Umuhimu wa kulinda na kutunza mazingira kwa ajili ya mafao ya wengi Umuhimu wa kulinda na kutunza mazingira kwa ajili ya mafao ya wengi 

Umuhimu wa kulinda na kutunza bahari kwa mafao ya wengi!

Shughuli za kibiashara zenye mahusiano na nishati ya maji, utamaduni na vyanzo vingine vya nishati, suala la tiba na afya, teknolojia ya kibaiolojia, uchimbaji wa madini na usafirishaji katika maeneo nje ya mipaka ya kitaifa ni mambo yanayochangia ongozeko la idadi ya watu, ukuaji wa uchumi, maendeleo ya teknolojia,

Na Padre Celestine Nyanda. - Vatican.

Hivi karibuni, 16 – 18 Aprili 2018, Jijini New York katika kumbi za Umoja wa Mataifa kumefanyika mkutano shirikishi wa serikali za Jumuiya ya Kimataifa ili kusuka nyaraka fungamani ya kisheria juu ya utunzaji na ulindaji wa matumizi ya viumbe hai baharini katika maeneo yaliyo nje ya mipaka kitaifa. Katika mkutano huo Askofu mkuu Bernadirto Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, amefungua hotuba yake kwa kukumbusha kwamba ulindaji na utunzaji bora wa sayari dunia kwa nyenzo zote ikiwemo utawala wa sheria ni jukumu-amri la pamoja.

Shughuli za kibiashara zenye mahusiano na nishati ya maji, utamaduni na vyanzo vingine vya nishati, suala la tiba na afya, teknolojia ya kibaiolojia, uchimbaji wa madini na usafirishaji katika maeneo nje ya mipaka ya kitaifa ni mambo yanayochangia ongozeko la idadi ya watu, ukuaji wa uchumi, maendeleo ya teknolojia, kupanuka kwa uelewa wa sayansi na mmong’onyoko wa kingo maeneo ya maji. Hii ni changamoto kubwa katika maendeleo ya mwanadamu na mahitaji yake msingi. Kwa kuzingatia hayo, Ujumbe wa Vatican katika Umoja wa Mataifa, unapendekeza mambo mawili ya msingi katika kuzingatia uandaaji wa nyaraka nyenzo fungamani juu ya ulindaji na utunzaji wa matumizi ya bahari na viumbe vilivyomo.

Kwanza kabisa ni matumizi ya maneno kutunza na kulinda. Kutunza maana yake ni kuhifadhi hali asilia ya bahari na viumbe vilivyomo au kuchukua hatua kurudisha mazingira yake asilia ambayo kwa namna moja ama nyingine yameharibika. Wakati kulinda ni kuchukua hatua madhubuti ili kuhakikisha kwamba rasilimali zitokanazo na mazingira ya bahari zinaendelea kutumika na vizazi vijavyo.

Hivyo utunzaji unahusisha kuondoa matumizi na haki fulani zinazopelekea uharibifu wa mazingira-bahari, wakati ulindaji ni kuchukua maamuzi yanayoendana na kuruhusu matumizi halali na haki msingi za matumizi ya bahari na rasilimali zake. Taratibu za kisheria zimekwishasukwa kiasi kwamba shughuli za baharini zinazingatia kanda, sekta na sehemu mahalia kwenye mambo mfano uvuvi, usafirishaji, uchimbaji madini na uwindaji wa nyangumi kwa ajili ya mafuta, nyama au mifupa.

Jambo la pili ni mwono na mwelekeo wa utekelezaji wa nyaraka nyenzo fungamani, ambapo Jumuiya ya Kimataifa itapaswa kuzingatia, sio tu haki lakini pia uwajibikaji wa kila mmoja katika matumizi, utunzaji na ulindaji wa bahari na rasilimali zake. Kwa muda mrefu sasa na hata katika maandalizi ya mikutano ya Umoja wa Mataifa juu ya utunzaji wa mazingira Nyumba ya wote, msisitizo umekuwa ukiwekwa zaidi katika haki za kila taifa na wadau wafanyabiashara katika matumizi na ugawanyaji sawa wa faida na ushirikishaji wa teknolojia.

Askofu mkuu Bernadirto Auza anasisitiza kwamba, umefika wakati ambapo uwajibikaji wa kila taifa na kila mdau wa biashara kuzingatia nafasi yake ya uwajibikaji katika kutunza na kulinda nishati maji na rasilimali zipatikanazo majini. Wengi wanashobokea zaidi uwajibikaji katika bei na mbinu zinazotumika katika biashara, lakini hawaweki nguvu ya kutosha katika uwajibikaji wa matumizi bora, utunzaji na ulindaji wa bahari na rasilimali zake.

Ni jambo lisilopingika kwamba kuna mahusiano makubwa kati ya ukuaji wa shughuli za binadamu na kuzorota kwa afya ya mazingira baharini. Kufuatia kukua kwa mahitaji ya rasilimali za baharini, Vatican inatoa mwaliko kuboresha mshikamano wa pamoja wa kutengeneza nyaraka nyenzo fungamani kisheria kwa ajili ya mafao ya wengi kwa Familia ya binadamu kwa nyakati za sasa na kwa siku za usoni.

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

02 August 2018, 15:00