Tafuta

Vatican News
Utu, heshima na haki msingi za binadamu zipewe kipaumbele cha kwanza ktika sera na mikakati ya maendeleo fungamani. Utu, heshima na haki msingi za binadamu zipewe kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya maendeleo fungamani.  (AFP or licensors)

Maendeleo endelevu na fungamani yazingatie kanuni maadili, utu na heshima ya binadamu

Kardinali Turkson analipongeza Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo na Biashara, UNCTAD kwa juhudi linazofanya mpaka sasa kuhakikisha linatokomeza umaskini wa kupindukia, kukuza uchumi wa haki, usawa fungamani na kukabiliana na changamoto za biashara na maendeleo ya mahusiano ya fedha na teknolojia kimataifa.

Padre Celestine Nyanda. - Vatican.

Katika Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko Geneva, Uswiss, tarehe 6 Juni 2018, kumefanyika kikao cha 65 cha Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo na Biashara, ambapo Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Maendeleo Endelevu ya Binadamu, ameshiriki. Shirika hili lilianzishwa mnamo mwaka 1964 kutokana na kuridhia kwamba nchi zinazoendelea zinahitaji msaada kutoka kwa Jumuiya ya Kimataifa ili kufanikisha maendeleo endelevu na shirikishi. Miaka miwili iliyopita Jijini Nairobi, Shirika hili lilipyaisha tena dhamana hiyo na kwa namna ya pekee kuelekeza nguvu katika uchumi shirikishi.

Kardinali Peter Turkson katika hotuba yake kwenye kikao cha 65 cha Shirika hilo huko Geneva, anasema kwamba, maendeleo endelevu na shirikishi yanapaswa kutetea ukomavu katika kupiga hatua, na hii inamaanisha maendeleo fungamani ya mwanadamu yenye msingi wake katika kanuni maadili zinazoeleweka. Hata hivyo maendeleo fungamani haya yapo hatarini zaidi sasa kuliko wakati ambapo Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo na Biashara lilipoanzishwa. Vyombo vya juu vya uongozi wa Shirika hilo vimekwishajadili baadhi ya changamoto hizi zikiwa ni pamoja na mahusiano ya biashara, kukua kwa teknolojia mpya, jinsi soko la fedha linavyoyumbisha hali njema za binadamu na hali nyonge za mazingira, uchumi na siasa.

Mpango wa biashara za kimataifa na ajenda ya ajira uliopaniwa kushughulikiwa baada ya vita ya pili ya dunia, ulibaini kanuni ya msingi sana kwamba, ili mahusiano ya kimataifa kwenye biashara yaweze kusaidia maendeleo ya binadamu, yanapaswa kuwa ni sehemu fungamani ya ukuaji wa uchumi wa dunia ulio sawa. Uchumi huu ni ule ambao unalinda nchi husika dhidi ya tabia za unyonyaji na ubepari wa makampuni makubwa; utendaji wa pamoja unadhibiti matumizi na ugawanyaji wa rasilimali watu na rasilimali asilia; na nchi hizo zinakuwa zinachangia katika juhudi za kimataifa kila nchi kadiri ya uwezo wa maendeleo kiuchumi na kijamii.

Kardinali Turkson anapembua kwamba, ukuaji wa biashra kimataifa ulichukuliwa sio kama lengo la mwisho, bali ni nyenzo ya kuhakikisha uwepo wa amani thabiti na kukuza maendeleo sawa ya binadamu. Leo hii kinachokwamisha kufikiwa kwa malengo haya, sio tu kwamba kuna kinzani za kiuchumi na kisiasa kati ya mataifa makubwa katika biashara na wateteaji wa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu, bali zaidi sana, kuna ongezeko kubwa la mikataba na makubaliano kati ya pande mbili au makundi mengi ya kibiashara katika kanda. Mpasuko huu wa biashara na mijadala husika vimepelekea kufunguka kwa mianya mingi ya makumpuni makubwa kibiashara na hivyo kukandamiza sera za nchi na kupelekea mamilioni ya watu kuumia.

Tayari mwaka 1930, Papa Pius XI aliutahadharisha ulimwengu kwamba kuna hatari ya kuwa na utandawazi wa udikteta wa uchumi. Takribani miaka kumi baadae, Raul Prebisch, Katibu mkuu wa kwanza wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo na Biashara akasema kwamba, ongezeko la ufinyu wa masoko na nguvu ya makumpuni vimeshusha maendeleo ya nchi za kusini baada ya vita ya pili ya dunia, kitu ambacho kimepelekea ukuaji wa maendeleo na faida kwa nchi za kaskazini kwa mgongo wa biashara na uwekezaji kimataifa. Raul Prebisch alionya juu ya hatari ya kukauka kwa kipato cha watu kutokana na makumpuni ya biashara kuwa huru kuvuka mipaka ya nchi kwa kulinda masilahi yao zaidi bila kujali maendeleo ya watu mahalia na jamii husika kwa ujumla. Leo hii, ukuaji na upanukaji wa baadhi ya makampuni kisiasa na kiuchumi upo mbali sana zaidi ya takribani miaka 100 iliyopita.

