PERU-POPE-VISIT-INDIGENOUS PERU-POPE-VISIT-INDIGENOUS 

Utangazaji na ushuhuda wa imani ni kiini cha Habari Njema!

Kongamano la Kimisionari Amerika ya Kusini linakazia umuhimu wa kumwilisha imani katika maisha na utume wa Kanisa; mambo msingi yanayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa kama sehemu ya uinjilishaji mpya. Pia kuna umuhimu wa kumwangalia Kristo Yesu na kuwa wanyenyekevu kwa roho Mtakatifu, Mhimili wa uinjilishaji, maisha na utume wa Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini, kuanzia tarehe 9 -14 Julai 2018 linaadhimisha Kongamano VI la Kimisionari Amerika ya Kusini linaloongozwa na kauli mbiu “Furaha ya Injili, kiini cha utume wa kinabii, chemchemi ya upatanisho na umoja”. Katika maadhimisho haya, Baba Mtakatifu Francisko anawakilishwa na Kardinali Ferdinando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilsihaji wa watu. Lengo kuu la kongamano hili ni kuweza kujenga jamii inayosimikwa katika haki, udugu na mshikamano huko Amerika ya Kusini.

Waamini watambue kwamba, wao kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, wanashiriki: Unabii, Ukuhani na Ufalme wa Kristo, kumbe, wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa mataifa, lakini zaidi, kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili hata wao, waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, kielelezo cha imani tendaji. Familia ya Mungu Amerika ya Kusini, inapaswa kuwa ni shuhuda na chombo cha uinjilishaji mpya kwa kusoma alama za nyakati, ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo zinazomwandama mwanadamu! Huu ndio mwelekeo unaotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya uinjilishaji Amerika ya Kusini, hususan kwenye Ukanda wa Amazonia.

Baba Mtakatifu ameamua kwamba, Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia itakayoadhimishwa mwezi Oktoba, 2019 iongozwe na kauli mbiu “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia endelevu”. Uinjilishaji na Utamadunisho ni mchakato unaolitajirisha Kanisa na kwamba, Kanisa linataka kuwajengea watu uwezo wa kupambana na changamoto za maisha, ili siku moja Kanisa liweze kuwa na sura ya Amazonia inayofumbatwa na uwepo wa watu mahalia.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wataendelea kuimarisha mafungamano ya kijamii, kimaumbile na mang’amuzi ya imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Kanisa linapenda kukazia Injili ya upendo na mshikamano unaowashirikisha wananchi mahalia katika maamuzi na utekelezaji wa sera na mikakati yake kwa kuongozwa na mbinu mkakati wa kuona, kung’amua na kutenda kwa kukazia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine.

Askofu mkuu Giovanni Pietro Dal Toso, Katibu Mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu katika hotuba yake amekazia umuhimu wa kumwilisha mani katika maisha na utume wa Kanisa; mambo msingi ya imani yanayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa kama sehemu ya uinjilishaji mpya. Umuhimu wa kumwangalia Kristo Yesu na kuwa wanyenyekevu kwa Roho Mtakatifu, mhimili mkuu wa utangazaji wa Habari Njema.

Mbinu mkakati wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, limbuko lao walillala katika usingizi wa amani. Mwishoni, ni umuhimu wa kuendelea kuwatangazia watu wasiomjua Kristo furaha ya Injili katika maisha yao na kwamba, huu ni ujumbe unaopaswa kupelekwa kwa watu wote bila ubaguzi kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

 

Askofu mkuu Giovanni Pietro Dal Toso anasema, maadhimisho ya Kongamano la Kimisionari Amerika ya Kusini ni mchakato wa kutembea kwa pamoja, kwa kutambua kwamba, wameitwa na sasa wanatumwa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Hii ni changamoto ya kuunganisha imani inayomwilishwa katika matendo, kama sehemu muhimu sana ya utume wa Kanisa kwa watu wa Mataifa, ili hatimaye, familia ya Mungu Amerika ya Kusini katika ujumla wake, iweze kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani! Hii ndiyo maana kwamba, Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa yanaunga mkono jitihada zote hizi zinazofanyika kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya.

