Tafuta

Vatican inaunga mkono mchakato wa udhibiti wa silaha ndogo ndogo na nyepesi duniani ili kudumisha amani na utulivu. Vatican inaunga mkono mchakato wa udhibiti wa silaha ndogo ndogo na nyepesi duniani ili kudumisha amani na utulivu. 

Vatican inaunga mkono mkakati wa kudhibiti silaha duniani!

Biashara haramu ya silaha ndogo ndogo na nyepesi ni tishio kwa amani, maendeleo na usalama duniani. Kwa sababu hiyo, Vatican inapaza sauti kualika juhudi za pamoja sio tu kutokomeza biashara haramu ya silaha ndogo ndogo na nyepesi, lakini pia kupambana na shughuli zote za uhalifu zinazohusiana na: ugaidi, biashara ya binadamu na utumwa mamboleo.

Na Padre Celestine Nyanda. – Vatican.

Vatican imeunga mkono Mpango Kazi na Nyenzo ya kimataifa ya Ufuatiliaji kuzuia, kupambana na kutokomeza biashara haramu ya silaha ndogo ndogo na nyepesi katika maeneo yote. Askofu mkuu Bernadirto Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, katika kikao cha tatu cha kupitia hatua zilizofikiwa mpaka sasa kwenye mpango kazi huo, anapongeza kazi iliyofanyika kwani kunaonekana kukua kwa uelewa wa kimataifa juu ya hitaji la kuzuia, kupambana na kutokomeza biashara haramu ya silaha ndogo ndogo na nyepesi.

Ongezeko la ukusanyaji taarifa, uzoefu na mazoezi inashuhudia kwamba, hata kama mpango kazi huu unasonga kwa taratibu na kusuasua, haidhuru sana kwani mafanikio yanaonekana kwa kiwango fulani katika kuliendea lile lengo la pamoja. Ujumbe wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa unatambua kwa namna ya pekee juhudi kubwa zinazofanywa na vyama vya kiraia na taasisi zisizo za kiserikali katika kufanikisha lengo hili. Hata hivyo, anakumbusha Askofu mkuu Auza, mshikamano mkubwa wa kimataifa unahitajika ili kuzuia, kupambana na kutokomezea mbali biashara haramu ya silaha ndogo ndogo na nyepesi.

Dunia salama ndiyo kiini cha maendeleo na upambanaji wa umaskini wa kupindukia. Mnamo mwaka 1967, Mwenyeheri Paulo VI alisema kwamba, maendeleo ni jina lingine la amani. Ukweli huu, kwamba jina lingine la amani ni maendeleo, umekuja kuakisiwa baadae kwenye Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa kufikia 2030 inaposema: hayawezi kuwepo maendeleo endelevu bila amani na haiwezi kuwepo amani bila maendeleo endelevu.

Biashara haramu ya silaha ndogo ndogo na nyepesi ni tishio kwa amani, maendeleo na usalama duniani. Kwa sababu hiyo, Vatican inapaza sauti kualika juhudi za pamoja sio tu kutokomeza biashara haramu ya silaha ndogo ndogo na nyepesi, lakini pia kupambana na shughuli zote za uhalifu zinazohusiana na biashara hiyo, mfano ugaidi, biashara ya binadamu, biashara haramu ya dawa za kulevya na uhalifu mipango. Kwa upande wake Vatican, kwa kutumia nyenzo zinazoendana na uwepo na utume wake, inaunga mkono juhudi za kupambana na biashara haramu ya silaha ndogo ndogo na nyepesi, ili utendaji wa pamoja kimataifa ufanikishe kuifikia ile amani na utulivu ambavyo dunia ya leo ina kiu navyo sana.

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

07 August 2018, 10:58