Tafuta

 Kardinali Theodore McCarrick ameng'atuka kutoka Baraza la Makardinali Kardinali Theodore McCarrick ameng'atuka kutoka Baraza la Makardinali 

Kardinali Theodore McCarrick ang'atuka kutoka Baraza la Makardinali

Kutokana na kung’atuka kwa Kardinali Theodore McCarrick kutoka katika Baraza la Makardinali na uamuzi huo kuridhiwa na Baba Mtakatifu, hadi kufikia tarehe 28 Julai 2018 kuna jumla ya Makardinali 224 kati yao 124 wana haki ya kupiga na kupigiwa kura na wengine 100 kwa sasa hawana tena haki ya kupiga wala kupigiwa kura!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara nyingi amegusia sana kuhusu nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo zinazofanywa kwenye familia, shule, jumuiya na taasisi ambazo zimepewa dhamana ya kuwalinda! Anasema hii kashfa isiyovumilika kabisa na kwamba, Kanisa litaendelea kuwashughulikia wale wote watakaotiwa hatiani kujihusisha na nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo.

Kutokana na shutuma za nyanyaso zinazomkabili Kardinali Theodore McCarrick, Askofu mkuu Mstaafu wa Jimbo kuu la Washington DC. Nchini Marekani, ameamua kuwasilisha barua ya kung’atuka kutoka katika Baraza la Makardinali na kutojihusisha na shughuli yoyote ya maisha na utume wa Kanisa hadharani pamoja na kukaa katika nyumba atakayopangiwa kwa ajili ya toba na wongofu wa ndani, sala na tafakari, hadi hapo shutuma za nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo zitakapofikia hatima yake kadiri ya sheria za Kanisa. Kutokana na kung’atuka kwa Kardinali Theodore McCarrick kutoka katika Baraza la Makardinali, hadi kufikia tarehe 28 Julai 2018 kuna jumla ya Makardinali 224 kati yao 124 wana haki ya kupiga na kupigiwa kura na wengine 100 kwa sasa hawana tena haki ya kupiga wala kupigiwa kura!

Hivi karibuni Kardinali Seàn Patrick O’Malley, Mwenyekiti wa Tume ya Kipapa ya Kulinda Watoto Wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia, PCPM, iliyoundwa mwezi Machi 2014 na Baba Mtakatifu Francisko alisikika akisema, nyanyaso za kijinsia ni vitendo ambavyo kamwe haviwezi kukubalika kimaadili na ikiwa kama vitendo hivi vinafanywa na watu wenye dhamana katika uongozi wa Kanisa. Ni vitendo vinavyokera na kuudhi sana, kwani vinakwenda kinyume kabisa cha dhamana na wajibu wao wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Kashfa kama hizi zinapotokea ndani ya Kanisa, haitoshi tu kwa wahusika kuomba radhi, bali Kanisa kuchukua hatua za kinidhamu mara moja, ili kuhakikisha kwamba, kashfa za namna hii hazijirudii tena ndani ya Kanisa.

Shutuma za nyanyaso za kijinsia zinazowakabili viongozi wa ngazi za juu wa Kanisa nchini Marekani zinaonekana kuwa na uzito na kwamba, zimesababisha kuchafuka tena kwa hali ya amani na utulivu miongoni mwa familia ya Mungu ndani na nje ya Marekani. Kardinali O’Malley anasema, kila mara kunapoibuka shutuma kama hizi, Kanisa linapaswa kuwa makini zaidi kutambua kwamba, hapa kuna mapambano makubwa dhidi ya kumong’onyoka kwa maadili na utu wema.

Katika mazingira kama haya, Kanisa linapaswa kuendelea kujizatiti zaidi katika kutekeleza sera na mbinu mkakati ambayo imetungwa hivi karibuni ili kuweza kukabiliana na kashfa za nyanyaso ndani ya Kanisa kwa kuunda mazingira ya ulinzi na usalama kwa malezi na makuzi ya watoto wanaokuwa katika mazingira ya Kanisa. Ukweli na uwazi katika kesi hizi ni muhimu sana katika kuhakikisha kwamba, haki inatendeka kwa wale wote wanaohusika. Kanisa liendelee kutoa umuhimu wa pekee katika kushughulikia kesi hizi, kwani wakati mwingine ni matokeo ya matumizi mabaya ya madaraka ndani ya Kanisa.

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

28 July 2018, 16:24