zinalindwa na kudumishwa. Hapa kanuni maadili na Mafundisho tanzu ya Kanisa yanapewa kipaumbele cha kwanza.

Hii ni Idara inayojihusisha pia na masuala ya: haki msingi ya maisha, tiba muafaka kwa maisha ya binadamu; sera na mikakati inayosaidia kulinda na kudumisha Injili ya uhai. Hapa, kuna ushirikiano mkubwa na mabaraza pamoja na taasisi nyingine zinazoendeshwa na kusimamiwa na Vatican, kwa mfano, Taasisi ya Kipapa kwa ajili ya Maisha ina uhusiano wa moja kwa moja na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha na kwamba, Baraza linawakilishwa na Monsinyo Carlos Simòn Vasquez katika Baraza la Taasisi ya Kipapa kwa ajili ya Maisha. Hii ni idara inayoratibu tafiti maalum kwa ajili ya maisha!

Kardinali Kevin Farrell anasema kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anatambua na kuthamini mchango wa wanawake katika maisha na utume wa Kanisa,  ndiyo maana amewateua wanawake kuwa ni Makatibu wakuu wa Idara ya Maisha na idara ya Walei. Baba Mtakatifu anaendelea kutafakari ni nani anayeweza kumpatia dhamana ya kuwa Katibu mkuu msaidizi Idara ya familia. Baraza hili linawashirikisha waamini walei kutoka katika medani mbalimbali za maisha, ilikuchangia uzoefu, mang’amuzi na weledi wao katika maisha na utume wa Kanisa. Baraza hili ni jukwaa la ushirikiano kati ya wanawake na wanaume kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Mungu. Marta Rodriguez ni afisa mwandamizi anayeshughulikia masuala ya wanawake katika Baraza hili!

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

15 August 2018, 09:00