Tafuta

Vatican News
VATICAN-RELIGION-ANGELUS-POPE VATICAN-RELIGION-ANGELUS-POPE  (AFP or licensors)

Papa Francisko asema kiini na utume wa Kanisa ni Kristo Yesu!

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, asema, Kristo Yesu ni kiini na sura ya utume wa Kanisa unaopaswa kumwilishwa katika hali ya unyenyekevu kwa kutambua kwamba, wakati mwingine, Mwenyezi Mungu katika utashi wake, anatumia vyombo dhaifu ili kufikishia ujumbe unaokusudia kwa watu wake! Wakristo wanashiriki: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican

Injili ya Jumapili ya XV ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa inamwonesha Yesu akiwatuma mitume wake kumi na wawili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kati ya watu wa Mataifa. Hawa ni wale ambao aliwaita kwa majina, ili waweze kukaa pamoja naye, kusikiliza na kuona matendo makuu ya Mungu kwa njia ya miujiza iliyotendwa na Kristo Yesu mwenyewe! Yesu akaamua kuwatuma wawili wawili ili kwenda katika miji na vijiji ambavyo angepitia mwenyewe. Haya ni mafunzo kazini ambayo Yesu aliamua kuwapatia wafuasi wake, dhamana na utume ambao wangeuendeleza baada ya Ufufuko wake, kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 15 Julai 2018 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana. Baba Mtakatifu anakaza kusema, mtindo wa maisha ya kimisionari una kiini na sura yake, mambo makuu mawili ambayo ni sawa ni chanda na pete! Kristo Yesu ni kiini cha mtume mmisionari, ambaye anatambua kwamba, ameitwa, akapewa madaraka na hatimaye kutumwa na Kristo Yesu kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! Kumbe, Kristo Yesu ni kiini cha mitume wamisionari ambao wanapaswa kumtangaza na kumshuhudia Kristo kwani wao ni wajumbe wake!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, sehemu hii ya Injili inawagusa hata Wakristo wa nyakati hizi, wanaoitwa kutangaza na kumshuhudia Kristo Yesu katika medani mbali mbali za maisha na kwamba, Kristo Yesu ndiye kiini cha Habari Njema ya Wokovu. Hii ni dhamana na utume wa Kanisa unaofumbatwa katika maisha ya Kristo Yesu. Wakristo wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo, dhamana na utume ambao wamejitwalia kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, unaowashirikisha: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, mtindo wa maisha ya kimisionari una sura na unatumia wakati mwingine vyombo dhaifu kinyume kabisa cha matarajio na matamanio ya kibinadamu. Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu anawataka wafuasi wake wawe wepesi kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini bila kuelemewa na mizigo isiyokuwa ya lazima. Anawataka wawe ni mahujaji wanaobeba fimbo ya kuwaongoza pamoja na kujifunga viatu miguuni! Hizi ni alama za mahujaji wanaojitosa kimasomaso kujenga Ufalme wa Mungu! Wanakumbushwa kwamba, wao si watawala wala mameneja, bali wajumbe wa Habari Njema ya Wokovu.

Baba Mtakatifu amewatolea mfano wa watakatifu kutoka Jimbo kuu la Roma waliojisadaka bila ya kujibakiza katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Hawa si wengine bali ni akina Mtakatifu Filipo Neri, Mtakatifu Benedikto Giuseppe Labre, Mtakatifu Alessio, Mtakatifu Ludovica Albertini, Mtakatifu Francesca Romana bila kumsahau Mtakatifu Gaspari del Bufalo, muasisi wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu ambaye kwa njia ya mahubiri, majitoleo na mfano bora wa maisha, aliweza kuwaongoa watu wengi waliokuwa wamekengeuka kutokana na utepetevu wa imani kwa nyakati hizi. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hawa walikuwa ni wamisionari wanyenyekevu, wenye bidii, juhudi na maarifa na wala hawakujitambulisha kama wafanyakazi wa mshahara, wala wafanyabiashara, bali watumishi waaminifu katika shamba la Bwana.

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, sura ya utume inategemea pia na jinsi ambavyo Habari Njema ya Wokovu inavyoweza kupokelewa na kukubalika, kielelezo cha umaskini hali inayogusa mang’amuzi ya kushindwa kutekeleza utume huu. Hii ndiyo hali iliyomkumba hata Kristo Yesu katika maisha na utume wake, watu wakashindwa kumpokea kutokana na unyenyekevu wake uliofumbatwa katika Kashfa ya Fumbo la Umwilisho! Baada ya kukataliwa, baadaye Kristo Yesu aliteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Mateso na hali ya kukataliwa ni mambo yanayoweza kuwakumba hata wamisionari na watangazaji wa Habari Njema ya Wokovu kwa nyakati hizi! Waswahili husema, Popo kamwe hawezi kudondosha manyoya yake! Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, iwe ni nguvu na ujasiri kwa wamisionati mitume kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kati ya watu wa Mataifa kwa ari na moyo mkuu. Mwishoni, mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika  waamini kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mtume na Mmisionari wa Neno wa Mungu, ili awasaidie kutangaza na kushuhudia Injili katika hali ya unyenyekevu na angavu, licha ya kukataliwa, kutoeleweka au kwa kukumbana na mateso, dhuluma na nyanyaso mbali mbali!

Sikiliza

 

15 July 2018, 16:45