Tafuta

Vatican News
Kanisa litaendelea kutetea na kudumisha haki msingi za wazawa dhidi ya ukoloni mamboleo Kanisa litaendelea kutetea na kudumisha haki msingi za wazawa dhidi ya ukoloni mamboleo  (AFP or licensors)

Kanisa litaendelea kutetea utu, heshima na haki msingi za wazawa!

Papa Francisko katika nafasi mbali mbali, na kwa namna ya pekee alipotembelea Amerika ya kusini amesisitiza matamanio yake ya kuwa sauti ya wazawa katika matarajio yao mema, na kujenga uelewa wa hadhara wa jinsi gani ardhi, tamaduni, haki, uchumi na utu wa wazawa unaendelea kutishiwa sababu ya mataifa makubwa na wafanyabishara wanaoangalia masilahi yao binafsi

Na Padre Celestine Nyanda. - Vatican.

Hivi karibuni, 19 Aprili 2018, katika Ofisi za Umoja wa Mataifa, Jijini New York, kumefanyika kikao kwa ajili ya kulinda na kutetea haki na utu wa watu wazawa wa eneo la Amazonia. Tukio hili linakuja takribani zaidi ya miaka kumi tangu Tamko la Kimataifa juu ya ulindaji wa haki za wazawa, ambapo mataifa na wawakilishi wa wazawa sehemu mbali mbali duniani wamekuwa wakiendelea kusisitiza juhudi na uwajibikaji wa pamoja katika kulinda na kutetea thamani na haki za wazawa zinazofumbatwa katika Tamko hilo la Kimataifa. Vatican inaendelea kusimamia mwaliko wake wa kuwachukulia kwa heshima wazawa katika vyombo vya kitaifa na kimataifa.

Askofu mkuu Bernadirto Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa anasema, hii sio nadharia, bali ni wajibu wa kila taifa kuhakikisha kwamba, hakuna lolote linalofanyika wala kuamuliwa bila kuwahusisha wazawa wa eneo husika kadiri ya Tamko la Kimataifa juu ya ulindaji wa haki za wazawa. Kiuhalisia, hii ni kuwapa wazawa haki zao za pamoja kuhusu ardhi yao na rasilimali zao. Kwa namna hii, wazawa wanahakikishiwa sauti yao kusikilizwa, lakini pia wanapewa fursa ya kushiriki katika nafasi za kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa ajili ya maendeleo yao wenyewe, na hivyo kuhakikisha utambuzi wao, malengo yao, hatima yao, na kuhakikisha mapatano ya kweli kati ya wazawa na serikali zao. Huo ndio mwelekeo wa kuleta maendeleo kwa manufaa ya wote.

Baba Mtakatifu Francisko katika nafasi mbali mbali, na kwa namna ya pekee alipotembelea Amerika ya kusini amesisitiza matamanio yake ya kuwa sauti ya wazawa katika matarajio yao mema, na kujenga uelewa wa hadhara wa jinsi gani ardhi, tamaduni, haki, uchumi na utu wa wazawa unaendelea kutishiwa sababu ya mataifa makubwa na wafanyabishara wanaoangalia masilahi yao binafsi na hata kuwa tayari kuharibu utajiri na hazina ya wazawa, kwa mataifa na wafanyabiashara hao kujinufaisha wenyewe bila kuwajali wazawa na maendeleo yao kwa siku za usoni na urithi kwa vizazi vyao. Kwa namna ya pekee mtazamo na mawazo ya Vatican vinaelekea katika msitu wa Amazonia, wenye ukubwa wa mraba maili milioni 2.1, unaosambaa katika nchi 9, ukikumbatia takribani idadi ya wazawa milioni 2.8, makabila 390, na lugha 240. Baba Mtakatifu Francisko alipotembelea Brazil mnamo 2013 alikumbusha ile roho ya uwajibikaji ambayo Kanisa inaguswa nayo kwa ajili ya wazawa, ardhi na kanda nzima ya Pan-amazonia.

