Tafuta

Askofu mkuu Paul Richard Gallagher akisalimiana na Rais wa Korea ya Kusini Askofu mkuu Paul Richard Gallagher akisalimiana na Rais wa Korea ya Kusini 

Vatican yaitaka Korea kujikita katika matumaini na upatanisho

Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Vatican, katika ziara yake ya kikazi nchini Korea ya Kusini, ameitaka kuanza mchakato wa kujikita katika ujenzi wa matumaini, haki, amani na upatanisho miongoni mwa wananchi wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Vatican

Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa mjini Vatican, kuanzia tarehe 4-9 Julai, 2018 anafanya ziara ya kikazi nchini Korea ya Kusini. Akiwa huko amekutana na kuzungumza na Rais Moon Jae-in, huku akiwasilisha salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko ambaye anaendelea kuwatia shime kujikita katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi ili kuimarisha matumaini na maridhiano kati ya Korea ya Kusini na Korea ya Kaskazini.

Hatua inayofuatia kwa sasa ni kwa nchi hizi mbili anasema Askofu mkuu Gallagher ni kuanza kujielekeza zaidi katika huduma kwa ajili ya kukidhi mahitaji msingi sanjari na kuwajengea vijana utamaduni wa haki, amani na maridhiano; mambo msingi katika kukuza na kudumisha mchakato wa maendeleo fungamani! Akiwa nchini Korea, ametembelea eneo la kijeshi ambalo ni muhimu sana kwa historia na maendeleo ya Korea ya Kusini. Askofu mkuu Gallagher alikuwa ameandamana na viongozi wakuu wa Jeshi, kwani hili ni eneo ambalo si rahisi sana kutembelewa na watu wa kawaida!

Ameonesha matumaini yake kwa siku za usoni na kwamba, Vatican inapania kuendeleza na kudumisha uhusiano wake wa kidiplomasia na Korea ya Kusini, baada ya miaka 55. Lengo ni kuhakikisha kwamba, uchungu na fadhaa ya wananchi wa Korea ya Kusini, hasa zaidi maskini na wale wanaoteseka inakuwa ni furaha, matumaini, uchungu na fadhaa ya Kanisa la Kristo! Vatican inapenda kuheshimu na kuthamini utajiri wa tamaduni za wananchi wa Korea na kutaka nchi hii kwa sasa kujielekeza zaidi katika mchakato wa haki, amani na maridhiano.

Askofu mkuu Gallagher akizungumza na Wabunge Wakatoliki nchini Korea ya Kusini, amekazia umuhimu wa waamini kushiriki kikamilifu katika masuala ya kisiasa kama njia makini ya kuyatakatifuza malimwengu kwa tunu msingi za Kiinjili. Amewataka wanasiasa kujenga na kudumisha dhamiri nyofu, itakayowawezesha kupambanua mema na mabaya; kusimamia haki, ukweli, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wanasiasa wajikite zaidi katika kutafuta haki, ili kukuza amani na kusimamia ukweli!

Kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa, uongozi ni huduma kwa familia ya Mungu na wala si kichaka cha kujitafutia utajiri na mali. Kumbe, ni wajibu wa wanasiasa kusimama kidete kulinda, kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; kukuza na kudumisha amani duniani, utu, heshima, haki msingi za binadamu na maendeleo fungamani yanayomgusa mtu mzima: kiroho na kimwili. Diplomasia ya Vatican kwa ajili ya huduma ya haki na amani duniani ni kati ya mambo ambayo ameyakazia zaidi alipokutana na kuzungumza na Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki nchini Korea. Askofu mkuu Paul Richard Gallagher katika safari yake ya kikazi ana andamana na Askofu mkuu Afred Xuereb, Balozi wa Vatican nchini Korea pamoja na maafisa wa Ubalozi wa Vatican nchini Korea.

Ziara ya Askofu mkuu Paul Richard Gallagher nchini Korea ya Kusini
07 July 2018, 15:28