Tafuta

Vatican News
ETIOPIA Assemblea Plenaria di AMECEA ETIOPIA Assemblea Plenaria di AMECEA 

Baraza la Kipapa la Mawasiliano kuendelea kushirikiana na AMECEA

Dr. Paolo Rufini Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika ujumbe aliowaandikia Mababa wa AMECEA katika mkutano wao mkuu wa 19 anasema, Vatican itaendelea kushirikiana na kushikamana na Nchi za AMECEA katika tasnia ya mawasiliano ya jamii, ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa njia za mawasiliano ya kisasa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, linaadhimisha mkutano wake mkuu wa 19 huko Addis Ababa, Ethiopia, kuanzia tarehe 13 – 23 Julai, 2018, wakiongozwa na mada: Tofauti mtetemo, Hadhi sawa, Umoja wa Amani ndani ya Mungu kwenye kanda ya AMECEA. Maaskofu wa AMECEA wamechagua tema hii kuongoza mkutano wao mkuu wa 19, ili kusisitiza ukweli kwamba, katika tofauti za tamaduni, mila na desturi za kabila au watu mbalimbali, kuna uzuri wenye thamani kubwa unaopaswa kuenziwa, kuheshimiwa na kushirikishana; na wala isiwe chanzo cha kinzani, migogoro na mipasuko. Familia ya Mungu katika Ukanda wa AMECEA ijenge na kudumisha umoja katika utofauti kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko.

Dr. Paolo Rufini, Mwenyekiti mpya wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano aliyetueliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu, amewatumia ujumbe Mababa wa AMECEA, akikazia kwamba, Baraza la Kipapa la Mawasiliano litaendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na vituo vya mawasiliano ya jamii vilivyoko katika nchi za AMECEA ili kuwatangazia watu Habari Njema ya Wokovu. Dr. Paolo Rufini  katika ujumbe aliomwandikia Kardinali Berhaneyesus Demerew Souraphiel Mwenyekiti wa AMECEA anasema, Mababa wa Sinodi ya kwanza ya Maaskofu wa Afrika kunako mwaka 1994 waliwekeza sana katika kuanzisha Vituo vya Radio vya Majimbo.

Radio hizi zimeendelea kuwa ni sauti ya kinabii na zimetoa mchango mkubwa sana kwa Kanisa. Kwa njia ya ushirikiano na Radio Vatican, Radio hizi zimewezesha hata sauti ya Khalifa wa Mtakatifu Petro kuweza “kutia timu” katika familia ya watu wa Mungu, Ukanda wa AMECEA. Baraza la Kipapa la Mawasiliano, linawashukuru na kuwapongeza Mababa wa AMECEA kwa ujasiri na mwono wao wa mbali. Mtakatifu Yohane Paulo II katika Wosia wake wa kitume “Ecclesia in Africa” yaani “Kanisa Barani Afrika”, anakazia umuhimu wa kuinjilisha vyombo vya mawasiliano ya jamii pamoja na kuhakikisha kwamba, Kanisa linatumia kikamilifu maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ili kufikisha ujumbe wa Habari Njema kwa familia ya Mungu Barani Afrika, kwa kutambua kwamba, leo hii mawasiliano yameugeuza ulimwengu kuwa kama kijiji. Watumiaji wa vyombo vya mawasiliano ya jamii, waelimishwe zaidi, ili waweze kufaidika zaidi na zaidi na ujumbe unaotolewa na tasnia ya mawasiliano ya jamii ili kujenga, umoja, upendo na mshikamano wa dhati!

Dr. Paolo Rufini anakumbusha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko amefanya mageuzi makubwa katika vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican na sasa matunda yake yanaanza kuonekana, kwa njia ya ushirikiano, mshikamano na mafungamano ambayo yamesaidia sana kuboresha tija na weledi katika vyombo vya mawasiliano vya Vatican, ingawa bado kila chombo kina uhuru wake. Radio Vatican ambayo kwa miaka mingi imekuwa ni mdau wa sekta ya mawasiliano katika Nchi za AMECEA kwa sasa ni sehemu ya Baraza la Kipapa la Mawasiliano na sasa inarusha matangazo yake kwa mtindo wa kidigitali, ukweli wa mambo ambao Vatican imeamua kuuvalia njuga.

Baba Mtakatifu Francisko kunako tarehe 4 Mei 2017 aliwaambia wajumbe wa Sekretarieti ya Mawasiliano ya Vatican ambayo kwa sasa imegeuzwa na kuwa ni Baraza la Kipapa la Mawasiliano kwamba, kulikuwa kuna haja ya kuanza kujikita katika utamaduni wa kidigitali, ili kuviwezesha vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican kuendelea kuwa ni jukwaa la kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia.

Lakini hata katika maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia kuelekea katika utamaduni wa kidigitali, Baba Mtakatifu Francisko alivitaka vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican kuhakikisha kwamba, vinatoa kipaumbele cha pekee kwa Bara la Afrika katika sera na mikakati yake ya mawasiliano. Kutokana na changamoto hii, Vatican Media, inaendelea kurusha matangazo yake katika Masafa Mafupi kama ilivyokuwa tangu awali, kwa zile nchi ambazo bado zinahitaji huduma hii.

Dr. Paolo Rufini anakaza kusema, nchi za AMECEA bado zinaweza kuwa na matumaini ya kuendelea kupata ushirikiano wa dhati kutoka katika Baraza la Kipapa la Mawasiliano, hasa kwa kuhakikisha kwamba, Siku za Upashanaji habari Duniani zinafanikiwa zaidi, kwani hii ni siku ambayo Khalifa wa Mtakatifu Petro anatoa ujumbe maalum kwa ajili ya tasnia ya mawasiliano ya jamii kama sehemu ya utekelezaji wa changamoto iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Vatican Media inapania pamoja na mambo mengine, kuhakikisha kwamba, mafundisho, ujumbe na cheche za Habari Njema ya Wokovu zinawafikia watu wengi zaidi, ili kuliwezesha Kanisa Barani Afrika, kucharuka katika maendeleo fungamani ya binadamu; kwa kuzingatia mafanikio, matatizo na changamoto zinazoendelea kujitokeza.

Mwishoni, Dr. Paolo Rufini anapenda kuzipongeza Ethiopia na Eritrea ambazo kwa siku za hivi karibuni zimeanza mchakato wa haki, amani na upatanisho ili kuambata Injili ya amani, tukio ambalo lilipongezwa sana na Baba Mtakatifu Francisko kwamba, ni alama ya matumaini ya amani kwa nchi zilizoko Pwani ya Pembe ya Afrika, lakini pia kwa familia ya Mungu Barani Afrika katika ujumla wake. Anapenda kuwakaribisha wanapobahatika kutembelea Roma na kwamba, Baraza la Kipapa la Mawasiliano litaendelea kushirikiana na kushikamana na AMECEA katika tasnia ya mawasiliano ili pande zote mbili ziweze kukua na kuimarika zaidi!

Sikiliza

 

16 July 2018, 16:26