Tafuta

Vatican News
19th Plenary AMECEA Assembly Ethiopia 19th Plenary AMECEA Assembly Ethiopia 

Papa Francisko aitaka AMECEA kujikita katika umoja, udugu, mshikamano, wema, ukweli na haki

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin na kusomwa na Askofu mkuu Luigi Bianco, Balozi wa Vatican nchini Ethiopia kwa Mababa wa AMECEA amewataka kujikita katika ujenzi wa mshikamano, umoja, udugu, wema, ukweli na haki kama chachu ya ujenzi wa jamii inayosimikwa katika amani na maendeleo ya kweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, kuanzia tarehe 13 - 23 Julai 2018 linaadhimisha mkutano wake wa 19 unaoongozwa na kauli mbiu “Tofauti mtetemo, Hadhi sawa, Umoja wa Amani ndani ya Mungu kwenye kanda ya AMECEA”. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican na kusomwa wakati wa Ibada ya Misa ya ufunguzi wa Mkutano mkuu wa AMECEA, huko Addis Ababa, Ethiopia, Jumapili, 15 Julai 2018 na Askofu mkuu Luigi Bianco, Balozi wa Vatican nchini Ethiopia, amekazia umuhimu wa kujikita katika mshikamano, umoja, udugu pamoja na kuendeleza kiu ya kutafuta mambo mema, ukweli na haki. Haya ni mambo msingi ambayo yanapaswa kuvaliwa njuga, kuvumbuliwa na hatimaye, kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu wa Ukanda wa AMECEA.

Baba Mtakatifu amewatumia salam na matashi mema Mababa wa AMECEA, katika mkutano wao unaojadili na kupembua maisha na utume wa Kanisa la Kristo Afrika Mashariki na Kati, ili hatimaye, waweze kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa ari, moyo mkuu pamoja na kujiamini. Amewataka waendelee kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Mitume wa Yesu kwa kujenga na kuimarisha mshikamano, udugu, wema, ukweli na haki katika Ukanda wa AMECEA.

Askofu mkuu Bianco amesema, Maaskofu ambao wameteuliwa kati ya watu kwa ajili ya Mungu na mambo matakatifu, wanapaswa daima kuendelea kupyaisha maisha na utume wao kwa kuondokana na kutenda kazi kwa mazoea! Maaskofu wanaitwa na kutumwa kwenda kuganga na kuwaponywa watu wa Mungu waliojeruhiwa sana kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini; kwa kuwapatia maana halisi ya maisha na kujibu maswali msingi katika maisha yao. Baba Mtakatifu kwa njia ya maisha na utume wake, analihamasisha Kanisa kuanza mchakato wa uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda, ari na mwamko wa furaha ya Injili, kielelezo makini cha watu waliokutana na Kristo Yesu katika maisha yao! Baba Mtakatifu ameukabidhi mkutano wa 19 wa AMECEA chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa. Mwishoni, ametoa baraka zake za kitume.

Sikiliza

 

 

15 July 2018, 17:02