Tafuta

Vatican News
Kazi za suluba kwa watoto wadogo Kazi za suluba kwa watoto wadogo  (AFP or licensors)

Siku ya Kupambana na biashara ya binadamu 2018

Makundi ya kigaidi na magenge ya uhalifu wa kimataifa yanatumia njia za wakimbizi na wahamiaji kujipatia fedha haramu. Jumuiya ya Kimataifa, tarehe 30 Julai 2018 inaadhimisha Siku ya Kupambana na Biashara ya Binadamu Duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kutokana na kukosena kwa fursa halali za uhamiaji, Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema, watu wengi wanajikuta wakihatarisha maisha yao kwa kujitumbukiza hata katika mitego haramu inayohatarisha maisha, utu na heshima yao kama binadamu. Matokeo yake ni wahamiaji na wakimbizi kutumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Makundi ya kigaidi na magenge ya uhalifu wa kimataifa yanatumia njia za wakimbizi na wahamiaji kujipatia fedha haramu. Jumuiya ya Kimataifa, tarehe 30 Julai 2018 inaadhimisha Siku ya Kupambana na Biashara Binadamu Duniani.

Baba Mtakatifu anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuunganisha nguvu zao, ili kupambana na biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo; kwa kuwalinda na kuwasaidia kwa dhati waathirika. Baba Mtakatifu anamwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwaongoa wafanyabiashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo, na awajalie waathirika matumaini ya kuweza kujipatia tena uhuru, wale wote wanaoteseka kutokana na kashfa hii katika ulimwengu mamboleo.

Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu, linawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kushiriki kikamilifu katika kampeni dhidi ya biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Hii ni kampeni ambayo itaendelezwa na kudumishwa mwezi wote wa Agosti, 2018. Takwimu zinaonesha kwamba, hii ni biashara inayozalisha zaidi ya bilioni 150 kwa mwaka kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Biashara hii ni janga na donda ndugu kwa utu na heshima ya binadamu, inapaswa kufikia ukomo, kwa kutambua kwamba, mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kamwe mwili wake si bidhaa ya kuuzwa au kununuliwa sokoni.

Biashara haramu ya binadamu ni jambo linaloendelea kukua na kuongezeka siku kwa siku, huku wahusika wakijitahidi kutafuta mbinu mbadala za kuweza kufanikisha malengo yao machafu ili wasikumbwe na mkondo wa sheria.  Kumbe, kuna haja ya kusimama kidete ili kulinda na kutetea haki, utu na heshima ya binadamu sanjari na kushiriki kikamilifu katika kampeni maalum zinazoendelea kutoa ulinzi na usalama kwa ajili ya watoto ili wasitumbukizwe katika utalii wa ngono, kazi za suluba na ndoa za shuruti.

Ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia umeiwezesha Jumuiya ya Kimataifa kuwa na mwingiliano mkubwa kiasi kwamba, leo hii Dunia ni kama ulimwengukijiji. Watu waelimishwe kuhusu: utu na heshima yao kama binadamu; haki zao msingi na wapi wanapoweza kupata msaada wa dharura pale wanapojikuta kwamba, wametumbukizwa kwenye biashara haramu ya binadamu na mifumo ya utumwa mamboleo. Takwimu zinaonesha kwamba, idadi ya watoto na vijana wanaoendelea kutumbukizwa kwenye biashara ya binadamu na utumwa mamboleo inaongezeka maradufu na kwamba, kwa sasa wamefikia kiasi cha milioni 40, wengi wao wakiwa ni wasichana na wanawake. Kati ya mwaka 2012 hadi mwaka 2016 watoto waliokuwa wametumbukizwa kwenye mifumo ya utumwa mamboleo walikuwa ni milioni 152.

Takwimu za “Global Slavary Index” zinaonesha kwamba, Korea ya Kaskazini na Eritrea ni kati ya nchi zinazoongoza duniani kwa utumwa mamboleo. Burundi inashika nafasi ya tatu kutokana na kazi za suluba, mauaji na watu kuendelea kupotea katika mazingira ya kutatanisha. Katika orodha hii, zimo pia nchi kama Pakistani, Afghanistan, Sudan ya Kusini na Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati. Kiwango hiki ni kikubwa kwenye Nchi za Amerika ya Kusini ambako wasichana na wanawake wanatumbukizwa kwa urahisi sana katika biashara ya ngono kutokana na ugumu wa maisha.

Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kwa kushirikiana na wadau mbali mbali kuwajengea uwezo wanawake katika masuala ya elimu, uchumi, sheria, imani na utu wema, ili kuweza kupambana na changamoto, fursa na kinzani zinazojitokeza katika mapito yao ya maisha.  Wanawake na wasichana wajenge utamaduni wa kukataa katu katu kutumiwa na baadhi ya wajanja wachache kwa ajili ya masilahi yao binafsi. Wakumbuke kwamba, Mwenyezi Mungu amemuumba mwanadamu kwa uhuru, utashi na mapendo kamili, akamshirikisha katika mpango wa kazi ya uumbaji; yote haya yafanyike kwa sifa na utukufu wa Mungu na kwa ajili ya utakatifu wa maisha ya mwanadamu, kwani huu ni wito wa kila mwamini na kamwe asiwepo mtu anayetumbukizwa katika biashara ya binadamu!

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

30 July 2018, 11:20