Tafuta

Vatican News
Vijana wana kiu ya haki na amani duniani. Vijana wana kiu ya haki na amani duniani.  (ANSA)

Vijana wa kizazi kipya wana kiu ya haki na amani!

Injili ya amani ni kiu na matamanio ya watu wengi duniani, inayoweza kujengwa na kudumishwa katika umoja na utofauti wa watu kama ilivyokuwa kwa vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ambao wanashuhudia kwamba, amani ni inawezekana, ikiwa kama watu watajenga utamaduni wa kukutana; wataendelea kujikita katika: sala na mapendo kwa Mungu na jirani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kuanzia tarehe 30 Julai 2018 hadi tarehe 3 Agosti 2018, Mji wa Roma umefunikwa na watumishi wa Altareni zaidi ya sabini elfu, kutoka katika nchi 19 duniani walioitikia mwaliko wa “Associazione Internationalis Ministrantium, CIM, yaani “Chama cha Kimataifa cha Watumishi Altareni”, kinachoongozwa na Askofu Ladislav Nemet. Hija mwaka 2018 inaongozwa na kauli mbiu “Utafute amani ukaifuatie”. Hiki ni kilio, furaha na shukrani ya maskini mbele ya Mwenyezi Mungu, kwa huruma, wema na upendo mkuu aliomtendea na kwamba, anaona wajibu wa kushirikishana furaha na jirani zake.

Askofu Ladislav Nemet katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko ili aweze kuzungumza na watumishi wa Altareni, Jumanne, tarehe 31 Julai 2018, amesema, hija hii inapania pamoja na mambo mengine kuhakikisha kwamba, vijana wanamwilisha ndani mwao umuhimu wa kuthamini Injili ya uhai, daima wakitafuta amani ili kweli iwe ni sehemu ya maisha ya watu na wala si jambo la kufikirika! Injili ya amani ni kiu na matamanio ya watu wengi duniani, inayoweza kujengwa na kudumishwa katika umoja na utofauti wa watu kama ilivyokuwa kwa vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ambao wanashuhudia kwamba, amani ni inawezekana, ikiwa kama watu watajenga utamaduni na sanaa ya kukutana; wataendelea kujikita katika maisha ya sala, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa ambazo zinapaswa kumwilishwa katika upendo kwa Mungu na jirani.

Michezo na burudani ni mambo ambayo yanaweza kuwakutanisha vijana na kuanza kujikita katika mchakato wa kutafuta na kudumisha Injili ya amani. Vijana hawa 70, 000 kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wanataka kushuhudia mang’amuzi yao katika familia, jamii na kwenye nchi wanamotoka, jambo ambalo si rahisi sana kulitekeleza kutokana na uwepo wa changamoto changamani. Amani na utulivu ndicho kilio ambacho vijana hawa wamependa kumshirikisha Baba Mtakatifu Francisko ili aweze kuwasindikiza katika hija ya amani. Watumishi wa Altareni wanapenda kumuunga mkono Baba Mtakatifu katika juhudi zake za kuwa ni chombo na shuhuda wa amani sehemu mbali mbali za dunia. Wamempatia Baba Mtakatifu zawadi kutoka Marekani, Ujerumani na Ukraini, kama alama na ushuhuda kwamba, vijana wanataka amani na utulivu.

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

 

31 July 2018, 10:38