Baba Mtakatifu anasema, uwepo wa Kanisa maeneo ya Amazonia, una utofauti wa aina yake, sababu Kanisa lipo Amazonia kwa lengo la kuishi na kubaki na watu wa Amazonia kwa kujali, kulinda na kutetea haki na utu wao, na sio kama wezi na wanyang’anyi wengine wanaokwenda maeneo hayo na mabegi na mifuko mikubwa mikubwa kupora mali na utajiri wa wazawa na kisha kukimbia baada ya kuliacha eneo na watu wake wamebaki katika umaskini na uharibifu mkubwa. Ndio sababu kanisa linajikita katika kuandaa watumishi wa Kanisa katika eneo mahalia na watendaji wengine kama walimu, wataalamu na viongozi wanaofaa kwa ajili ya wazawa, eneo na maendeleo yao.

Kwa kuonesha kujitosa kwake kwa ajili ya watu wa Amazonia, Baba Mtakatifu Francisko ameitisha Sinodi kwa ajili ya maaskofu wa Amazonia, itakayofanyika mwezi Oktoba 2019 mjini Vatican, itakayolenga kutafakari kinachofanyika na kinachohitaji kufanyika ili kuinua maendeleo ya pamoja ya wazawa mmoja mmoja, na kwa pamoja katika eneo zima, kulinda maisha yao, haki zao, tamaduni na ardhi. Pia kuwasaidia wale wasioishi eneo hilo kujifunza uelewa na hekima ya wazawa, wanaotambua na kuiheshimu ardhi na rasilimali zake kama zawadi ya thamani kutoka kwa Mwenyezi Mungu, zawadi inayowasaidia kuwa na mahusiano na mawasiliano mazuri na Mungu mwenyewe, wahenga na wanajamii wote. Watu wanaoitazama Amazonia kwa tamaa ya mali na uporaji, wakijifunza hekima hii, itawasaidia kuingia na kufanya shughuli zao katika eneo hilo bila kuharibu hazina zilizosheheni eneo hilo, na watalinda na kutetea haki na heshima ya wazawa, anasema Askofu mkuu Auza.

Baba Mtakatifu Francisko alipotembelea eneo la Amazonia huko Puerto Maldonado huko Peruvia, aliwasikiliza wazawa kwa utulivu, na kisha katika hekima yake akasema kuwa watu wa eneo hilo kwa sasa wanakabiliwa na changamoto kuu mbili: kwanza, ni uporaji mamboleo na shinikizo la wafanyabiashara wakubwa wenye nia ya kuweka mikono yao kwenye uchimbaji mafuta, gas, mbao, dhahabu na mfumo wa kilimo-viwanda, ambavyo ni sura mpya ya unyonyaji na unapelekea uharibifu mkubwa wa mazingira; pili ni sera zinazodai kuwa na lengo la kuhifadhi uasilia wa eneo la Amazonia, sera zinazopandisha bei ya rasilimali na malighafi, wazawa wanashindwa kumudu gharama hizo na kupelekea wengi wao kukimbia na kuwa wahamiaji nchi zingine, hasa vijana.

Kinachohitajika kwa sasa, ni kuvunja kitendawili cha kihistoria cha kuitazama Amazonia kana kwamba ni eneo lenye rasilimali isiyowezakuisha kwa wazawa. Kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume Laudato sì, juu ya Utunzaji wa Mazingira Nyumba ya wote, kwamba haiwezekani uchumi wa kimataifa ukafunika haki na mamlaka ya taifa. Ni muhimu kila mmoja kuwa makini na kuweka juhudi za makusudi kutunza rasilimali za nchi mahalia. Zaidi, lazima kutambua juhudi zinazowekwa na wazawa katika kulinda rasilimali zao na kuhusika katika maendeleo yao wenyewe.

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

10 August 2018, 16:31