Cerca

Vatican News
Hivi karibuni  Askofu mkuu Vincenzo Zani ametembelea Rwanda kikazi. Hivi karibuni Askofu mkuu Vincenzo Zani ametembelea Rwanda kikazi. 

Shule za Kanisa Katoliki; Kipaumbele: Ushirikishwaji, Majadiliano na mshikamano

Askofu mkuu Vincenzo Zani anasema dhana ya haki, amani na upatanisho ni sehemu muhimu sana ya malezi ili kuwafunda vijana dhamana na wajibu wao kwa sasa na kwa siku za usoni. Ikiwa kama elimu katoliki itajikita na kufumbatwa katika: ushirikishaji, majadiliano na mshikamano, familia ya Mungu itakuwa na uhakika wa kuwapata raia wema na wachamungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Upatanisho, haki na amani ni ni sera na mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji kwa Kanisa Barani Afrika. Hii ni njia makini ya kupambana na changamoto changamani kwa kujikita zaidi katika  mchakato wa kuwa na uhakika wa usalama wa chakula; maji safi na salama, nishati rafiki kwa mazingira; huduma bora ya afya na elimu makini;  misingi bora ya kifamilia na uwiano mzuri wa biashara ya kimataifa. Lengo ni kuipatia familia ya Mungu Barani Afrika, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Vipaumbele vya shughuli za kichungaji Barani Afrika vinagusia hasa: umuhimu wa utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu, Uinjilishaji kama sehemu ya utamadunisho; majadiliano, haki na amani pamoja na mawasiliano; yote haya yanapania kujenga Familia ya Mungu Barani Afrika.Tangu wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Kwanza ya Maaskofu Barani Afrika kumekuwepo na mabadiliko na kwa hakika, cheche za matumaini zinaanza kuonekana licha ya vita, kinzani na migogoro inayoendelea kujionesha katika baadhi ya Nchi Barani Afrika.

Kanisa linapaswa kuendeleza mchakato wa kudumisha haki, amani na upatanisho, kwa kukazia upendo na msamaha. Ili Kanisa Barani Afrika, liweze kutekeleza utume wake kama shuhuda na chombo cha Kristo, familia ya watu wa Mungu, inapaswa kuchuchumilia upatanisho, haki na amani, kama karama za Pentekoste Mpya Barani Afrika, msisitizo ni umoja kati ya Mungu na umoja unaojionesha kati ya watu.

Ili vijana waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho Barani Afrika, kuna haja ya kuwekeza zaidi katika sekta ya elimu makini itakayowawezesha vijana kupambana na hali pamoja na mazingira yao, ili kujenga Afrika yenye matumaini zaidi pamoja na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati, unaowawezesha watu kuthaminiana, kupendana na kuheshimiana kama ndugu wamoja, licha ya tofauti zao msingi.

Hii ni changamoto iliyotolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Vincenzo Zani, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki, wakati alipokuwa anashiriki mkutano wa kimataifa uliokuwa umeandaliwa na Chuo Kikuu cha Kikatoliki Rwanda kwa kushirikiana na Kitivo cha tafiti za kidini na elimu cha Lovanio, kilichoko nchini Ubelgiji. Akiwa nchini Rwanda kwa muda wa siku tano, Askofu mkuu Zani alikuwa ana andamana na Askofu mkuu Andrzej Jozwowicz, Balozi wa Vatican nchini Rwanda pamoja na Askofu Philippe Rukamba wa Jimbo Katoliki Butare.

Askofu mkuu Zani amepata nafasi ya kuteta na wanafunzi waliosoma kwenye shule zinazoendeshwa na kumilikiwa na Kanisa Katoliki nchini Rwanda. Kauli mbiu iliyoongoza mkutano huu, ilikuwa “Sisi ni chachu ya upatanisho wa watu wa Mungu”. Kanisa Katoliki duniani, linamiliki na kuendesha shule, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu 217, 000, vikiwa na wanafunzi zaidi ya milioni 62 wanaohudhuria katika shule za msingi na milioni 11 wako katika shule za sekondari, kiasi cha kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu, sehemu mbali mbali za dunia. Taasisi na vyuo vikuu vinakabiliwa na changamoto kubwa katika sekta ya elimu. Hizi ni changamoto zinazojikita katika uwezo wa kiuchumi, taaluma na hali za kijamii. Ili kuwajengea vijana matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi, Kanisa na jamii katika ujumla wake, havina budi kushikamana na kusaidiana katika mchakato wa maboresho ya sekta ya elimu, ili kujibu kilio na mahitaji halali ya  vijana wa kizazi kipya.

