Papa Francisko:Yesu ni mwokozi,mwanga na ishara ya kupingana!
Na Angella Rwezaula – Vatican
Baba Mtakatifu Francisko tarehe 2 Februari 2025, Mama Kanisa akiwa anaadhimisha Siku kuu ya Kutolewa kwa Bwana Hekaluni, Sanjari na Siku ya Watawa Ulimwenguni, akiwa katika dirisha la Jumba la kitume mjini Vatican, alitoa tafakari yake kwa waamini na mahujaji waliounganika katika uwanja wa Mtakatifu Petro, mjini Vatican kabla ya Sala ya Malaika wa Bwana. Kwa kuongozwa na Injili ya Siku, Baba Mtakatifu Francisko alisema kuwa: “ Injili ya Liturujia (Lk 2:22-40) ya leo inatuambia kuhusu Maria na Yosefu ambao walimpeleka mtoto Yesu kwenye Hekalu la Yerusalemu. Kulingana na Sheria wanamwasilisha katika makao ya Mungu, ili kutukumbusha kwamba uzima unatoka kwa Bwana. Na wakati Familia Takatifu inafanya kile ambacho watu wa Israeli wamekuwa wakifanya kila wakati, kutoka kizazi hadi kizazi, kitu kinatokea ambacho hakijawahi kutokea hapo awali.”
Wazee wawili Simeoni na Anna, walitabiri kuhusiana na Yesu: wanamsifu Mungu na kusema juu ya mtoto “kwa wote waliokuwa wakitazamia ukombozi wa Yerusalemu” (Lk 2, 38). Sauti zao za kusisimua zinasikika kati ya mawe ya kale ya Hekalu, zikitangaza utimilifu wa matarajio ya Israeli. Mungu yuko kweli kati ya watu wake: si kwa sababu anaishi ndani ya kuta nne, lakini kwa sababu anaishi kama mwanadamu kati ya wanadamu. Haya ni mapya ya Yesu… Katika uzee wa Simeoni na Anna, kitu kipya kinatokea ambacho kinabadilisha historia ya ulimwengu. Kwa upande wao, Maria na Yosefu “walishangazwa na maneno waliyokuwa wanasikia ”kuhusu Yesu(Lk 2, 33). Kiukweli, Simeoni alipomchukua mtoto, anamwita kwa njia tatu nzuri, ambazo zinastahili kutafakari. Papa aliongeza “Kwa njia tatum na majna matatu anampatia: Yesu ni wokovu; Yesu ni nuru; Yesu ni ishara ya kupingana.
Kwanza kabisa, Yesu ni wokovu. Simeoni alisema hivi, akimwomba Mungu: “Macho yangu yameuona wokovu wako, uliouweka tayari machoni pa mataifa yote” (Lk 2: 30-31). Hii daima inatushangaza: wokovu wa ulimwengu wote umejilimbikizia katika moja! Ndiyo, kwa sababu ndani ya Yesu unakaa utimilifu wote wa Mungu, wa Upendo wake (taz Kol 2:9).
Kipengele cha pili: Yesu ni “mwanga wa ufunuo kwa Mataifa”(Lk 2,32). Kama jua likichomoza juu ya ulimwengu, mtoto huyu atamkomboa kutoka katika giza la uovu, maumivu na kifo. Tunahitaji mwanga huu kiasi gani, hata leo!
Hatimaye, mtoto aliyekumbatiwa na Simeoni ni ishara ya kupingana “ili mawazo ya mioyo mingi yafunuliwe” (Lk 2,35). Yesu anafunua kigezo cha kuhukumu historia yote na maagizo yake, na pia maisha ya kila mmoja wetu. Na hiyo ni kigezo gani hiki? Ni upendo: anayependa anaishi, anayechukia hufa. Yaani Yesu ni mwokozi, Yesu ni mwanga na Yesu ni ishara ya kupingana.
Kwa kuangazwa na kukutana huku na Yesu, basi tunaweza kujiuliza: Mimi, wewe, ninatazamia nini maishani mwangu? Tumaini langu kubwa ni nini? Moyo wangu unatamani kuuona uso wa Bwana? Je, ninangoja udhihirisho wa mpango Wake wa wokovu kwa wanadamu? Tusali pamoja na Maria, Mama safi kabisa, ili atusindikize katika mwanga na katika giza za historia kukutana na Bwana.