Vatican News
Kanisa nchini Nicaragua kuendesha mapambano ya kudai, haki, amani na maridhiano kwa njia ya sala. Kanisa nchini Nicaragua kuendesha mapambano ya kudai, haki, amani na maridhiano kwa njia ya sala.  (ANSA)

Kanisa nchini Nicaragua kuendesha mapambano kwa njia ya sala!

Maaskofu Nicaragua bado wanayo nia na utashi thabiti wa kutaka kuendeleza mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu nchini humo. Kanisa linaendelea kujenga na kudumisha mshikamano wa upendo na sala; jambo linalounga mkono pia na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Amerika ya Kusini, CELAM.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Kanisa nchini Nicaragua linaendelea kunyanyaswa na kudhulumiwa, lakini Baraza la Maaskofu Katoliki Nicaragua linasema, pamoja na mambo yote haya, lakini Maaskofu bado wanayo ni ana utashi thabiti wa kutaka kuendeleza mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu nchini humo. Kanisa linaendelea kujenga na kudumisha mshikamano wa upendo na sala; jambo linalounga mkono pia na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Amerika ya Kusini, CELAM.

Hali ya kiuchumi, kisiasa na kijamii inaendelea kuwa tete kila kukicha. Dhamana na utume wa Kanisa wanasema Maaskofu Katoliki Nicaragua ni kwa Kanisa kuendelea kuwa chombo na shuhuda wa haki, amani na upatanisho hata kama Rais Daniel Ortega amefutilia mbali mchakato wa majadiliano na kwamba, kwa sasa ameamua kuwashughulikia wananchi wake kama “Mbwa koko” pamoja na kulishutumu Kanisa kwamba, limebuni mbinu mkakati wa kutaka kupindua serikali yake. Ili kudhihirisha hili, Serikali imeendelea kushambulia viongozi wa Kanisa pamoja na miundo mbinu ya Kanisa.

Serikali inadai kwamba, huko kulikuwa kumefichwa silaha za kutaka kuipindua serikali iliyoko halali madarakani. Hata katika mazingira kama haya, Kanisa bado linaendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano kwa kuitaka Serikali kutumia vyema vikosi vya ulinzi na usalama kwa ajili ya kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na utulivu badala ya kugeuka kuwa ni vikosi vya mauaji ya watu wasiokuwa na hatia! Viongozi wa vyama vya upinzani wanashutumiwa kwa kuongoza vitendo vya kigaidi na kwamba, adhabu yake ambayo imepitishwa hivi karibuni ni kifungo cha miaka kati ya 15 – 20. Wapinzani wanasema, hii ni sheria kandamizi inayokwenda kinyume cha haki msingi za binadamu, utu na heshima yake!

Wakati huo, Kardinali Mauro Piacenza, Mhudumu mkuu wa Idara ya Toba ya Kitume na Rais wa Shirika la Kipapa Kuhudumia Makanisa Hitaji, anasema, baada ya kuzungumza kwa faragha na viongozi wa Kanisa nchini Nicaragua, wamefikia uamuzi kwamba, waendeleze mapambano ya kutaka, haki, amani na maridhiano ya kitaifa kwa njia ya sala. Kardinali Piacenza anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya sala.

Anawaalika waamini kutolea nia zao, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa umoja na mshikamano katika mambo matakatifu, ili kuwaenzi na kuwasaidia viongozi wa Kanisa ambao wananyanyasika sana. Juhudi hizi zinaungwa mkono pia na Kardinali Leopoldo Josè Brenes Solorzano, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Managua, nchini Nicaragua. Shirika la Kipapa la Kuhudumia Makanisa hitaji litaendelea kutoa taarifa za mara kwa mara juu ya machafuko ya kisiasa nchini Nicaragua, ili kuamsha ari na moyo wa sala kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwaonea huruma na upendo na hatimaye kukomesha dhuluma na nyanyaso hizi. Itakumbukwa kwamba, sala ni chakula cha maisha na utume wa Kanisa, hiki ndicho chakula cha kwanza kabisa kinachotolewa na Mama Kanisa kwa ajili ya watoto wake na baadaye, kupiga hatua kubwa zaidi kwa kuhakikisha kwamba, watu wanapata mahitaji yao msingi.

Nicaragua

 

26 July 2018, 15:08