Taarifa ya mwaka 2017 ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo na Biashara inaonesha kwamba kuna mzunguko wa kilema cha tamaa kila siku kutafuta donge nono zaidi la fedha ili kupata madaraka ama kutafuta madaraka ili kupata donge nono la fedha.  Tabia ya mzunguko wa kilema hichi imekwishaathiri kila maeneo yanayohusika na shughuli za fedha na uchumi na hata yale yasiyohusika navyo. Mzunguko wa kilema hiki umekuwa kikwazo kikubwa cha kuwa na mahusiano mazuri, shirikishi na yenye usawa katika uzalishaji. Kardinali Turkson anasisitiza kuwe na sera hai na zilizo kwenye mpangilio mzuri, pamoja na ushirikiano kimataifa ili kutawala vema uzalishaji na masoko katika uwiano sahihi na kurudisha tena biashara kimataifa katika lengo la maendeleo endelvu na fungamani.

Ukuaji wa haraka wa teknolojia ni sehemu ya kile ambacho Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo na Biashara linakiita mfumuko wa Utandawazi (hyperglobalization), ambao ni ukuaji wa ghafula na upanukaji wa viwango na malengo ya utandawazi kwa kasi kubwa. Kwa namna ya pekee teknolojia ya kidijitali imevunja mipaka ya kitamaduni kati ya taifa na taifa, na badala yake imefungua maeneo mengine ya fursa za kiuchumi na uwezekano wa biashara. Katika kiini cha teknolojia hizi mpya, kuna maendelo ya aina mbili.

Kwanza ni nafasi ya mwanadamu kuchukuliwa na akili ya kubumba, mfano roboti; na pili ni ukusanyaji, uchambuzi na usambazaji wa taarifa hata zile kubwa kwa kupitia internet na mifumo ya namna hiyo. Hata hivyo, bado kuna changamoto ya kufahamu vema athari za teknolojia hizi kwa maendeleo fungamani ya binadamu, anasema Kardinali Turkson. Ni muhimu kuepuka kwanza kabisa ule woga wa tishio la kushushwa hadhi ya ajira na wafanyakazi, lakini pia kuepuka kuamini kiwendawazimu kwamba ukuaji wa teknolojia hizi utaleta maendeleo kwa manufaa ya wengi. Zaidi sana, lazima kuweka tahadhari kwa kuruhusu kuibua uchambuzi wa kina, kabla ya kuweka sheria na sera stahiki za kujibu changamoto hizi.

Vatican kwa upande wake, kwa unyenyekevu wa uhakika inasimamia ukweli kwamba, hakuna eneo ama nyanja yeyote ya mwanadamu inayoweza kukaa nje ya kanuni maadili zenye msingi wake katika uhuru, ukweli, haki na mshikamano. Ikitokea mtu, kikundi ama taifa lolote kudai hilo, itakuwa ni kinyume cha sheria na ni uvunjaji wa haki. Hivyo hata katika maendeleo na matumizi ya teknolojia, ni lazima yote yatendeke kadiri ya kanuni maadili katika uhuru, ukweli, haki na mshikamano.

Ingawa utengenezaji wa sera za maendeleo na matumizi ya teknolojia zinahitaji ufahamu bora zaidi wa suala hilo, maamuzi yanayofanyika yasipingane na utu wa mwanadamu, bali yasaidie katika maendeleo fungamani. Sera hizo, ziepuke kabisa kupendelea tabia za unyonyaji na udikteta wa uchumi kwa wachache dhidi ya wengi wanaoumizwa. Hivyo sera hizo zizingatie namna ya kuendesha biashara kimataifa, ukuaji wa teknolojia, mahusiano ya kina kati ya wengi, maendeleo endelevu na fungamani, na ugawanyaji wa mali kwa haki na usawa. Kardinali Turkson anasema, inawezekana kabisa kwamba tishio kubwa katika kukuza na kutetea maendeleo fungamani ya mwanadamu linatokana na nafasi ya dunia ya fedha katika maisha ya kila siku. Mwaliko wa Vatican ni kudumisha jicho la karibu kwa mifumo na mihamala ya fedha isiyo halali, kwa hiyo lazima kualika pia wataalamu kutoka serikali mbali mbali ili kukabiliana na suala hilo katika mipango na sera za Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo na Biashara.

Vatican inaendelea kusisitiza kwa nguvu yale mahusiano mahususi kati ya fikra za kiuchumi na fikra za kimaadili. Kwa bahati mbaya sana, haya mahusiano yamevunjika katika maeneo mengi ya mifumo na sekta za fedha kimataifa, kiasi cha kukuza athari hasi za makampuni makubwa na biashara haramu. Utawala wa sheria katika umiliki na uendeshaji wa biashara hautoshi kufanyika katika kuweka tu sheria, kunahitajika nguvu ya ziada kiutendaji katika kukabiliana nayo, mfano wakwepa kodi na walanguzi wa maliasili. Vatican inaunga mkono juhudi za kuweka taratibu na sheria zilizo za haki katika mifumo ya fedha kama vile ukopeshaji na upangishaji. Kardinali Turkson anaongeza kwamba, ni tumaini la Vatican kwamba mifumo, mipango na utendaji wa namna hii utasaidia pia nchi zinazoendelea kuepuka mtego wa madeni yanayokuwa mzigo kulipa na kurudisha maendeleo ya taifa.

Kardinali Turkson analipongeza Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo na Biashara kwa juhudi linazofanya mpaka sasa kuhakikisha linatokomeza umaskini wa kupindukia, kukuza uchumi wa haki, usawa fungamani na kukabiliana na changamoto za biashara na maendeleo ya mahusiano ya fedha na teknolojia kimataifa.

Sikiliza mwenyewe kwa raha zako!
02 August 2018, 14:44