Familia ni amana na utajiri wa binadamu. Familia ni amana na utajiri wa binadamu. 

Papa Francisko: Familia ni amana na utajiri wa dunia!

Baba Mtakatifu anasema haitoshi kuzungumzia umuhimu wa familia, bali kuna haja kwa serikali, watunga sera na watekelezaji wa sera na mikakati hii kuhakikisha kwamba, wanaibua mbinu mkakati utakaoziwezesha familia kutekeleza kikamilifu dhamana na wajibu wake ndani ya jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa Mwezi Agosti 2018 ni kwa ajili ya kuombea sera na mikakati madhubuti zitakazolinda familia kama amana na utajiri wa binadamu. Ujumbe huu wa Baba Mtakatifu kwa njia ya video unasambazwa sehemu mbali mbali za dunia kwa njia ya mtandao wa utume wa sala duniani. Na unaweza kupatikana kwa anuani ifuatayo: (www.thepopevideo.org). Baba Mtakatifu anakaza kusema, anapotafakari na kuzungumzia kuhusu familia, kichwani kwake, inamwijia picha ya amana na utajiri mkubwa ambao Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanadamu hapa duniani.

Baba Mtakatifu anasema, anatambua fika mchaka mchaka wa maisha unaozikabili familia nyingi duniani, kiasi hata cha kukumbwa na ugonjwa wa sonona. Ikiwa kama serikali mbali mbali zitashindwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa familia, hatari inaweza kuwa ni kubwa zaidi. Baba Mtakatifu anakaza kusema, haitoshi kuzungumzia umuhimu wa familia, bali kuna haja kwa serikali, watunga sera na watekelezaji wa sera na mikakati hii kuhakikisha kwamba, wanaibua mbinu mkakati utakaoziwezesha familia kutekeleza kikamilifu dhamana na wajibu wake ndani ya jamii.

Kumbe, hapa kuna haja ya kuwa na sera na mbinu mkakati wa kuendeleza na kudumisha familia. Baba Mtakatifu anatambua fika matatizo, changamoto na fursa mbali mbali, ambazo familia zinakumbana nazo katika uhalisia wa maisha ya kila siku. Anasifia mchango wa wazazi na walezi katika kurithisha tunu msingi za maisha kwa watoto wao. Kama sehemu muhimu ya malezi na makuzi ya watoto kuanzia kwenye familia hadi shuleni, Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa kuwa na watu rejea katika maisha, ili kupata malezi na makuzi bora.

Kwa njia hii, watoto wataweza kuongezeka kwa kimo na busara na kwamba, majadiliano kati ya wazazi na walezi ni muhimu sana kwa ustawi, maendeleo na makuzi ya watoto ambao kimsingi ni taifa la leo na matumaini ya kesho. Baba Mtakatifu anagusia pia dhamana ya uzazi, ulemavu katika familia na afya; mambo ambayo yanapaswa kuangaliwa kwa jicho la imani, vinginevyo, familia itageuka kuwa ni uwanja wa vita na patashika nguo kuchanika. Baba Mtakatifu anawaalika wale wote wenye dhamana ya maisha, malezi na makuzi ya watoto kuhakikisha kwamba, wanatekeleza wajibu huu nyeti kwa ari, moyo mkuu na unyenyekevu wa hali ya juu kabisa.

 

06 August 2018, 14:18