Beta Version

Cerca

Vatican News
The Te Deum (© Biblioteca Apostolica Vaticana)

Utenzi wa sifa na shukrani, Te Deum

Tunakusifu wewe, Mungu:
tunakukiri kuwa Bwana.
Dunia yote inakukiri,
Baba wa milele.
Malaika wote,
nao wote wenye mamlaka,
makerubi na maserafi,
wanakuimbia wewe wasikome:
Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu,
Bwana, Mungu wa majeshi.
Mbingu na dunia zimejaa,
ukuu wa utukufu wako.
Kwaya tukufu ya mitume,
idadi sifiwa ya manabii,
jeshi safi la wafiadini vinakusifu wewe.
Duniani kote Kanisa takatifu linakukiri,
Baba wa ukuu usio na mipaka;
Mwanao halisi na pekee,
anayestahili kuabudiwa;
na Roho Mtakatifu mfariji.
Wewe Kristo, ni mfalme wa utukufu.
Ni mwana wa milele wa Baba.
Ili kuokoa binadamu,
hukusita kutwaa utu tumboni mwa Bikira.
Kwa kushinda mauti,
umewafungulia waamini ufalme wa mbinguni.
Umeketi kuumeni mwa Mungu,
katika utukufu wa Baba.
Unasadikiwa ndiye Hakimu ajaye.
Basi tunakuomba wewe,
utusaidie watumishi wako,
uliotukomboa kwa damu azizi.
Utujalie tuhesabiwe kati ya watakatifu,
katika utukufu wa milele.
Uliokoe taifa lako, Bwana,
na kubariki urithi wako.
Utuongoze na kutulinda hata milele.
Kila siku tunakuhimidi;
tunasifu jina lako daima na milele.
Kwa huruma yako, Bwana,
utukinge leo na dhambi yoyote.
Uturehemu, Bwana,
uturehemu sisi.
Huruma yako, Bwana, iwe juu yetu,
kwa kuwa tumekutumainia wewe.
Ndiwe tumaini letu, Bwana:
tusiaibike milele.