ETIOPIA Assemblea Plenaria di AMECEA ETIOPIA Assemblea Plenaria di AMECEA 

Yaliyojiri wakati wa kufungua Mkutano mkuu wa AMECEA, 2018

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA kuanzia tarehe 13 - 23 Julai 2018 linaadhimisha Mkutano wake mkuu wa 19 unaongozwa na kauli mbiu "Tofauti mtetemo, hadhi sawa, umoja wa amani ndani ya Mwenyezi Mungu kwenye Kanda ya AMECEA". Ni muafaka wa ukazia umoja na utofauti kadiri ya mpango wa Mungu kwa wanadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa. C.PP.S. - Vatican.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA kuanzia tarehe 13 - 23 Julai 2018 linaadhimisha mkutano wake wa 19 unaoongozwa na kauli mbiu “Tofauti mtetemo, Hadhi sawa, Umoja wa Amani ndani ya Mungu kwenye kanda ya AMECEA”. Kardinali Berhaneyesus Demerew Souraphiel, Mwenyekiti wa AMECEA, ameufungua mkutano huu rasmi kwa Ibada ya Misa Takatifu, Jumapili, tarehe 15 Julai 2018, kwa kukazia umoja, upendo na mshikamano wa familia ya Mungu katika nchi za AMECEA ambazo kwa miaka ya hivi karibuni zimetikiswa sana na kinzani pamoja na mipasuko ya kisiasa ambayo imepelekea machungu katika maisha ya watu wengi.

Kardinali Berhaneyesus Demerew Souraphiel, anamshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amewezesha tena mchakato wa haki, amani na maridhiano kuanza tena kati ya Ethiopia na Eritrea, kwa kuwekeana mkataba wa amani hapo tarehe 9 Julai 2018 baada ya vita na misigano iliyodumu kwa takribani miaka ishirini. Katika kipindi chote hiki, AMECEA imekuwa ikishiriki kikamilifu katika mchakato wa kutafuta amani na maridhiano na sasa AMECEA inafurahi kuona matunda ya juhudi hizi ambazo ni upatanisho, amani na umoja kati ya nchi hizi mbili, ambazo hapo awali zilikuwa ni nchi moja hadi kunako mwaka 1991 zilipotengana!

Mkutano huu unahudhuriwa pia na wajumbe kutoka Gjibuti na Somalia, nchi ambazo bado zinaogelea katika kinzani na mipasuko ya kijamii. Ni matumaini ya AMECEA kwamba, Sudan ya Kusini ambayo tangu ijipatie uhuru wake, imeendelea kupambana na hali ngumu ya maisha kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe, itaiga mfano bora kutoka kwa Ethiopia na Eritrea na hivyo kuanza kuandika ukurasa mpya wa haki, amani, ustawi na maendeleo endelevu ya wananchi wake, ambao bado wamezama katika umaskini, magonjwa na ujinga; matokeo ya vita ya wenyewe kwa wenyewe pamoja na kinzani za kijamii.

Kardinali Berhaneyesus Demerew Souraphiel, amelishukuru Baraza la Kipapa la Mawasiliano kwa kuendelea kurusha matangazo kwa lugha Amharic na Kitigrinya, lugha ambazo zinatumika Ethiopia na Eritrea, hali ambayo pia imesaidia sana kukuza moyo wa majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Tema inayoongoza Mkutano mkuu wa 19 wa AMECEA imechaguliwa kwa kusoma alama za nyakati. Lengo ni kusaidia kuhamasisha umoja, upendo na mshikamano unaofumbatwa hata katika tofauti zao msingi, ziwe za kikabila, kidini na kitamaduni kama inavyoshuhudiwa katika Nchi za AMECEA.

