Papa Francisko kukutana na kusali na vijana kutoka Italia, Jumamosi tarehe 11-12 Agosti 2018 Papa Francisko kukutana na kusali na vijana kutoka Italia, Jumamosi tarehe 11-12 Agosti 2018 

Vijana wa Italia kuwasha moto wa Sinodi ya Maaskofu, Roma!

Wawakilishi 70, 000 kutoka katika Majimbo 195 kati ya Majimbo 226 yanayounda Kanisa Katoliki nchini Italia, tayari wako njiani, huku wakifanya vituo vya maisha ya kiroho, kama sehemu ya majiundo yao ya kiroho na kiutu, ili hatimaye, kukutana na Baba Mtakatifu Francisko kwa mkesha na maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu mjini Vatican, tarehe 11-12 Agosti 2018.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Vijana kati ya miaka 16 – 30 kutoka sehemu mbali mbali za Italia, Jumamosi tarehe 11 Agosti 2018 watakutana kwa mkesha na Baba Mtakatifu Francisko, kwenye Uwanja wa Circo Massimo ulioko mjini Roma ili kufanya majadiliano ya ana kwa ana kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, itakayofanyika kuanzia tarehe 3 – 28 Oktoba 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, imani na mang’amuzi ya miito”.

Tukio hili litakamilishwa kwa Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na baadaye kufuatiwa na Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 12 Agosti 2018. Hii ni sehemu ya utekelezaji wa changamoto kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko anayelitaka Kanisa kujenga utamaduni na sanaa ya kusikiliza kilio na matamanio halali ya vijana wa kizazi kipya!

Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia ameyasema haya, Jumanne, tarehe 7 Agosti 2018 alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari mjini Vatican kuhusu tukio hili muhimu litakalowakusanya wawakilishi 70, 000 kutoka katika Majimbo 195 kati ya Majimbo 226 yanayounda Kanisa Katoliki nchini Italia. Vijana hawa tayari wako njiani, huku wakifanya vituo vya maisha ya kiroho, kama sehemu ya majiundo yao ya kiroho na kiutu. Mama Kanisa, daima amekuwa mstari wa mbele katika makuzi na majiundo makini ya watoto na vijana wa kizazi kipya.

Kwa namna ya pekee, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia limewataka vijana kufanya hija na kutembea kwa pamoja ili waweze kufahamiana, kuheshimiana na kuthaminiana hata katika tofauti zao msingi, tayari kujenga madaraja ya watu kukutana. Ni wakati wa kutoka katika ubinafsi na kuanza kujikita katika maisha ya kijumuiya. Kardinali Gualtiero Bassetti anawaalika vijana kuwashirikisha vijana wenzao yale wanayofaidika nayo katika malezi na majiundo ya maisha yao ya kiroho kwa kutumia mitandao ya kijamii. Hapa mkazo ni umuhimu wa majadiliano kati ya vijana wa kizazi kipya na Mama Kanisa, kwani Kanisa linataka kusikiliza kwa makini kilio cha vijana wa kizazi kipya.

Hawa ndio walengwa wakuu wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, matumaini, jeuri na mapambazuko ya Kanisa. Hapa kinachoangaliwa si idadi ya vijana wanaoshiriki, bali ujumbe kutoka kwa vijana na changamoto makini kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya vijana. Vijana kutoka majimbo mbali mbali ya Italia wanatembea kwa miguu, ili waweze kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linasema, hakuna kulala hadi kieleweke!

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

08 August 2018, 15:28