Kiini cha utume na maisha ya Kanisa yanapata chimbuko lake kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu na kwamba, waamini wanaitwa kuwa ni mashuhuda, vyombo na watangazaji wa kazi ya ukombozi iliyotekelezwa na Kristo Yesu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake kutoka kwa wafu. Utume na maisha ya kimisionari yanabubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu kwa kufumbatwa na huruma pamoja na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani. Kumbe, Wakristo wote wanapaswa kuwa ni wajumbe wa huduma na utume wa uinjilishaji.

Familia ya Mungu Amerika ya Kusini inahamasishwa kumwangalia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ili aweze kuwakomboa kutoka katika lindi la dhambi na mauti na hatimaye, kuwapatanisha na Baba yake wa milele. Huu ni mwaliko wa kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wake kwa waja wake! Waamini wamwangalie Kristo Yesu aliyetumwa na Baba wa milele, mmisionari wa kwanza, wakiwa na nyoyo wazi, ili waweze kumtafakari kwa kina na mapana na hatimaye, kumwachia nafasi ya kuweza kuzungumza nao kutoka katika undani mwa maisha yao!

Waamini wawe wanyenyekevu kwa Roho Mtakatifu anayekuja kuwainua na kuwasaidia katika unyonge na udhaifu wao. Anawawezesha kuwa na ari, moyo mkuu, ubunifu na uaminifu katika maisha na utume wa Kanisa, tayari kupyaishwa na Roho Mtakatifu. Jambo la msingi kwa waamini ni kujiaminisha kwa Roho Mtakatifu na kwamba, kiini cha ujumbe wa Habari Njema ya Wokovu ni kwamba, “Kristo Yesu, alitwaa mwili akakaa kwetu, akateswa, akafa na kufufuka kwa wafu na ameketi kuume kwa Baba kwa utukufu”. Hiki ndicho Kiini Fundisho cha Imani yaani “Kerygma”.

Mitume walianza kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu katika uhalisia wa maisha ya watu, lakini daima waliendelea kufanya rejea kwenye kiini fundisho cha imani! Watu wakasikiliza, wakaguswa, wakatubu na kumwongokea Mungu. Hii ndiyo changamoto inayopaswa kufanyiwa kazi hata na Wakristo wa nyakati hizi. Huu ni mwaliko wa kutoka na kuwaendea wale wote ambao hawajapata bahati ya kusikia Habari Njema ya Wokovu ikitangazwa maskinio mwao. Hii ni hija ya maisha yote, kwa kukua na kuendelea kugundua na kutambua uwepo wa Mungu katika maisha yao. Habari Njema ya Wokovu ni kwa ajili ya watu wote na wala si kwa ajili ya wateule wachache. Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu inayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa hadi miisho ya dunia.

Askofu mkuu Giovanni Pietro Dal Toso anahitimisha hotuba yake kwa kukazia umuhimu wa kumwilisha imani katika matendo kama kielelezo makini cha ushuhuda wenye mvuto, sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya. Wakristo watambue kwamba, wao ni wamisionari kwa ajili pamoja na Kanisa. Waendelee kujikita katika malezi na majiundo awali na endelevu ya katekesi; kwa kushiriki kikamilifu katika vyama vya kitume, Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo pamoja na kujiandaa kikamilifu katika maadhimisho ya Mwezi Maalum wa Kimisionari Oktoba 2019, Kanisa litakapokuwa linazindua tena upya ari na mwamko wa kimisionari.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mwezi Oktoba 2019 kitakuwa ni kipindi maalum sana kwa maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Utakuwa ni muda wa kusali na kutafakari utume kama msingi wa mchakato mzima wa uinjilishaji mpya unaotekelezwa na Mama Kanisa. Kwa hakika hiki ni kipindi cha ushuhuda wa  huruma ya Mungu inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu!  

Mwezi Oktoba 2019 Kanisa litakuwa linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Benedikto XV alipochapisha Waraka wa Kitume"Maximum Illud" yaani “Kuhusu Shughuli za Kimisionari.” Ni muda wa: sala, katakesi, tafakari na matendo ya huruma! Ni wakati muafaka kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanatelekeza vyema dhamana na wajibu waliojitwaliwa kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo inayowashirikisha: Unabii, Ukuhani na Ufalme wa Kristo. Waamini wakiwa wamezaliwa kwa “Maji na Roho Mtakatifu”, wanawajibu wa kukiri na kutangaza imani ambayo wameipokea kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kanisa na hivyo kushiriki katika utendaji wa kitume na wa kimisionari wa Taifa la Mungu.

 

12 July 2018, 15:46