Tangu Maaskofu wa AMECEA walipowasili, Ijumaa tarehe 13 Julai 2018, wamepata fursa ya kufunga na kusali pamoja na kusikiliza mada ambazo zimewasilishwa na Askofu mkuu mstaafu Telesphore Mpundu wa Jimbo kuu la Lusaka, Zambia na Padre Ferdinand Lugonzo, Katibu mkuu wa AMECEA kuhusu: moyo na utume wa AMECEA. Wamesikiliza hotuba mbali mbali za ufunguzi kutoka kwa viongozi wa Serikali na Kanisa na kwa namna ya pekee kutoka kwa Askofu mkuu Luigi Bianco, Balozi wa Vatican nchini Ethiopia. Wamesali  na kuwaombea Maaskofu walioaga dunia wakiwa na tumaini la ufufuko na maisha ya uzima wa milele kati ya mwaka 2014 hadi mwaka 2018. Mababa wa AMECEA wamesomewa pia ujumbe wa upendo na mshikamano kutoka katika taasisi mbali mbali na wadau katika huduma fungamani na endelevu kwa familia ya Mungu katika nchi za AMECEA.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu katika hotuna yake elekezi, amezitaka nchi wanachama wa AMECEA kujenga na kudumisha: umoja, upendo na mshikamano kati yao, ili kukuza haki, amani na maridhiano kati ya watu, tayari kuambata na kukumbatia changamoto ya mageuzi ya miundo mbinu ya maisha na utume wa Kanisa mintarafu sera na mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji unaotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu. Huu ni wakati muafaka wa kuangalia sera na utekelezaji wake, ili kuhakikisha kwamba, huduma makini inayokusudiwa kwa ajili ya watu wa Mungu Afrika Mashariki na Kati, inawafikia kwa ubora uliotukuka.

Askofu mkuu Rugambwa, amewakumbusha Mababa wa AMECEA mchango mkubwa uliotolewa na Mwenyeheri Paulo VI, katika Waraka wake wa kitume “Africae Terrarum” yaani “Bara la Afrika” uliochapishwa kunako tarehe 29 Oktoba 1967 ambamo anakazia pamoja na mambo mengine: Utajiri, amana na urithi mkubwa wa Mapokeo kutoka Barani Afrika sanjari na mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu.

Mwenyeheri Paulo VI, alikazia umoja na mshikamano kama chachu msingi ya maendeleo endelevu na fungamani, kwa kutambua kwamba, Bara la Afrika lilikuwa limebarikiwa kuwa na tunu msingi za maisha ya kifamilia, kiroho, kiutu na kijamii; tunu ambazo zinapaswa kuendelezwa ili kupambana na ubaguzi, ukabila, udini, vita na misigano, tayari kujikita katika mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani, haki msingi za binadamu, ili hatimaye, kufutilia mbali maadui wakuu wa Afrika ambao ni ujinga, umaskini na magonjwa.

Mwenyeheri Paulo VI alionesha pia matumaini ya Bara la Afrika wakati ambapo nchi nyingi zilikuwa zinajipatia uhuru wake; vikwazo na vizingiti ambavyo vilikuwa mbele yao na kwamba, maendeleo na msaada wa hali na mali ni mambo msingi katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Aliwataka Wakleri na watawa kujikita zaidi katika utamadunisho na huduma makini kwa watu wa Mungu, kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kwa viongozi wa Serikali, alikazia umuhimu wa kukuza na kudumisha uhuru wa kidini, demokrasia ya kweli na uhuru na kwamba, wanazuoni na wasomi, wasadake maisha yao kwa ajili ya maendeleo ya Bara la Afrika. Alizitaka familia kuwa ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu kwa mwanadamu, bila kusahau kuheshimu, kulinda na kudumisha haki, utu na heshima ya wanawake wa Bara la Afrika. Askofu mkuu Rugambwa anasema, Waraka huu unapaswa kupitiwa na kupyaishwa kwa kusoma alama za nyakati Barani Afrika na kwamba, ustawi na maendeleo ya Bara la Afrika yanawategemea waafrika wenyewe!

Sikiliza

 

 

16 July 2018, 16:22