Tafuta

Vatican News
Vatican: Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi duniani: Usalama, utu, heshima na haki msingi za binadamu zizingatiwe na wote. Vatican: Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi duniani: Usalama, utu, heshima na haki msingi za binadamu zizingatiwe na wote.  (AFP or licensors)

Vatican: Usalama, utu na haki msingi za wakimbizi ni muhimu sana katika kukabiliana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani.

Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume kama Khalifa wa Mtakatifu Petro anaendelea kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: usalama, utu, heshima na haki msingi za wakimbizi na wahamiaji, kwani hata wao wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kanisa linakazia umuhimu wa kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwashirikisha katika maisha ya jamii husika.

Na Padre Celestine Nyanda. - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mnamo tarehe 7 Julai 2013 alitembelea Lampedusa, kisiwa kilichoko kusini mwa nchi ya Italia, katika bahari ya Mediterania, ambako kuna idadi kubwa ya wakimbizi na wahamiaji wanaofikia hapo wakati wa safari yao ya matumaini kupata hifadhi, unafuu wa maisha na usalama. Tendo hili la huruma kiroho na kimwili la Baba Mtakatifu Francisko liligusa hisia za watu wengi na kuonesha jinsi gani Kanisa linawajali na kuwahangaikia wahitaji, wanyonge na wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Mtazamo na juhudi za Kanisa kwa ushirikiano wa serikali na wote wenye mapenzi mema katika kuwahudumia wakimbizi na wahamijai, vikapelekea wimbi kubwa la wahamiaji kuingia Bara la Ulaya kati ya mwaka 2015 na 2016. Hali hii ikapelekea Umoja wa Mataifa kulazimika kufanya mkutano wa dharura huko New York Marekani mnamo Septemba 2016. Katika mkutano huo, viongozi wa dunia walionesha nia yao ya pamoja kuchukua hatua madhubuti ili kuokoa maisha ya wakimbizi na wahamiaji, kulinda haki zao msingi, kutafuta vyanzo vya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji, na kushiriki uwajibikaji wa pamoja kimataifa kukabiliana na changamoto hii.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mkutano huo, pamoja na vyanzo vinavyopelekea wimbi la wakimbizi na wahamiaji, aliwaalika viongozi wa kimataifa kutafuta mbinu mkakati wa kufutilia mbali sababu zinazopelekea umaskini na baa la njaa, kupata matokeo ya kuridhisha zaidi kulinda mazingira nyumba ya wote, kuhakikisha ajira zenye hadhi na mafanikio kwa wote, kutoa fursa za elimu bora na kulinda familia, kiini cha mendeleo ya mwanadamu na jamii kwa ujumla.

Tamko la New York lilipitisha mikataba miwili ya kimataifa kwa ajili ya usalama wa wakimbizi na wahamiaji, Global Compacts 2018. Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wakimbizi wa 2018, unatoa jibu la pamoja katika mpango kazi kimataifa kulinda wakimbizi kwa namna ambayo inafaa na yenye fanisi zaidi. Kwa upande wa Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji 2018, una lengo la kujadiliana na serikali mbali mbali ili kuhusisha Uhamiaji kimataifa katika nyanja zote, kwa namna ya pekee, kuwezesha uhamiaji salama, wenye taratibu madhubuti, kadiri ya sheria na uwajibikaji wa wote.

Vatican na Kanisa katika ujumla wake, vimekuwa vikitoa ushirikiano mkubwa katika mshikamano na uwajibikaji wa pamoja katika kuhudumia wakimbizi na wahamiaji. Mabaraza ya maaskofu, majimbo, parokia na taasisi mbali mbali duniani, vimekuwa mstari wa mbele kwa ushirikiano wa waamini na wote wenye mapenzi mema kuwakaribisha, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji. Padre Michael Czerny Katibu mkuu msaidizi wa Idara ya Wahamiaji na Wakimbizi katika Baraza la Kipapa la huduma ya maendeleo endelevu na fungamani anasema, haidhuru mtu una fursa ya kufanya tendo dogo kiasi gani, ni bora kulitenda hilo dogo kuliko kubaki umekodoa macho tu, au kufumba macho kana kwamba huoni, au kujiengua kana kwamba halikuhusu. Mtakatifu mama Theresa wa Kalkulta anasema, saidia mtu mmoja kwa wakati, na anza na aliye karibu yako zaidi.