Askofu mkuu Zani amekaza kusema, changamoto zote hizi hazina budi kukabiliwa kwa njia ya mwanga wa Injili, kanuni maadili na utu wema, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na mahitaji yake msingi. Kwa kuheshimu na kuthamini utu, heshima na haki zake msingi; kwa kuendelea kujikita zaidi na zaidi katika uhuru, upendo na mshikamano wa dhati. Tunu hizi ni muhimu sana kwa maisha na utume wa familia ya Mungu nchini Rwanda ambayo kunako mwaka 1994 ilijikuta ikitumbukia katika mauaji ya kimbari. Kumbe, Kanisa kwa kuwekeza zaidi na zaidi katika sekta ya elimu, linataka kusaidia mchakato wa haki, amani na upatanisho, changamoto iliyotolewa na Mababa wa Awamu ya Kwanza ya Sinodi ya Afrika.

Taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu vinavyosimamiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki, hazina budi kujikita katika mchakato wa kutoa elimu ya haki, amani na upatanisho wa kweli. Huu ndio mwelekeo sahihi wa elimu inayotolewa na Kanisa. Mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu anapaswa kuheshimiwa na wote, huyu ndiye kiini cha kazi nzima ya uumbaji na ukombozi. Kumbe, wanafunzi hawana budi kufundwa vyema: kiroho, kimwili, kiakili; kijamii na kitamaduni, ili hatimaye, kuwa na jamii inayojikita katika haki, amani, udugu na mshikamano. Vijana waliofundwa na kuiva barabara katika nyanja mbali mbali za maisha wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa haki, amani na upatanisho. Vijana wajifunze kuwa waaminifu, wakweli na wawazi, ili kusaidia kuandika ukurasa wa historia na tamaduni za watu husika.

Askofu mkuu Vincenzo Zani anakaza kusema, dhana ya haki, amani na upatanisho ni sehemu muhimu sana ya malezi ili kuwafunda vijana wa kizazi kipya dhamana na wajibu wao kwa sasa na kwa siku za usoni. Ikiwa kama elimu katoliki itajikita na kufumbatwa katika: ushirikishaji, majadiliano na mshikamano, familia ya Mungu itakuwa na uhakika wa kuwapata raia wema na wachamungu, watakaoweza kuvuka mipaka ya ukabila, udini na umajimbo usiokuwa na mvuto wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu na badala yake, jamii itakuwa na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho wa kitaifa ndani na nje ya Rwanda.

Askofu mkuu Zani wakati wa ziara yake ya kikazi nchini Rwanda amekazia kwa namna ya pekee kabisa mchakato wa ujenzi wa elimu ya uraia; majadiliano katika ukweli na uwazi; elimu inayomfunda mtu mzima: kiroho na kimwili kwa kutambua uwepo wa Mungu na upendo kwa jirani. Katekesi makini, iwe ni chombo cha kuwafunda watu: kiroho na kimwili. Elimu ya dini shuleni, ipewe msukumo wa pekee na Kanisa Barani Afrika, vinginevyo watoto na vijana watakosa dira na mwelekeo sahihi katika maisha na kuanza kutangatanga kama “daladala zilizokatika usukani”.

Askofu mkuu Vincenzo Zani amepata pia nafasi ya kukutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Rwanda, majalimu na walimu ili kujenga mtandao wa mshikamano katika sekta ya elimu Barani Afrika, jambo ambalo linatiliwa mkazo pia na Baba Mtakatifu Francisko.

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

28 July 2018, 15:50