Hivyo  Padre Michael Czerny anapendekeza watu wawaajili wakimbizi na wahamiaji; wawalipe ujira stahiki na kuwaheshimu; wawazungumzie vizuri katika vyombo vya habari na mitandao jamii, badala ya kuwarushia madongo kana kwamba ni mbu au wadudu wakunyunyizia dawa kali na kuwafukuzia mbali; wawafundishe lugha za mahali wanamojikuta na kupata hifadhi; wawahusishe katika sherehe za utamaduni na kuwafanya washirikishe tamaduni zao za chakula, mavazi na kadhalika. Matendo haya madogo madogo yatasaidia kuwakaribisha, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji, ili kujenga utamaduni wa kukutana na kushirikishana utajiri wa tofauti za mila na desturi, vipaji na weledi wa kila mmoja. Katika utendaji wa namna hii, kunahitajika huruma, mtazamo chanya na unaolenga mbali, pamoja na ujasiri mkubwa. Mwenyezi Mungu anawatia hamasa wahisani wa wakimbizi na wahamiaji: panua nafasi hemani mwako, tandaza mapazia hapo unapoishi, usijali gharama zake (Rej., Isaya 54:2).

Katika ujasiri huo, Padre Michael Czerny anaanza kwa kukosoa maneno yanayotumika kwenye baadhi ya mambo, mfano utumwa mamboleo. Iwapo jambo ni ovu, linabaki kuwa ovu, na lifahamike kuwa ovu bila kulitafutia namna ya kulipamba au kulipunguza makali. Kutoa uhai wa binadamu kwa karne za zamani na leo hii ni uovu ule ule, kusema ni cha kale au mamboleo kunaweza kusisaidie sana katika kupambana na kutokomeza maovu haya kama utumwa na biashara ya binadamu. Wengi hawapendi kukubali kwamba katika miji na nchi zao kuna maovu haya, na sababu ya kusita kukubali ni aibu inayoshushua nyuso za watu wanaoshiriki katika uovu huu.

Wanaohusika na maovu haya ni wengi, na ni ndugu, jamaa na marafiki. Kila anayeajiri watu kwa kuwatumikisha kwa ujira mdogo; anayetumia wanawake kwa kujiridhisha kwa ngono; anayetafuta picha na video za mambo machafu katika mitandao; anayesambaza dawa za kulevya; anayekwenda kupora rasilimali katika nchi zingine na kuwaacha raia wa eneno hilo bila kitu; anayefumba mdomo bila kukemea maovu haya; anayepaswa kuweka mpango mkakati na kutumia nguvu ya dola kuwakamata na kuwawajibisha wahusika wakuu wa maovu haya, na kadhalika.

Biashara ya binadamu na utumwa, pamoja na maovu mengine kimataifa yasingekuwepo kama isingekuwa kuhusika kwa baadhi ya viongozi wa jamii na vyombo vya usalama kwa namna fulani. Kila mmoja aweke juhudi kadiri ya nafasi na wajibu aliyo nao, vinginevyo maovu haya hayatakoma na wengi wataendelea kuumia sababu tu ya kutaka kuwa wakaidi kama Kaini na kujibu kwa kiburi na bila kujali: kwani mimi ni mlinzi wa ndugu yangu? (Rej., Mwanzo 4:9). Kila taifa linapaswa lipambane ili kujenga uchumi fungamani, utandawazi imara wa usafirishaji na mpango mkakati endelevu, ili kuhakikisha usalama na haki msingi za binadamu zinalindwa.

Sikiliza

 

20 July 2018, 17:02